NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO
MKUU wa Wilaya
ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa amewaonya vikali baadhi ya dereva
pamoja na makondakta wenye tabia ya kutupa taka ovyo katika eneo la stendi
ya mabasi madogo kwani kufanya hivyo kunasababisha uchafuzi wa
mazingira na kunaweza kupelekea kuleta madhara makubwa ya kuibuka kwa mlipuko
wa magonjwa mbalimbali ikiwemo kipindupindu.
Kawawa, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuhusiana na changamoto za usafi wa mazingira katika baadhi ya maeeno pamoja na
mipango endelevu waliyojiwekea katika kuthibiti hali ya mlipuko wa magonjwa
mbali mbali pamoja na kuhakikisha kwamba sehemu zote zinakuwa katika hali ya
usafi katika kipindi chote.
“Kitu kikubwa ambacho ninawaasa baadhi ya madereva ambao
wamekuwa wakivunja taratibu ambazo tumeziweka katika kuhakikisha kwamba suala
la usafi wa mazingira linazingatiwa kwa kiasi kikubwa hivyo nimarufuku kabisa
kutupa takataka ovyo katika eneo la stendi yetu pamoja na maeneo mengine hii ni
kwa ajii ya manufaa ya wananchi wote wa Wilaya ya bagamoyo na watu wengine
wanakuja kwa ajili ya kutembelea vivutio vilivyopo,”alisema Kawawa.
Pia, katika hatua nyingine aliongeza kuwa madereva hao kwa sasa
wanapaswa kubadilika kwa kufanya usafi katika sare zao ambazo wanakuwa
wakizitumia ili waweze kuwa safi na kwamba wahakikishe wanaweka utaratibu mzuri
katika gari zao la kuwa na sehemu au kifaa kwa ajili ya kuweza kuwapa fura
abiria waweze kuhifadhi takataka pindi wanapokuwa katika safari.
“Mara nyingine unaweza kukuta abiria wengine wananunua vitu
njiani kwa ajili ya kuweza kula lakini sasa kutokana na gari husika kutokuwa na
sehemu ya kutupia taka wanaamua kutupia dirishani hii nayo ni changamoto kubwa
na pia inafanya mazingira kuonekana machafu na kwa hali hiyo ni hatari sana kwa
usalama wa afya za wananchi hasa katika kipindi cha mvua
zinaponyesha,”aliongezea Kawawa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo aliwawakumbusha wananchi wa
Bagamoyo kwa ujumla kuendelea kutimiza Agizo la Makamu wa Rais Mama Samia
Suluhu la kufanya usafi katika maeneo mbalimbali kila jumamosi ya mwisho wa
mwezi ili kuboresha zaidi mazingira na kuthibiti mlipuko wa magonjwa ambayo
yanaweza kujitiokeza kutokana na kukithiri kwa uchafu.

No comments:
Post a Comment