Breaking News

Feb 22, 2021

CHAMA CHA SOKA MKOA WA PWANI CHAPATA VIONGOZI WAPYA,DAS AONGEZA HAMASA

 

KATIBU TAWALA WILAYA YA BAGAMOYO,KASILDA MGENI AKIWASA WADAU WA MICHEZO

                

NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO

CHAMA cha soka Mkoa wa Pwani (COREFA), kimepata safu yake mpya ya uongozi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Wilayani Bagamoyo ambapo katika nafasi ya Mwenyekiti imechukuliwa na Othuman Hassan Hassanoo kwa kuibuka na ushindi  kwa kupata kura 15 akifuatiwa na mpinzani wake Robert Munisi ambaye alipata kura 14 kati ya 32 zilizopigwa.

Katika  uchaguzi huo ambao ulikuwa wa vuta ni kuvute na ushindani mkali ukiringanisha na chaguzi nyingine zilizopita, uliweza kusimamiwa na Shirikisho la soka Tanzania (TTF) chini ya  Mwenyekiti wa uchaguzi huo Kiomoni Kibamba ambaye aliweza kuendesha zoezi hilo kwa kuzingatia sheria na taratibu zote za mchezo wa soka.

Mwenyekiti huyo mpya wa Corefa, amefanikiwa kutetea  kiti  chake katika  kivumbi hicho cha uchaguzi aliweza kupata kura  15 za ndiyo, na kura 14 za hapana huku kura tatu zikiwa zimeharibika huku mpinzani wake wa karibu Robert Munisi alipata kura 14 za ndiyo huku kura 15 za hapana na tatu zikiharibika.

MWENYEKITI WA CHAMA CHA SOKA MKOA WA PWANI,OTHMAN HASSAN HASANOO (KULIA) AKITOA NENO BAADA YA KUCHAGULIWA KUSHIKA NAFASI HIYO

Upande wa nafasi ya Makamu mwenyekiti ilinyakuliwa na Ibrahim Gama ambaye alijizolea kura 23, huku nafasi ya Katibu Mkuu ikienda kwa mwandishi wa michezo wa zamani wa Gazeti la Tanzania daima Athuman Masenga aliyepata kura 15 huku mpinzani wake  Frorence Ambonisye akipata kura 14.

Kwa upande wa nafasi ya Katibu Msaidizi ilikwenda kwa Hafidhi Konyamale aliyepata kura 17 huku mpinzani wake Charles Ndagala akijinyakulia kura 12 ambapo nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu ikienda kwa Priscus Miyangu aliyepata kura 11, nafasi ya Mweka hazina ikienda kwa Mohamed Ally aliyepata kura 18 na mpinzani wake Bernard Yombayomba akipata kura 11.

Katika nafasi ya Mwakilishi wa vilabu ilinyakuliwa na mtangazaji kutoka shirika la utangazaji TBC, Jesse John ambaye aliibuka kidedea baada ya kuinyinyakulia kura 18, huku mpinzani wake Ramadhani Lukanga  akiambulia kura 10.

Kwa upande wa nafasi Kamati ya utendaji,  zilinyakuliwa na Siman Mbelwa, Godfrey Haule, pamoja an Abdul Pyala, ambapo kwa wawakilishi wa soko la wanawake ilikwenda kwa Faraja Makale.

Naye,  Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni  ambaye alikuwa Mgen rasmi katika uchaguzi huo, aliwapongeza viongozi wapya waliochaguliwa na kuwataka kuungana kwa pamoja katika kukuza mchezo wa soka ndani ya Mkoa wa Pwani sambamba na kuelekeza nguvu zao katika kuisaidia timu ya Bagafriends ambayo  ni mabingwa wa ligi daraja la tatu ngazi ya Mkoa.

Aliutaka Uongozi wa chama cha soka kuhakikisha kwamba inawekeza zaidi katika kuzisaidia timu mbalimbali za soko ambazo zinakuwa zikiwakilisha katika michuano mbalimbali ili ziweze kufanya vizuri na kuuletea heshima Mkoa wa Pwani katika sekta ya michezo.

Aidha Mgeni aliongeza kuwa vyama  vya soka husika vinatakiwa kuweka mikakati endelevu katika kuanzia programu maalumu kwa ajili ya kukuza vipaji kwa wachezaji wadogo pamoja na kuzipandisha daraja timu mbali mbali ambazo zinashiriki katika ligi tofauti.

“Kikubwa ninachowaomba viongozi tusigeuze changamoto ya timu zetu kwa lengo la kuweza kujinufaisha sisi wenyewe na kwamba wahakikishe wanashirikiana na wadau wa mchezo wa soko katika kuwekeza nguvu zao katika kuzisaidia timu amabzo zinakuwa zinawakilisha Mkoa ili wachezaji waweze kucheza katika mazingira ambayo ni rafiki,”alisema Mgeni.

No comments:

Post a Comment