Breaking News

Sep 1, 2026

MWANAMKE MOROGORO MBARONI KWA TUHUMA YA MAUAJII YA MUMEWE

MWANAMKE MOROGORO MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA MUMEWE

Na Thadei Hafigwa

JESHI la Polisi mkoa wa Morogoro limemtia mbaroni,Mwanamke Jobita Bategeuye Budyo(30) mkazi wa Maafisa,Manispaa ya Morogoro kwa tuhuma ya mauji ya mume Abeli Charles(44) kwa kile kinachodaiwa ni kutokana na mapenzi.

inaelezwa kuwa kabla ya kifo kulitokea kama mabishano ya wanandoa wakati wa maandalizi ya chakula, 

Kutokana na hali hiyo ikasababisha  tukio la kusikitisha baada ya mwanaume mwenye umri wa miaka 44 kupoteza maisha katika mazingira yanayodaiwa kuhusishwa na mgogoro wa kifamilia katika eneo la Mafisa, Manispaa ya Morogoro.

Abeli Charles wakati wa uhai wake,alikuwa. ni mfanyabiashara, huku mtuhumiwa akitajwa kuwa ni fundi cherehani na mkazi wa eneo hilo.

Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa Agosti 31, 2026, nyumbani kwa wanandoa hao, baada ya mazungumzo yao kubadilika na kuwa mabishano makali yaliyodaiwa kuhusishwa na masuala ya unyumba.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, mabishano hayo yaligeuka kuwa ugomvi, ambao baadaye ulipelekea Abeli Charles kupata majeraha makubwa katika maeneo ya shingoni na kichwani na kusababisha kifo chake.

Kamanda Kantimbo amesema, kwa mujibu wa taarifa za awali za uchunguzi, mtuhumiwa anadaiwa kutumia kitu chenye ncha kali kumshambulia na kumjeruhi marehemu, ambaye baadaye alipoteza maisha kutokana na majeraha aliyoyapata.

“Chanzo cha awali cha tukio hilo kinahusishwa na mgogoro wa kifamilia unaodaiwa kuchochewa na masuala ya unyumba,” amesema Kamanda Kantimbo, huku akibainisha kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kubaini mazingira yote ya tukio hilo.

Jeshi la Polisi linamshikilia Jovita kwa ajili ya uchunguzi zaidi kabla ya kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria kulingana na matokeo ya uchunguzi.

Tukio hilo limeibua tena mjadala kuhusu namna migogoro ya kifamilia inavyoweza kugeuka kuwa matukio ya ukatili pale ambapo wahusika wanashindwa kutumia mazungumzo, uvumilivu na njia nyingine za amani kutatua tofauti zao.

Kamanda Kantimbo ametoa wito kwa wanandoa na familia kwa ujumla kuepuka matumizi ya nguvu katika kushughulikia migogoro, akisisitiza umuhimu wa kutafuta msaada kutoka kwa ndugu, viongozi wa jamii, viongozi wa dini au mamlaka nyingine zinazohusika kabla ya migogoro kufikia hatua ya kuhatarisha maisha.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kwa wakati kuhusu matukio ya ukatili na viashiria vya migogoro inayoweza kuhatarisha usalama wa watu.

Amesema ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kuzuia matukio ya uhalifu na kulinda makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, yakiwemo wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu. 

TMA YAHADHARISHA MVUA YA EL-NINO

 


Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya hali ya hewa imeendelea kutoa tahadhari ikiwataka wananchi kuchukua hatua za mapema kukabiliana na El-Nino ambayo wamekuwa wakiifuatilia kwa ukaribu zaidi ikitajwa kuwa kubwa kati ya zilizowahi kutokea.

Kwa muujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), DR. Ladislaus Chang’a, Amesema katika historia baadhi ya El-Nino ambazo zilikuwa na nguvu kubwa ni ya 1982 -1983, 1997-1998, 2015-2016, na 2023-2024 na hii ambayo wanaendelea kuifuatilia 2026 tayari imefikia kiwango cha El Nino yenye nguvu kubwa kuelekea Oktoba itakuwa na nguvu kubwa zaidi.

Ametaja baadhi ya maeneo ambayo yataathirika kupata mvua za juu ya wastani ni pamoja na mikoa ya ukanda wa ziwa Viktoria (Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara), mvua zikitarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi septemba.

Ukanda wa nyada za Juu Kaskazini Mashariki (Kilimanjaro, Arusha na Manyara) ametaja kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani mvua zikitarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, visiwa vya Mafia) yatarajiwa kupata mvua za juu ya Wastani hadi wastani).

TANZANIA NA UJERUMANI ZAIMARISHA USHIRIKIANO UHIFADHI WA BIOANUWAO



Tanzania na Ujerumani Zaimarisha Ushirikiano wa Uhifadhi wa Bioanuwai

Na Mwandishi wetu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi akiwa na Mwenyekiti Mwenza ambaye ni Mkuu wa Ushirikiano katika Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bi. Julia Kronberg wameongoza Kikao cha 13 cha Kamati ya Uendeshaji Steering Commitee) wa Miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Ujerumani na Tanzania.

Kikao hicho kimepokea na kujadili  taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya maendeleo ya Ujerumani (KFW). Miradi hiyo inatekelezwa katika maeneo ya ikolojia za Serengeti, Katavi, Mahale na Selous Nyerere. 


Vilevile kikao hicho kimejadili  masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani katika uhifadhi wa bioanuwai, usimamizi endelevu wa rasilimali za asili na kulinda mifumo ya ikolojia nchini.

Ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuhakikisha utajiri wa bioanuwai wa Tanzania unaendelea kulindwa na kutumika kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kikao hicho kimefanyika leo Septemba 1, 2026 katika Chuo cha Utalii jijini Dar es salaam.

Aug 30, 2026

PURA WATOA UFAFANUZI KUHUSU UTAFUTAJI WA MAFUTA, GESI ASILIA


PURA WATOA UFAFANUZI  KUHUSU UTAFUTAJI WA MAFUTA, GESI ASILIA

Na Thadei Hafigwa

WANANCHI mkoani Morogoro wameonyesha shauku kubwa ya kupata taarifa sahihi kuhusu shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini, huku wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) wakitoa ufafanuzi kuhusu hatua iliyofikiwa katika utafutaji wa rasilimali hizo.

Shauku hiyo imejitokeza wakati wa Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika mkoani Morogoro, ambapo wananchi waliotembelea banda la PURA waliuliza maswali kuhusu uwepo wa mafuta nchini, shughuli za utafutaji zinazoendelea na uwezekano wa kuanza uzalishaji wa mafuta iwapo yatathibitishwa kuwepo kwa kiwango kinachoweza kuendelezwa kibiashara.

Baadhi ya wananchi walitaka kufahamu iwapo tayari Tanzania imethibitisha uwepo wa mafuta na ni lini shughuli za uchimbaji zinaweza kuanza.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha tamasha hilo, Mjiolojia kutoka PURA, Lukelo Matimbwi, alisema shughuli za utafutaji wa mafuta bado zinaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kubaini uwepo na kiwango cha rasilimali hiyo.

Matimbwi alisema Tanzania tayari imebaini uwepo wa gesi asilia, huku shughuli za utafutaji wa mafuta zikiendelea kwa kutumia tafiti na teknolojia zinazotumika katika sekta ya petroli.

“Bado kuna tafiti na shughuli za utafutaji zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini ili kubaini uwepo na kiwango cha rasilimali za mafuta,” alisema Matimbwi.

Alisema hatua za utafutaji zinahitaji tafiti za kitaalamu na tathmini mbalimbali kabla ya kufikia hatua ya kuthibitisha uwepo wa rasilimali inayoweza kuendelezwa.

Matimbwi pia alieleza kuwa PURA inatumia fursa kama tamasha hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake katika kusimamia na kudhibiti shughuli za mkondo wa juu wa petroli.

Kwa mujibu wa Matimbwi, shughuli hizo zinahusisha mchakato wa utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia.

CHIFU LUKWELE AIPONGEZA PURA

Kwa upande wake, Chifu Lukwele wa Morogoro amezipongeza taasisi za serikali na wataalamu walioshiriki katika tamasha hilo kwa kutumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zao na tafiti zinazofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.

Chifu Lukwele alisema ushiriki wa taasisi hizo ni muhimu kwa sababu unawawezesha wananchi kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu shughuli zinazofanywa na serikali na wataalamu katika sekta mbalimbali.


“Niipongeze sana PURA kwa kuweka banda lao katika tamasha hili, ambapo wananchi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu shughuli mbalimbali wanazofanya,” alisema.

Alisema viongozi wa mila na Machifu wataendelea kushirikiana na serikali pamoja na wataalamu na watafiti watakaofika katika maeneo yao kwa ajili ya shughuli za utafiti na maendeleo.

Chifu Lukwele alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kuhakikisha tafiti na shughuli nyingine za maendeleo zinafanyika kwa utaratibu unaozingatia maslahi ya wananchi na uhifadhi wa rasilimali na maliasili za taifa.

WANANCHI WATAKA ELIMU ZAIDI

Kwa upande wao, wananchi waliofika katika banda la PURA walitumia fursa hiyo kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia.

Maswali yao yalijikita zaidi katika hatua iliyofikiwa katika utafutaji wa mafuta, namna shughuli hizo zinavyosimamiwa na fursa ambazo sekta ya petroli inaweza kuzalisha kwa taifa endapo rasilimali hizo zitagundulika na kuendelezwa kibiashara.

Ushiriki wa PURA katika Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni umeongeza nafasi ya wananchi kupata elimu kuhusu sekta ya petroli nje ya majukwaa ya kitaalamu, huku ukitoa fursa kwa wataalamu kujibu maswali na kueleza taratibu zinazotumika katika utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia.

Tamasha hilo limeendelea kuwa jukwaa la taasisi mbalimbali za serikali na wadau kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma, tafiti na fursa zinazohusiana na maendeleo ya taifa.

MACHIFU WASISITIZA KUHIFADHI URITHI WA MTANZANIA

 MACHIFU WASISITIZA KUHIFADHI URITHI WA MTANZANIA

Na Thadei Hafigwa

KATIBU wa Umoja wa Machifu Tanzania, Chifu Aron Nyamironda wa Pili kutoka mkoani Mwanza, amesema kuwa uamuzi wa serikali kwa kuwashirikisha Machifu katika tamasha la utamaduni i na kutambua mchango wao katika kurejesha, kuenzi na kuhifadhi mila na utamaduni wa Mtanzania.

Chifu Nyamironda amebainisha hayo kwa niaba ya wenzake wakati wa hafla ya kufunga tamasha hilo la nne la kitaifa lililofanyika mkoani Morogoro,aliongeza kuwa  moja ya majukumu ya Machifu ni kuhakikisha utamaduni wa Mtanzania unadumishwa na kurithishwa kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.

Chifu Nyamironda alisema wamefarijika kuona mwamko mkubwa wa vijana waliojitokeza kushiriki na kushuhudia tamasha hilo, jambo ambalo linaonesha bado kuna nafasi ya kuendeleza mila, desturi na utambulisho wa makabila mbalimbali nchini.

“Miongoni mwa majukumu yetu ni kuikumbusha jamii, kwa vitendo, historia na asili ya Mtanzania, alikotoka na anakokwenda, lakini pia kushiriki katika utunzaji wa maeneo na vitu vya kihistoria kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema.

Awali, akitoa salamu za Mkoa wa Morogoro, mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa, Sebastian Waryuba, alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kutunza amani na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha mshikamano na utulivu wa nchi.

Ramadhan Divunyagale,Mwenyekiti wa Mila na Desturi Mkoa wa Morogoro(SHIWAMILA) amesema kuwa wazee wa Mkoa wa Morogoro watahakikisha ya kuwa maadili kwa vijana na 

MSIGWA: MAADILI NA UTAMADUNI VIKO HATARINI

 MAADILI NA UTAMADUNI VIKO HATARINI
 

Na Thadei Hafigwa

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili, hali ambayo imeifanya serikali kutoa nafasi kubwa kwa viongozi wa kimila, wakiwemo Machifu, kushiriki katika juhudi za kusimamia na kuenzi maadili na utamaduni wa Mtanzania.

Msigwa, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, alisema hayo Agosti 29, 2026, wakati akifunga Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika katika Viwanja vya Jamhuri mkoani Morogoro.

Tamasha hilo liliwakutanisha vikundi vya ngoma za asili kutoka mikoa mbalimbali nchini, sambamba na maonesho ya vyakula, mavazi na bidhaa nyingine za asili.

Alisema kasi ya utandawazi na maendeleo ya teknolojia imeleta changamoto katika uhifadhi wa utamaduni wa Tanzania, hivyo kuwepo kwa umuhimu wa jamii, viongozi wa kimila na vyombo vya habari kushirikiana kuhakikisha mila, desturi na maadili mema yanaendelea kuhifadhiwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

Msigwa aliwataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao katika kukuza na kutangaza utamaduni wa Tanzania, akisisitiza kuwa utamaduni unaweza kuwa chanzo muhimu cha fursa za kiuchumi kwa wananchi.

“Leo hii nchini kwetu kijana mdogo kumtukana mtu mzima inaonekana ni kitu cha kawaida. Mimi ni baba na mtoto wangu wa kwanza ana umri wa miaka 25, lakini cha kusikitisha ni kwamba anashuhudia watoto wadogo wakinitukana mitandaoni,” alisema Msigwa.

Katika kuelezea changamoto za matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, Msigwa alisema hata yeye amewahi kukumbana na taarifa za uongo zilizosambazwa mitandaoni kuhusu familia yake.

Alisema wakati akiwa njiani kuelekea kwenye tamasha hilo alipokea jumbe nyingi za pole baada ya kusambaa kwa taarifa za uongo zilizodai kuwa mama yake amefariki dunia.

“Hata nilipokuwa nakuja hapa nilikuwa napokea pole nyingi kwa sababu kuna watu wameandika mitandaoni kuwa mama yangu amefariki. Nataka niwaambie kuwa mama yangu hajafa, ni mzima wa afya na yupo kijijini Iringa anaendelea na shughuli zake kama kawaida,” alisema.

Msigwa alisema moja ya dhamira ya serikali ni kuhakikisha utamaduni wa Mtanzania unarithiwa na vizazi vya sasa na vijavyo kwa kuwa unafundisha misingi ya kuheshimiana, kusaidiana na kupendana.

“Maadili na malezi yanaanzia nyumbani, hivyo niwaombe Watanzania tuwe waangalifu na maudhui yanayotangazwa au kuchapishwa mitandaoni,” alisema.

Aidha, aliwataka wadau wa utamaduni kujenga mazingira yatakayowezesha bunifu mbalimbali kustawi na kutumika kama sehemu ya kukuza uchumi wa wananchi.

Kupitia tamasha hilo, Msigwa pia aliwakumbusha Watanzania kujielekeza katika kutafuta na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, hususan kuelekea matukio makubwa yatakayofanyika nchini, ikiwemo mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Aug 29, 2026

ELIMU YA MAFUTA NA GESI ASILIA YAWAVUTIA WANANCHI MOROGORO

 

 ELIMU YA MAFUTA NA GESI ASILIA YAWAVUTIA WANANCHI MOROGORO

 Na Thadei Hafigwa

WANANCHI waliofika kutembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) katika Tamasha la Nne la Taifa la Utamaduni mkoani Morogoro wameonyesha shauku kubwa ya kupata elimu kuhusu shughuli za utafutaji, uchimbaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia nchini.

Shauku hiyo ilijitokeza baada ya wananchi mbalimbali kufika katika banda hilo na kuuliza maswali kuhusu uwepo wa mafuta nchini, hatua zilizofikiwa katika utafutaji wa rasilimali hiyo pamoja na lini Tanzania inaweza kuanza kunufaika na uchimbaji wa mafuta.


Baadhi ya wananchi hao,ni Charles Pangapanga,Mkulima wa skimu ya Umwagiliaji Mvomero abaye alihoji iwapo tayari kuna uhakika wa uwepo wa mafuta nchini na ni lini shughuli rasmi za uchimbaji zinaweza kuanza.

Mjiolojia kutoka PURA, Lukelo Matimbwi, alisema kuwa bado kuna tafiti na shughuli za utafutaji zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini ili kubaini uwepo na kiwango cha rasilimali za mafuta.

Alisema kuwa hadi sasa, Tanzania imefanikiwa kubaini uwepo wa gesi asilia, huku uchunguzi na tafiti za kutafuta mafuta zikiendelea kwa mujibu wa taratibu na teknolojia zinazotumika katika sekta ya petroli.

Matimbwi alieleza kuwa elimu inayotolewa na PURA inalenga kuwawezesha wananchi kuelewa nafasi ya mamlaka hiyo katika kusimamia na kudhibiti shughuli za mkondo wa juu wa petroli, zikiwemo shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia.

Aidha, wananchi waliofika katika banda hilo walipata fursa ya kuuliza maswali na kujifunza zaidi kuhusu rasilimali za mafuta na gesi asilia pamoja na mchango wake unaotarajiwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Tamasha la Nne la Taifa la Utamaduni, linaloendelea katika Viwanja vya Jamhuri mkoani Morogoro, limeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi mbalimbali za serikali na wadau wengine kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu, huduma na fursa zinazopatikana katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake,Chifu wa Morogoro,Musa Lukwele amezipongeza Taasisi za serikali ambazo zimeshiriki katika Tamasha la Utamaduni limefanya uamuzi wa kizalendo,na kutoa elimu huduma wanazotoa kwa wananchi,na tafiti mbalimbali zinazofanywa na wataalamu katika kuharakisha maendeleo ya nchi.

Chifu Lukwele,alisema kuwa Machifu na Wazee wa Mila,pamoja na majukumu yao mengine wataendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na watafiti watakapofika maeneo yao ya kiutawala ili kusipatwe vikwazo katika majukumu yao ya kuwaletea maendeleo yao.

Aug 23, 2026

MVOMERO DC YAANZA KUTIKISA SHIMISEMITA MBEYA

MVOMERO DC YATIKISA SHIMISEMITA MBEYA, PROF. SHEMDOE ATOA ONYO KALI DHIDI YA UDANGANYIFU

Na Mwandishi wetu

Viongozi, watumishi na wachezaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wameshiriki katika ufunguzi rasmi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA), yanayofanyika jijini Mbeya.

Ufunguzi wa mashindano hayo umefanyika leo, Agosti 23, 2026, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, huku mgeni rasmi akiwa Prof. Riziki Silas Shemdoe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Prof. Shemdoe amewataka washiriki wote kuzingatia kikamilifu kanuni, taratibu na sheria zinazoongoza mashindano hayo, akisisitiza umuhimu wa michezo kuendeshwa kwa haki, uadilifu na ushindani wa kiungwana.

Prof. Shemdoe ametoa onyo kali dhidi ya udanganyifu katika michezo, akisema timu au mchezaji yeyote atakayebainika kukiuka taratibu na kufanya udanganyifu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za mashindano, ikiwemo kufutiwa matokeo.

“Michezo inapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu. Hakutakuwa na nafasi ya udanganyifu. Timu au mchezaji atakayebainika kufanya udanganyifu atachukuliwa hatua, ikiwemo kufutiwa matokeo,” amesema Prof. Shemdoe.

Aidha, Prof. Shemdoe ameeleza kuwa SHIMISEMITA ni jukwaa muhimu la kuimarisha afya, ustawi, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa Serikali za Mitaa, sambamba na kutoa fursa kwa watumishi kuonesha vipaji vyao katika michezo mbalimbali.

Katika mashindano hayo, watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wanashiriki katika michezo mbalimbali kwa lengo la kuonesha uwezo, vipaji na ushindani, huku wakilenga kuiwakilisha vyema Halmashauri yao na kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Ushiriki wa Mvomero DC pia unalenga kuimarisha uhusiano na mshikamano miongoni mwa watumishi, pamoja na kutumia michezo kama sehemu ya kujenga afya bora na kuongeza morali ya utendaji kazi.

Kaulimbiu hiyo inaendana na maandalizi ya Tanzania kuelekea kuwa sehemu ya wenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambayo itafanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.

TAMASHA LA NNE LA KITAIFA LA UTAMADUNI KUFANYIKA MOROGORO AGOSTI 25


Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni Morogoro Kuanza Agosti 25

Na Mwandishi wetu

MOROGORO inatarajia kuwa mwenyeji wa Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni, litakalofanyika kuanzia Agosti 25 hadi 29, 2026, likiwa na lengo la kuendeleza, kutangaza na kuhifadhi utamaduni wa Tanzania pamoja na kufungua fursa za kiuchumi kupitia sekta ya utamaduni na sanaa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, tamasha hilo linatarajiwa kukutanisha wadau mbalimbali wa utamaduni, wasanii, wabunifu, wazalishaji wa vyakula vya asili pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Tamasha hilo litakuwa na burudani na shughuli mbalimbali zitakazolenga kuonyesha utajiri wa mila, desturi, sanaa na vipaji vya Watanzania.

Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni burudani za ngoma za asili, visasili na visakale, pamoja na maonesho ya vyakula vya asili kutoka makabila mbalimbali nchini.

Aidha, kutakuwa na mashindano ya vyakula vya asili na ngoma za asili, hatua inayolenga kuwahamasisha wananchi, hasa vijana, kuendelea kujifunza na kuthamini urithi wa kitamaduni wa Tanzania.

Mbali na burudani na uhifadhi wa mila na desturi, tamasha hilo linatarajiwa kutoa nafasi kwa wadau kujadili namna ambavyo utamaduni unaweza kuwa chanzo cha ajira, biashara na kipato kwa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kutakuwa na mdahalo wa Maadili pamoja na Kongamano la Kitaifa la fursa za kiuchumi zinazotokana na shughuli za Utamaduni na Sanaa, sambamba na maonesho ya filamu.

Kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kujadili namna wasanii, wabunifu, wajasiriamali na vijana wanavyoweza kutumia vipaji na rasilimali za kitamaduni kujenga shughuli endelevu za kiuchumi.

Tamasha hilo pia litatoa nafasi kwa wananchi kutembelea vivutio vya utalii na kiutamaduni vilivyopo Morogoro, hatua inayoweza kuongeza uelewa kuhusu utajiri wa Mkoa wa Morogoro katika eneo la utalii, historia na utamaduni.

Kwa upande wa burudani za usiku, ratiba inaonesha kuwa kutakuwa na Usiku wa Taarabu na Muziki wa Kale, utakaotoa fursa kwa wananchi kufurahia muziki wa kizazi cha zamani huku wakikumbushwa nafasi ya muziki huo katika historia na utamaduni wa Tanzania.

Kwa kufanyika kwa tamasha hilo Morogoro, mkoa huo unapata fursa ya kuendelea kujitambulisha kama moja ya maeneo muhimu nchini katika uhifadhi wa utamaduni, sanaa na urithi wa Taifa.

Tamasha hilo pia linaweza kuwa fursa kwa wafanyabiashara wadogo, wasanii, wajasiriamali, wazalishaji wa bidhaa za asili na sekta ya utalii kupata masoko mapya na kujenga mitandao ya kibiashara.

Wananchi na wadau wa utamaduni wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli hizo, huku msisitizo ukiwa katika kulinda, kuendeleza na kutumia utamaduni kama nyenzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni Morogoro linafanyika kuanzia Agosti 25 hadi 29, 2026, likiwa limebeba ujumbe wa kuunganisha utamaduni, sanaa, utalii na fursa za kiuchumi kwa maendeleo ya wananchi.

TANZANIA IMEANDIKA HISTORIA MPYA UZINDUZI WA MRADI WA KUFUA UMEME MW 2,115

JNHPP ya MW 2,115 Yazinduliwa Rasmi na Rais Samia

Na Mwandishi wetu

TANZANIA imeandika ukurasa mpya katika historia ya sekta ya nishati baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzindua rasmi Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.

Uzinduzi huo unaashiria kukamilika kwa moja ya miradi mikubwa na kimkakati ya Taifa katika kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme na kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa wananchi na shughuli za kiuchumi.

Mradi huo uliotekelezwa katika eneo la Mto Rufiji umejengwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme nchini, kupunguza changamoto za upungufu wa nishati na kuweka msingi imara wa kukuza shughuli za viwanda, biashara, kilimo na huduma mbalimbali.

Uzinduzi wa JNHPP unatajwa kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa uhakika unaoweza kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa uchumi na idadi ya watu.

Kwa wananchi, kukamilika kwa mradi huu ni zaidi ya kuongeza megawati kwenye gridi ya Taifa; ni hatua inayotarajiwa kuchochea uwekezaji, kuongeza uzalishaji, kuimarisha huduma za kijamii na kutoa mazingira bora kwa wafanyabiashara na wazalishaji.

Tukio hilo la kihistoria limewafanya Watanzania kushuhudia hatua nyingine muhimu katika safari ya maendeleo ya sekta ya nishati nchini.


Aug 21, 2026

FEASSA YARIDHISHWA NA MAZINGIRA YA UWANJA WA JAMHURI MOROGORO


FEASSA YARISHWA NA MAZINGIRA YA UWANJA WA JAMHURI MOROGORO 

Na Mwandishi wetu

 Uongozi wa Shirikisho la Michezo ya Shule za Msingi na Sekondari Afrika Mashariki (FEASSA) umeipongeza Serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa maandalizi bora ya mashindano ya michezo ya shule za msingi na sekondari Afrika Mashariki yanayoendelea mkoani humo.

Pongezi hizo zilitolewa Agosti 20, 2026, wakati viongozi wa FEASSA wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo, Justus Kamugisha, na Katibu Mkuu, Ngugi David, walipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, ofisini kwake.

Viongozi hao walisema maandalizi yaliyofanywa na Mkoa wa Morogoro yamewezesha mashindano hayo kufanyika katika mazingira salama na yenye utulivu, huku wakibainisha kuwa ushirikiano kati ya kamati ya maandalizi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa umechangia kufanikisha mashindano hayo.

Akizungumza baada ya kupokea pongezi hizo, Mhe. Malima alisema Morogoro itaendelea kutoa ushirikiano kwa FEASSA na wadau wengine wa michezo, akisisitiza kuwa mkoa huo una fursa kubwa za kuendeleza michezo na kukuza vipaji vya vijana.

“Morogoro ina fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuboresha mazingira ya michezo na kuongeza aina mbalimbali za michezo inayofanyika mkoani hapa,” alisema Malima.

Alisema mkoa una maeneo makubwa yanayoweza kutumika kwa shughuli za michezo, hivyo kuna haja ya kutumia fursa hizo kwa ufanisi ili kuibua vipaji vipya na kuongeza ushiriki wa vijana katika michezo mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Michezo, Utamaduni na Sanaa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Yusuph Singo Omari, alisema mashindano hayo yamefungua fursa muhimu za kiuchumi kwa Tanzania na maeneo yanayowahudumia washiriki.

Singo alisema ujio wa maelfu ya washiriki na wageni kutoka nchi za Afrika Mashariki unatoa fursa kwa wafanyabiashara, hususan wanaofanya biashara za hoteli, usafirishaji, chakula na huduma nyingine, kuongeza shughuli zao za kiuchumi.

Mashindano hayo yaliyoanza Agosti 12, 2026, yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti 23, 2026, yakishirikisha zaidi ya wanafunzi 6,000 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Lengo la mashindano hayo ni kukuza na kuibua vipaji vya michezo miongoni mwa wanafunzi, huku yakitoa fursa kwa vijana kutoka nchi za Afrika Mashariki kukutana, kushindana na kujenga urafiki na mshikamano kupitia michezo.

Baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo mwaka huu, Kigali, Rwanda, inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya FEASSA mwaka 2027.

Aug 17, 2026

RAIS SAMIA KUZINDUA UMEME WA JNHPP AGOSTI 22,2026 RUFIJI

HISTORIA YAANDIKWA: JNHPP KUKAMILIKA, RAIS SAMIA KUZINDUA MRADI AGOSTI 22

Na Thadei Hafigwa

Hatimaye historia inaandikwa katika sekta ya nishati nchini Tanzania, baada ya Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kukamilika na kutarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Agosti 22, 2026, katika eneo la Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Mradi huo mkubwa wa kimkakati umejengwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme nchini, kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na kuweka msingi wa kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya viwanda.

Kwa kujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma unaeleza kuwa mafanikio ya mradi huo ni matokeo ya nguvu za Watanzania na matumizi ya mapato ya Serikali, ikiwemo kodi zinazolipwa na wananchi na wafanyabiashara.

Kauli ya “Kwa kodi zetu, historia imeandikwa!” imebeba ujumbe wa umuhimu wa ulipaji kodi katika kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa kwa taifa.

Uzinduzi wa JNHPP unatarajiwa kuwa tukio muhimu katika historia ya maendeleo ya nishati nchini, huku Watanzania wakisubiri kwa hamu kuona mradi huo ukianza kutoa mchango wake katika kuongeza uwezo wa Taifa wa kuzalisha umeme.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wananchi wametakiwa “kukaa tayari” kushuhudia tukio hilo litakalofanyika Rufiji Agosti 22, 2026.

Mradi wa JNHPP ni sehemu ya jitihada za Tanzania kujenga mfumo imara wa nishati unaoweza kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa uchumi, viwanda, biashara na ongezeko la matumizi ya umeme.

Uzinduzi huo pia unatarajiwa kutoa fursa ya kuangazia hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi, matarajio yake kwa uchumi wa Taifa na namna wananchi watakavyonufaika na ongezeko la upatikanaji wa umeme. 

Aug 14, 2026

CRDB YAIPA SAPOTI SEKTA YA MICHEZO

CRDB Gairo Yaipa Gairo Sports Club Msaada Kuelekea SHIMISEMITA 2026

Na Mwandishi wetu

Benki ya CRDB, Tawi la Gairo, imeunga mkono safari ya Gairo Sports Club kuelekea Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) 2026 kwa kukabidhi zaidi ya katoni 30 za maji kwa ajili ya timu zinazoiwakilisha Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.

Msaada huo umekabidhiwa Agosti 14, 2026 katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Gairo na Bi. Elialice Lema, Afisa Mikopo wa CRDB Tawi la Gairo, kwa niaba ya benki hiyo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bi. Lema amesema CRDB inatambua umuhimu wa kushirikiana na Serikali pamoja na jamii katika kusaidia shughuli zenye manufaa kwa wananchi, ikiwemo maendeleo ya michezo na kukuza vipaji.

Amesema mchango huo ni sehemu ya juhudi za CRDB kuendelea kuwa karibu na jamii na kushirikiana na wadau katika maeneo mbalimbali yenye mchango katika maendeleo ya wananchi.

Msaada huo wa maji unalenga kuwasaidia wanamichezo wa Gairo Sports Club katika kipindi cha maandalizi na ushiriki wao kwenye mashindano hayo, ambayo yanatarajiwa kuanza Agosti 16, 2026, jijini Mbeya.


Kwa upande wake, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo umeipongeza CRDB Tawi la Gairo kwa hatua hiyo, huku ukitoa wito kwa taasisi, wafanyabiashara na wadau wengine kuendelea kushirikiana na Halmashauri katika kuendeleza michezo na kukuza vipaji vya vijana.

Gairo Sports Club ni miongoni mwa timu zinazotarajiwa kushiriki SHIMISEMITA 2026, mashindano yanayowakutanisha watumishi kutoka Halmashauri mbalimbali nchini katika michezo mbalimbali.

Mchango wa CRDB unatajwa kuwa sehemu ya ushirikiano kati ya sekta ya fedha na taasisi za Serikali katika kuunga mkono michezo, ustawi wa watumishi na kukuza vipaji kupitia mashindano ya SHIMISEMITA 2026.

SARA FESTIVAL KUZINDULIWA AGOSTI 18,MZUMBE


Mbunge Sara Msafiri Awaalika Wananchi Mvomero kwenye Uzinduzi wa “Sara Festival”

Na Thadei Hafigwa

 Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Mhe. Sara Msafiri, anatarajiwa kuungana na wananchi katika hafla ya uzinduzi wa “Sara Festival”, inayolenga kuwakutanisha wananchi katika shughuli za burudani, michezo na burudani za kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mvomero, tamasha hilo litafanyika Jumanne, Agosti 18, 2026, katika Viwanja vya Changawe, Kata ya Mzumbe.

Tamasha hilo linatarajiwa kuwa sehemu ya shughuli za kijamii zitakazowapa wananchi fursa ya kukutana, kuburudika na kushiriki michezo mbalimbali, huku likibeba kaulimbiu isemayo “Tamasha Letu, Fahari Yetu.”

Taarifa hiyo inaeleza kuwa burudani mbalimbali zitakuwepo wakati wa tamasha hilo, huku wananchi wakitarajiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli zitakazofanyika.

Miongoni mwa michezo na burudani zinazoonekana kutangazwa katika tamasha hilo ni mpira wa miguu, muziki na ngoma za asili, pamoja na mbio, jambo linalolifanya tamasha hilo kuwa jukwaa la kuchanganya michezo, utamaduni na burudani.

Uzinduzi wa “Sara Festival” pia unatarajiwa kuongeza fursa ya wananchi wa maeneo mbalimbali ya Jimbo la Mvomero kukutana katika mazingira ya kijamii na kushirikiana kupitia michezo na burudani.

Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mvomero imewahimiza wananchi kujitokeza kushiriki katika tamasha hilo litakalofanyika katika Viwanja vya Changawe, Kata ya Mzumbe.

Kwa ujumla, “Sara Festival” inatarajiwa kuwa tukio litakaloweka pamoja michezo, burudani na utamaduni, huku wananchi wakipewa nafasi ya kushiriki na kufurahia shughuli mbalimbali katika siku hiyo.

GAIRO WAFUNGUA MNADA WA ZAO LA TUMBAKU


MNADA WA KWANZA WA TUMBAKU GAIRO WAFUNGUA SOKO LA TANI 117

Na Mwandishi wetu

Katibu Tawala wa Wilaya ya Gairo, Jeremia Mapogo, amezindua rasmi mnada wa kwanza wa zao la tumbaku kwa msimu wa 2025/2026, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za soko na kipato kwa wakulima wa wilaya hiyo.

Uzinduzi huo uliofanyika hivi karibuni umefungua umefungua rasmi mchakato wa uuzaji wa tumbaku kwa msimu huu, huku zaidi ya tani 117 za tumbaku zikiwa zimewasilishwa kwa ajili ya kuuzwa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa wakati wa uzinduzi huo, mauzo ya tumbaku hiyo yanatarajiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 600, fedha ambazo zitakwenda kuongeza kipato cha wakulima na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi katika maeneo yanayolima zao hilo.


Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Gairo inatarajiwa kukusanya zaidi ya Sh milioni 18 kutokana na ushuru unaotokana na zao hilo, hivyo kuongeza uwezo wa Halmashauri katika kutekeleza shughuli za maendeleo kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mnada huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Gairo, Jeremia Mapogo, alisisitiza umuhimu wa zao hilo katika kukuza shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato cha wananchi, huku akieleza umuhimu wa wakulima kuendelea kuzingatia ubora na kuongeza uzalishaji.

Mnada huo pia unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuwawezesha wakulima kupata soko rasmi la mazao yao, jambo linaloweza kuongeza uhakika wa mapato na kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la tumbaku wilayani Gairo.


Tumbaku imeanza kuchukua nafasi muhimu katika kilimo cha biashara wilayani Gairo baada ya kuanzishwa kwa kilimo cha majaribio katika msimu wa 2024/2025.

Matokeo yaliyopatikana katika msimu huo yameendelea kuimarisha uamuzi wa kuitambua tumbaku kama moja ya mazao ya biashara yenye umuhimu kwa uchumi wa wilaya hiyo.

Kwa kuingia katika msimu wa 2025/2026, wadau wa kilimo wanatarajia zao hilo kuendelea kutoa fursa kwa wakulima kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora na kunufaika zaidi na soko la zao hilo.

Wakati huo huo, ongezeko la shughuli za kilimo na biashara ya tumbaku linatarajiwa kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi, ikiwamo usafirishaji, biashara na huduma mbalimbali zinazohusiana na mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Kwa wakulima wa Gairo, kuanzishwa kwa minada rasmi ya tumbaku kunaonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha kilimo cha kibiashara na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa kaya na maendeleo ya Wilaya ya Gairo kwa ujumla. 

WAZIRI WA FEDHA JIWE LA MSINGI UJENZI WA OFISI TRA KIZIMKAZI




Waziri wa Fedha aweka jiwe la msingi ujenzi wa Ofisi ya TRA Kizimkazi ya Sh bilioni 3.6

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (MB), ameshiriki katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival), lililofikia tamati leo, Agosti 14, 2026, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Kilele cha tamasha hilo kimehudhuriwa na Mgeni Rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wadau wa maendeleo, wananchi na washiriki wa tamasha hilo.

Tamasha la Kizimkazi limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuenzi na kuendeleza tamaduni, sanaa na urithi wa Zanzibar, huku likitoa fursa ya kuimarisha mshikamano wa kijamii, kukuza utalii na kuchochea shughuli za kiuchumi zinazowanufaisha wananchi.

Katika kilele cha tamasha hilo, Mhe. Balozi Omar aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Kizimkazi, Zanzibar, hatua inayolenga kuimarisha mazingira ya utoaji wa huduma za kikodi katika eneo hilo.

Jengo hilo linatarajiwa kuwa na ghorofa moja na litakapokamilika litagharimu takribani Shilingi bilioni 3.6.

Ujenzi wa ofisi hiyo unatarajiwa kuwa na umuhimu katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa TRA, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa walipakodi na kusogeza huduma za Serikali karibu zaidi na wananchi na wafanyabiashara wa eneo la Kizimkazi na maeneo jirani.

Akizungumza katika muktadha wa tukio hilo, umuhimu wa uwekezaji katika miundombinu ya huduma za Serikali unaendana na jitihada za Serikali za kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuweka mazingira rafiki kwa shughuli za kiuchumi.

Kwa upande mwingine, Tamasha la Kizimkazi limeendelea kuonesha namna ambavyo matukio ya utamaduni yanaweza kutumika kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kupitia sanaa, utamaduni na shughuli za utalii, wananchi hupata fursa za kujiajiri, kufanya biashara na kuongeza kipato.

Kushiriki kwa viongozi wa kitaifa katika tamasha hilo pia kunasisitiza umuhimu unaotolewa na Serikali katika kuhifadhi urithi wa Taifa, kukuza sekta ya utalii na kutumia fursa zinazotokana na utamaduni na sanaa katika kuimarisha uchumi wa wananchi.

Kwa kuweka jiwe la msingi la Ofisi ya TRA Kizimkazi yenye thamani ya Sh bilioni 3.6, hatua hiyo inaongeza sura nyingine katika matukio ya kilele cha tamasha hilo, huku ikiashiria uwekezaji katika miundombinu ya huduma za Serikali sambamba na jitihada za kukuza shughuli za kiuchumi katika maeneo ya Zanzibar.

Tamasha la Kizimkazi limehitimishwa likiwa limekusanya wadau mbalimbali katika kuadhimisha utamaduni, sanaa na urithi wa Zanzibar, pamoja na kuhamasisha matumizi ya fursa za utalii na ubunifu kwa ajili ya maendeleo endelevu.

MORUWASA YAWAONYA WANAOUZA MAJI KINYUME NA UTARATIBU

MORUWASA YAWAONYA UUZWAJI WA MAJI KINYUME NA SHERIA 

Na Mwandishi wetu

 Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) imewaonya wateja wanaotumia huduma ya maji kwa matumizi ya nyumbani na kisha kuuza maji hayo bila kibali, ikisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka masharti ya huduma hiyo.

Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa MORUWASA, Getrude Salama, kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Agosti 14, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, MORUWASA inawajulisha wateja wote ambao wameunganishiwa huduma ya maji kwa matumizi ya nyumbani (Domestic Use) kuwa hawaruhusiwi kuuza maji hayo bila kufuata taratibu na kupata kibali kinachotakiwa.

MORUWASA imesema matumizi ya maji kinyume na kusudi lililowekwa katika mkataba wa huduma ni kosa kwa mujibu wa Kanuni ya 22(i) ya Kanuni za Maji za mwaka 2019.

“Matumizi ya maji kinyume na kusudi la mkataba ni kosa,” imeeleza taarifa hiyo, ikirejea masharti ya kisheria yanayosimamia matumizi ya huduma ya maji.

Aidha, mamlaka hiyo imeeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 65(2) cha Sheria ya Maji ya mwaka 2019, mtu anayekiuka masharti hayo anaweza kukabiliwa na faini isiyozidi Shilingi milioni tano (Sh5,000,000), kifungo kisichozidi miezi sita au adhabu zote kwa pamoja.

MORUWASA pia imeeleza kuwa ina mamlaka ya kutoza kiasi cha fedha kilichotumika kununua maji yaliyotumika kinyume na kusudi la mkataba, kwa mujibu wa kifungu cha 65(3) cha Sheria ya Maji ya mwaka 2019.

Athari kwa huduma ya maji

MORUWASA imeonya kuwa uuzaji wa maji kwa njia isiyozingatia utaratibu unaweza kuathiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengine.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kusababisha ukosefu wa maji kwa baadhi ya wateja katika maeneo husika, kupungua kwa msukumo wa maji na kusababisha maji kushindwa kufika katika baadhi ya maeneo mengine.

Kutokana na hali hiyo, MORUWASA imewataka wateja wanaojihusisha na uuzaji wa maji bila kufuata taratibu kuacha mara moja, ikisisitiza kuwa hatua za kisheria zitaanza kuchukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka masharti hayo.

Mamlaka hiyo pia imewataka wananchi kutumia huduma ya maji kwa kuzingatia masharti ya mikataba yao na kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa ufanisi na kwa usawa.

Taarifa hiyo imetolewa na Getrude Salama, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, MORUWASA, kwa niaba ya mamlaka hiyo, Agosti 14, 2026.

TANZANIA NA UJERUMANI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA MAENDELEO

Tanzania na Ujerumani Kuimarisha Ushirikiano wa Maendeleo, Waweka Mkazo Uchumi na Uwekezaji

Na Mwandishi wetu

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani zimeanza mazungumzo ya pande mbili kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, huku zikielekeza nguvu katika miradi yenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi na inayochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Mazungumzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Fedha, Mtumba jijini Dodoma, yamejikita katika maeneo ya kimkakati yakiwemo maji na usafi wa mazingira, afya, nishati, matumizi endelevu ya rasilimali za asili, uhifadhi wa mazingira, upatikanaji wa haki, usimamizi wa fedha za umma na usawa wa kijinsia.


Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Elijah Mwandumbya, alisema mazungumzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Ujerumani wenye historia ya zaidi ya miongo sita.

Mwandumbya alisema ushirikiano huo ulianza katika miaka ya 1960 na kuendelea kuimarishwa kupitia Mkataba wa Mfumo wa Ushirikiano uliosainiwa mwaka 1975, ulioweka misingi ya kuendeleza mahusiano ya maendeleo kati ya nchi hizo mbili.

“Ujerumani imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa Tanzania katika sekta mbalimbali, zikiwemo maji, mawasiliano, utalii, maendeleo ya watu na ustawi wa jamii,” alisema Mwandumbya.

Alisema mazungumzo hayo yanatoa fursa kwa wataalamu kutoka pande zote mbili kutathmini mafanikio ya ushirikiano uliopo, kubaini changamoto na kuweka vipaumbele vya miradi na maeneo yatakayotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Kwa mujibu wa Mwandumbya, baada ya wataalamu kukamilisha majadiliano na kufikia makubaliano, Serikali hizo zinatarajiwa kuchukua hatua za kurasimisha makubaliano hayo, ikiwemo kusaini mkataba wa ushirikiano wa maendeleo.

Alisema mazungumzo hayo yanatarajiwa kuendelezwa mwezi Novemba mwaka 2026, hatua ambayo inalenga kuhakikisha vipaumbele vilivyokubaliwa vinaendelea kufanyiwa kazi hadi kufikia makubaliano ya utekelezaji.

Tanzania yaweka Dira 2050 mbele

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, alisema Tanzania iko tayari kuimarisha na kuhuisha ushirikiano wake wa muda mrefu na Ujerumani ili kuendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Alisema Dira hiyo inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati cha juu, mseto, himilivu na jumuishi, huku ikihakikisha wananchi wanapata maisha bora na ustawi wa hali ya juu.

“Tanzania imejiwekea lengo la kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 na kuongeza pato la Taifa kwa mtu mmoja hadi takribani dola 7,000, kutoka uchumi wa sasa unaokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 90,” alisema Dkt. Kida.

Alisema Tanzania pia inalenga kupunguza kwa kiasi kikubwa umaskini, kuondokana na umaskini uliokithiri na kukabiliana na umaskini wa chakula, sambamba na kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa uendelevu na mazingira yanalindwa.

Dkt. Kida alisema ushirikiano na Ujerumani unaweza kuwa sehemu muhimu ya kufanikisha malengo hayo kupitia uwekezaji, uendelezaji wa sekta za uzalishaji, uimarishaji wa huduma za jamii na matumizi bora ya rasilimali.

Ujerumani yasisitiza uwekezaji na sekta binafsi

Naye Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati katika Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani, Joachim Schmitt, alisema Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku ikilenga kujenga ushirikiano wa kimkakati unaoendana na vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania.

Schmitt alisema mkakati mpya wa ushirikiano utaelekezwa katika maeneo yenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kupunguza umaskini pamoja na ukosefu wa usawa.

Alisisitiza pia umuhimu wa kulinda utawala wa sheria, nafasi ya asasi za kiraia, amani na usalama katika kuhakikisha mazingira ya maendeleo yanakuwa endelevu.

Kwa mujibu wa Schmitt, Ujerumani inalenga kuona ushirikiano huo ukijikita zaidi katika miradi mikubwa na yenye mwelekeo wa kimkakati, badala ya kutegemea miradi midogo isiyounganishwa katika mpango mpana wa maendeleo.

Aidha, alisema Ujerumani imeweka msisitizo maalumu katika ushirikiano wa kiuchumi, maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji, ikiwemo kuongeza ushiriki wa kampuni za Ujerumani na Tanzania katika miradi yenye tija kwa uchumi na wananchi.

Wawakilishi wa pande zote washiriki

Mkutano huo umewakutanisha wawakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka wizara na taasisi mbalimbali, wakiwemo Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa upande wa Ujerumani, ujumbe huo umehusisha Serikali ya Shirikisho la Ujerumani pamoja na taasisi zake za ushirikiano wa maendeleo, zikiwemo KfW na GIZ.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuweka msingi wa awamu mpya ya ushirikiano wa Tanzania na Ujerumani, kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania na kuongeza fursa za uwekezaji, ajira na ukuaji wa uchumi wenye manufaa kwa wananchi.

Aug 13, 2026

KANGWANDA AIPA YANGA NGAO YA JAMII


KANGWANDA AIPA YANGA NGAO YA JAMII, SIMBA YAKABIDHIWA KICHAPO ZANZIBAR

Na Mwandishi wetu

 Sherehe za ufunguzi wa msimu mpya wa soka Tanzania zimetawaliwa na furaha upande wa Young Africans (Yanga) baada ya kuifunga Simba SC bao 1–0 na kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo katika mchezo uliochezwa Jumatano usiku, Agosti 12, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mchezo huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini uligeuka kuwa ushindi mwingine kwa Yanga katika Kariakoo Derby, huku bao pekee la mchezo likifungwa na mshambuliaji wa Zambia, Albert Kangwanda, dakika ya 31.

Kangwanda alifunga bao hilo kwa kichwa baada ya kupokea mpira uliopigwa kwa usahihi kutoka kwa beki wa kushoto wa Yanga, Chadrack Boka, akiwazidi walinzi wa Simba na kuupachika mpira wavuni.

Bao hilo liliongeza presha kwa Simba, ambayo ilianza mchezo kwa kasi na kutawala baadhi ya dakika za mwanzo, lakini ilishindwa kutumia nafasi ilizopata kuzalisha bao.

Baada ya Yanga kupata bao, mchezo ulianza kubadilika, huku kikosi hicho kikiongeza utulivu katika kumiliki mpira na kujilinda kwa nidhamu ili kulinda faida yake.

Simba, chini ya kocha Steve Barker, ilijaribu kurejea mchezoni katika kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya kikosi, lakini safu ya ulinzi ya Yanga ilifanikiwa kuzuia mashambulizi mengi na kuifanya Simba ishindwe kupata nafasi nyingi za wazi.

Nafasi kubwa ya kusawazisha ilitokea dakika ya 89, wakati mshambuliaji wa Simba, Bakari Msimu, alipounganisha mpira wa krosi kwa kichwa, lakini kipa wa Yanga, Djigui Diarra, alifanya kazi kubwa kwa kuokoa na kuilinda timu yake dhidi ya bao la kusawazisha.

Ushindi mwingine katika Kariakoo Derby

Ushindi huo umeipa Yanga mwanzo mzuri wa msimu wa 2026/27, huku pia ukiendeleza ushindani mkali kati ya miamba hiyo miwili ya soka la Tanzania.

Mchezo huo ulikuwa pia kivutio cha mbinu za makocha wawili kutoka Afrika Kusini, Manqoba Mngqithi wa Yanga na Steve Barker wa Simba, ambao walikutana katika mchezo wenye presha kubwa tangu mwanzo hadi mwisho.

Kwa Mngqithi, ushindi huo umekuwa mwanzo mzuri wa safari yake katika soka la Tanzania, huku Yanga ikiondoka Zanzibar ikiwa na taji la kwanza la msimu mpya na haki ya kujivunia ushindi dhidi ya mpinzani wake mkubwa.

Kangwanda aanza kwa kishindo

Kwa Kangwanda, bao hilo limekuwa mwanzo wa kuvutia katika maisha yake ya ushindani akiwa na Yanga, baada ya kujiunga na klabu hiyo.

Mshambuliaji huyo alionyesha uwezo wa kutumia nafasi muhimu, akitumia krosi ya Boka kwa ustadi na kuamua hatma ya mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Kwa upande wa Simba, kipigo hicho kinakuwa changamoto ya mapema katika maandalizi ya msimu mpya, huku timu hiyo ikitakiwa kurekebisha baadhi ya mapungufu kabla ya kuingia kikamilifu katika mashindano ya msimu wa 2026/27.

Msimu waanza kwa ushindani mkali

Ngao ya Jamii imeendelea kuwa moja ya michezo inayovuta hisia kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka Tanzania, hasa inapokutanisha Yanga na Simba.

Mchezo wa mwaka huu umeongeza sura mpya katika ushindani huo, huku Yanga ikianza msimu kwa kutwaa taji na Simba ikilazimika kusubiri nafasi nyingine ya kuwania ubingwa.

Kwa mashabiki wa soka nchini, ushindi wa Yanga dhidi ya Simba ni ishara ya kuanza kwa msimu mwingine wenye matarajio makubwa, ushindani mkali na presha kubwa kwa timu hizo mbili zinazobeba sehemu kubwa ya historia na mvuto wa soka la Tanzania.

TUME YA UTUMISHI WA UMMA YAWAJENGEA UELEWA WA HAKI NA WAJIBU KAZINI WATUMISHI GAIRO


Tume ya Utumishi wa Umma Yawajengea Uelewa Watumishi wa Gairo Kuhusu Haki na Wajibu Kazini

Na Mwandishi wetu

Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo wamepatiwa mafunzo kuhusu haki na wajibu wao katika Utumishi wa Umma, pamoja na wajibu wa mwajiri, katika hatua inayolenga kuimarisha uadilifu, uwajibikaji, nidhamu na weledi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mafunzo hayo yalitolewa Agosti 13, 2026, katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo na Maafisa kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, yakiongozwa na Jimu Lihyuka.

Mafunzo hayo yaliwakutanisha watumishi kutoka kada mbalimbali za Halmashauri, wakiwemo watumishi wa Makao Makuu ya Halmashauri, vituo vya kutolea huduma za afya, Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji, pamoja na wataalamu wa Maendeleo ya Jamii, Kilimo na Mifugo katika ngazi ya Kata.

Aidha, watumishi wa kada ya Elimu ya Awali na Msingi walishiriki katika mafunzo hayo yaliyolenga kuongeza uelewa kuhusu haki zao, wajibu wao na wajibu wa mwajiri, pamoja na taratibu zinazopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Jimu Lihyuka alisisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kufahamu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma.

Alisema uelewa wa masuala hayo ni muhimu katika kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na weledi, huku wakiheshimu haki na wajibu wa mwajiri pamoja na mtumishi.

Kwa mujibu wa Lihyuka, watumishi wenye uelewa mzuri wa taratibu za utumishi wana nafasi kubwa ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na kutofahamu au kutofuata taratibu za kiutumishi.

Lengo ni Kuboresha Utoaji wa Huduma kwa Wananchi

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uelewa wa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma, ikiwemo haki, wajibu, nidhamu na uwajibikaji kazini.

Uelewa huo unalenga pia kuchangia katika kujenga mazingira bora ya utendaji kazi na kuimarisha utoaji wa huduma zenye ufanisi kwa wananchi.

Hatua hiyo inaendana na umuhimu wa kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji, weledi na uzingatiaji wa sheria, ambayo ni nguzo muhimu katika utoaji wa huduma bora kwa umma.

TFS YAWAELiMISHA 'WANYAGO'SHERIA ZA BIASHARA NA USAFIRISHAJI MAZAO YA MISITU'

TFS Yawaelimisha Wachongaji Vinyago Sheria za Biashara na Usafirishaji wa Mazao ya Misitu

Na Mwandishi wetu

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetoa elimu kwa wafanyabiashara na wachongaji wa vinyago katika eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam, kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uvunaji, usafirishaji na biashara ya mazao ya misitu, ikiwemo taratibu za kusafirisha bidhaa hizo nje ya nchi.

Elimu hiyo iliyotolewa Agosti 12, 2026, inalenga kuwawezesha wafanyabiashara na wachongaji kuelewa matakwa ya kisheria katika shughuli zao, pamoja na hatua zinazopaswa kufuatwa ili kufanya biashara kwa ufanisi na kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na kutofuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhifadhi wa Misitu wa TFS kwa Wilaya za Kinondoni na Ubungo, Dotto Ndumbikwa, amesema utoaji wa elimu kwa wadau ni sehemu muhimu ya kuwajengea uelewa kuhusu taratibu za biashara ya mazao ya misitu.


Amesema wafanyabiashara wanapaswa kufahamu taratibu husika kuanzia upatikanaji wa mazao ya misitu, usafirishaji, uuzaji na, inapohitajika, taratibu za kuyasafirisha nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Ndumbikwa, uelewa huo ni muhimu katika kuhakikisha wafanyabiashara wanaendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria na kupunguza uwezekano wa kukumbana na usumbufu unaotokana na kutokidhi matakwa ya kisheria.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wasanii Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA), Sebastian Daniel Mbebe, amesema elimu hiyo imewasaidia wachongaji kupata uelewa mpana zaidi kuhusu sheria na taratibu zinazohusiana na shughuli zao.

Mbebe amesema baadhi ya changamoto na malalamiko ambayo wachongaji wamekuwa wakikabiliana nayo yalitokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu taratibu zinazotakiwa kufuatwa katika kupata na kusafirisha mazao ya misitu.

“Elimu hii imetusaidia kuelewa vizuri zaidi sheria na taratibu ambazo awali zilikuwa chanzo cha baadhi ya malalamiko na changamoto katika shughuli zetu,” amesema Mbebe.


Naye mdau wa mazao ya misitu, Mwanne Mashugu, ameishukuru TFS kwa kuwafikia wafanyabiashara katika eneo lao la biashara na kutoa elimu kuhusu taratibu za uendeshaji wa shughuli hizo.

Mashugu amesema elimu hiyo imewasaidia kuelewa taratibu zinazopaswa kufuatwa kuanzia hatua ya kupata mazao ya misitu hadi kuyafikisha katika maduka kwa ajili ya biashara.

Wito kwa wafanyabiashara

TFS imeendelea kusisitiza umuhimu wa wafanyabiashara, wachongaji na wadau wengine wa mazao ya misitu kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazotumika katika sekta hiyo.

Wakala huo umewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanapata taarifa sahihi, elimu na vibali kutoka katika ofisi husika za Serikali kabla ya kuanza biashara au kusafirisha bidhaa za misitu, hususan nje ya nchi.

Hatua hiyo inalenga kuweka mazingira ya biashara yanayozingatia sheria, wakati huohuo kuhakikisha matumizi ya rasilimali za misitu yanafanyika kwa utaratibu unaozingatia uhifadhi na uendelevu wa rasilimali hizo.