CRDB Gairo Yaipa Gairo Sports Club Msaada Kuelekea SHIMISEMITA 2026
Na Mwandishi wetu
Benki ya CRDB, Tawi la Gairo, imeunga mkono safari ya Gairo Sports Club kuelekea Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) 2026 kwa kukabidhi zaidi ya katoni 30 za maji kwa ajili ya timu zinazoiwakilisha Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Msaada huo umekabidhiwa Agosti 14, 2026 katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Gairo na Bi. Elialice Lema, Afisa Mikopo wa CRDB Tawi la Gairo, kwa niaba ya benki hiyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bi. Lema amesema CRDB inatambua umuhimu wa kushirikiana na Serikali pamoja na jamii katika kusaidia shughuli zenye manufaa kwa wananchi, ikiwemo maendeleo ya michezo na kukuza vipaji.
Amesema mchango huo ni sehemu ya juhudi za CRDB kuendelea kuwa karibu na jamii na kushirikiana na wadau katika maeneo mbalimbali yenye mchango katika maendeleo ya wananchi.
Msaada huo wa maji unalenga kuwasaidia wanamichezo wa Gairo Sports Club katika kipindi cha maandalizi na ushiriki wao kwenye mashindano hayo, ambayo yanatarajiwa kuanza Agosti 16, 2026, jijini Mbeya.
Kwa upande wake, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo umeipongeza CRDB Tawi la Gairo kwa hatua hiyo, huku ukitoa wito kwa taasisi, wafanyabiashara na wadau wengine kuendelea kushirikiana na Halmashauri katika kuendeleza michezo na kukuza vipaji vya vijana.
Gairo Sports Club ni miongoni mwa timu zinazotarajiwa kushiriki SHIMISEMITA 2026, mashindano yanayowakutanisha watumishi kutoka Halmashauri mbalimbali nchini katika michezo mbalimbali.
Mchango wa CRDB unatajwa kuwa sehemu ya ushirikiano kati ya sekta ya fedha na taasisi za Serikali katika kuunga mkono michezo, ustawi wa watumishi na kukuza vipaji kupitia mashindano ya SHIMISEMITA 2026.


No comments:
Post a Comment