PURA WATOA UFAFANUZI KUHUSU UTAFUTAJI WA MAFUTA, GESI ASILIA
Na Thadei Hafigwa
WANANCHI mkoani Morogoro wameonyesha shauku kubwa ya kupata taarifa sahihi kuhusu shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini, huku wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) wakitoa ufafanuzi kuhusu hatua iliyofikiwa katika utafutaji wa rasilimali hizo.
Shauku hiyo imejitokeza wakati wa Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika mkoani Morogoro, ambapo wananchi waliotembelea banda la PURA waliuliza maswali kuhusu uwepo wa mafuta nchini, shughuli za utafutaji zinazoendelea na uwezekano wa kuanza uzalishaji wa mafuta iwapo yatathibitishwa kuwepo kwa kiwango kinachoweza kuendelezwa kibiashara.
Baadhi ya wananchi walitaka kufahamu iwapo tayari Tanzania imethibitisha uwepo wa mafuta na ni lini shughuli za uchimbaji zinaweza kuanza.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha tamasha hilo, Mjiolojia kutoka PURA, Lukelo Matimbwi, alisema shughuli za utafutaji wa mafuta bado zinaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kubaini uwepo na kiwango cha rasilimali hiyo.
Matimbwi alisema Tanzania tayari imebaini uwepo wa gesi asilia, huku shughuli za utafutaji wa mafuta zikiendelea kwa kutumia tafiti na teknolojia zinazotumika katika sekta ya petroli.
“Bado kuna tafiti na shughuli za utafutaji zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini ili kubaini uwepo na kiwango cha rasilimali za mafuta,” alisema Matimbwi.
Alisema hatua za utafutaji zinahitaji tafiti za kitaalamu na tathmini mbalimbali kabla ya kufikia hatua ya kuthibitisha uwepo wa rasilimali inayoweza kuendelezwa.
Matimbwi pia alieleza kuwa PURA inatumia fursa kama tamasha hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake katika kusimamia na kudhibiti shughuli za mkondo wa juu wa petroli.
Kwa mujibu wa Matimbwi, shughuli hizo zinahusisha mchakato wa utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia.
CHIFU LUKWELE AIPONGEZA PURA
Kwa upande wake, Chifu Lukwele wa Morogoro amezipongeza taasisi za serikali na wataalamu walioshiriki katika tamasha hilo kwa kutumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zao na tafiti zinazofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Chifu Lukwele alisema ushiriki wa taasisi hizo ni muhimu kwa sababu unawawezesha wananchi kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu shughuli zinazofanywa na serikali na wataalamu katika sekta mbalimbali.
“Niipongeze sana PURA kwa kuweka banda lao katika tamasha hili, ambapo wananchi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu shughuli mbalimbali wanazofanya,” alisema.
Alisema viongozi wa mila na Machifu wataendelea kushirikiana na serikali pamoja na wataalamu na watafiti watakaofika katika maeneo yao kwa ajili ya shughuli za utafiti na maendeleo.
Chifu Lukwele alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kuhakikisha tafiti na shughuli nyingine za maendeleo zinafanyika kwa utaratibu unaozingatia maslahi ya wananchi na uhifadhi wa rasilimali na maliasili za taifa.
WANANCHI WATAKA ELIMU ZAIDI
Kwa upande wao, wananchi waliofika katika banda la PURA walitumia fursa hiyo kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia.
Maswali yao yalijikita zaidi katika hatua iliyofikiwa katika utafutaji wa mafuta, namna shughuli hizo zinavyosimamiwa na fursa ambazo sekta ya petroli inaweza kuzalisha kwa taifa endapo rasilimali hizo zitagundulika na kuendelezwa kibiashara.
Ushiriki wa PURA katika Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni umeongeza nafasi ya wananchi kupata elimu kuhusu sekta ya petroli nje ya majukwaa ya kitaalamu, huku ukitoa fursa kwa wataalamu kujibu maswali na kueleza taratibu zinazotumika katika utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia.
Tamasha hilo limeendelea kuwa jukwaa la taasisi mbalimbali za serikali na wadau kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma, tafiti na fursa zinazohusiana na maendeleo ya taifa.




No comments:
Post a Comment