Breaking News

Aug 23, 2026

MVOMERO DC YAANZA KUTIKISA SHIMISEMITA MBEYA

MVOMERO DC YATIKISA SHIMISEMITA MBEYA, PROF. SHEMDOE ATOA ONYO KALI DHIDI YA UDANGANYIFU

Na Mwandishi wetu

Viongozi, watumishi na wachezaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wameshiriki katika ufunguzi rasmi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA), yanayofanyika jijini Mbeya.

Ufunguzi wa mashindano hayo umefanyika leo, Agosti 23, 2026, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, huku mgeni rasmi akiwa Prof. Riziki Silas Shemdoe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), aliyemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Prof. Shemdoe amewataka washiriki wote kuzingatia kikamilifu kanuni, taratibu na sheria zinazoongoza mashindano hayo, akisisitiza umuhimu wa michezo kuendeshwa kwa haki, uadilifu na ushindani wa kiungwana.

Prof. Shemdoe ametoa onyo kali dhidi ya udanganyifu katika michezo, akisema timu au mchezaji yeyote atakayebainika kukiuka taratibu na kufanya udanganyifu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za mashindano, ikiwemo kufutiwa matokeo.

“Michezo inapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu. Hakutakuwa na nafasi ya udanganyifu. Timu au mchezaji atakayebainika kufanya udanganyifu atachukuliwa hatua, ikiwemo kufutiwa matokeo,” amesema Prof. Shemdoe.

Aidha, Prof. Shemdoe ameeleza kuwa SHIMISEMITA ni jukwaa muhimu la kuimarisha afya, ustawi, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa Serikali za Mitaa, sambamba na kutoa fursa kwa watumishi kuonesha vipaji vyao katika michezo mbalimbali.

Katika mashindano hayo, watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wanashiriki katika michezo mbalimbali kwa lengo la kuonesha uwezo, vipaji na ushindani, huku wakilenga kuiwakilisha vyema Halmashauri yao na kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Ushiriki wa Mvomero DC pia unalenga kuimarisha uhusiano na mshikamano miongoni mwa watumishi, pamoja na kutumia michezo kama sehemu ya kujenga afya bora na kuongeza morali ya utendaji kazi.

Kaulimbiu hiyo inaendana na maandalizi ya Tanzania kuelekea kuwa sehemu ya wenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambayo itafanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.

No comments:

Post a Comment