Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro,Mhandisi Emanuel Kalobelo
Na Andrew Chimesela
KATIBU Tawala Mkoa wa
Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amezitaka Taasisi za Umma Mkoani humo kuwasogezea karibu huduma Wananchi wa
Halmashauri ambazo zimeazisha makao mapya hivi karibuni ili kuwaondolea kero
wananchi hao.
Mhandisi Kalobelo ametoa
agizo hilo leo Oktoba 19 wakati wa Kikao na Wakuu wa Taasisi hizo
kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa lengo la
kufahamiana na kuwakumbusha wajibu wao katika kuwahudumia wananchi kulingana na
Taasisi zao.
Kiongozi huyo ambaye ndiye
Mtendaji Mkuu wa Serikali ngazi ya Mkoa amesema kuna Halmashauri katika Mkoa wa
Morogoro ambazo zimeanza makao yao mapya hivi karibuni ambazo wananchi wake
wanahitaji huduma kwa karibu zaidi hivyo
kuzitaka Taasisi ambazo hazijapeleka huduma kwenye halmashauri hizo kufanya
hivyo.
“Ningependa kuwakumbusha
wajibu wetu kama Taasisi za Umma ndani ya Mkoa wa Morogoro umuhimu wa kuhamia
kwenye Makao mapya ya kiutawala ndani ya Mkoa huu. Mtakumbuka kwamba Serikali
kwa nyakati tofauti tofauti imekua ikianzisha maeneo mbalimbali ya kiutawala
ndani ya Mkoa wa Morogoro”
Akifafanua zaidi Mhandisi
Kalobelo amezitaja Halmashauri ambazo zinahitaji wananchi wake kusogezewa
huduma kwa karibu zaidi kutoka Taasisi mbalimbali ni pamoja na Malinyi, Mlimba
yenye makao yake makuu Mngeta na
Morogoro vijijini ambapo Makao makuu yake yako Mvuha.
Aidha, Mhandisi Kalobelo
amezitaka Taasisi hizo kuongeza jitihada katika kutatua kero za Wananchi kwa
wakati na kwa lugha yenye staha huku akikumbushia agizo lake la kutaka lijengwe
jengo moja (One Stop Centre) ambalo Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali
watafanyia kazi humo ili kurahisisha upatikanaji wa vibali mbalimbali katika
sehemu moja.
Sambamba na agizo hilo
amezikumbusha Taasisi hizo kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji mbalimbali
wanaotaka kuwekeza ndani ya Mkoa huo huku akibainisha kuwa baadhi ya Taasisi
zimekuwa kikwanzo kwa wawekezaji wanapojitokeza kuwekeza hivyo amewataka
kubadilika na kuiunga Mkono Serikali katika kukuza Uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Serikali za Mitaa Leopold Ngilwa amesema agizo la Katibu Tawala wa Mkoa kwa Taasisi za Umma limekuja kwa wakati muafaka maana changamoto kwa maeneo yalioanzishwa bado ni kubwa , na sehemu nyingi kama Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mlimba na bado hawajapata huduma muhimu kama kibenki, TANESCO, TCCL na kusababisha kero kwa wananchi wa maeneo hayo.
Naye,Frazina Gwimo
amesema kikao hicho kimesaidia wao kama Taasisi za Umma Mkoani humo kufahamiana
wao kwa wao na wametambua namna ya
Utendaji kazi wa Taasisi kuhakikisha
inashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kuweza kutatua changamoto za
Wananchi wa Mkoa kwa ukaribu zaidi
badala ya kufikisha kero zao moja
kwa moja Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Naye, Kiongozi wa Huduma ya
Misitu Tanzania - TFS Wilaya ya Malinyi Kamanda Amari Mramba amesema kupitia
kikao hicho wameweza kufahamiana na wengine
na wamekumbushwa kushirikiana na Taasisi nyingine na katika shughuli zao
za Uhifadhi kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa .
No comments:
Post a Comment