Breaking News

Sep 13, 2020

UTALII WA UTAMADUNI:Vivutio vilivyopo Halmashauri ya Morogoro

Na Thadei Hafigwa

MKOA wa Morogoro wenye Halmashauri za Wilaya 9 ambazo vina vivutio lukuki ambapo kupitia Moropc Blog tutakuwa tukiviangaza kimoja baada ya kingine.

Halmashauri hizo ni pamoja na Morogoro,Mvomero,Gairo,Ulanga,Malinyi,Kilombero,Ifakara mjini,Kilosa na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro,Leo tutaanza na baadhi ya vivutio vya kiutamaduni vilivyopo katika Halmashauri ya Morogoro ambapo ni pamoja na;

MWAMBA WA FUKWE:eneo hili lipo Tegerero,ambapo kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo katika Halmashauri zinaeleza kuwa Mwamba huu uko  umbali wa km 57 kutoka  Morogoro mjini.  Eneo hili hufikika kwa wastani wa masaa mawili kutokea Kanisa la Tegetero.
Mwamba huu umezungukwa  na msitu wa asili wa Ugulo katika eneo la Tegetero,ni miongoni mwa maeneo yanayovutiwa na watalii  una mandhali ya kuvutia kwa kupumzikia na kuweka kambi ili kuangalia maeneo ya milima na maporomoko    ya maji kwa upande wa Kaskazini wa Mwamba huo.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro,Mhe.Bakar Msulwa (pichani)

Katika Mwamba huu kuna kambi  tatu zilizopo katika msitu  wa eneo la Fukwe hutumiwa na watalii kutembelea na kuangalia ndege na maua aina ya “Saint Pauline”.
Katika msitu wa Ugulo kuna ndege waitwao “Uluguru Bush light”wenye maumbo makubwa rangi nyekundu na nyeusi ambao hpendelea kuishi katika miti mikubwa ya Msitu huo mnene.

KIJIJI CHA KIMILA:Kijiji cha Kimila kinapatikana huko Kinole ambalo eneo la pembezoni mwa mji wa Morogoro umbali wa km 45 kutoka Morogoro mjini .
Ukifika Kijiji cha Kinole unaweza  kuona Mwamba wa Fukwi ambao jamii ya Kabila la waluguru walikuwa wakijificha wakati wa ukoloni.

Ukitoka Kinole unaelekea Tegetero unaweza kuona msitu wa Ugulo  ambapo chief wa Kijiji cha Tegetero (Chief Magoma  alikuwa akifanya Ibada Kupanda kwenye mlima kitundu ambao unaweza kuona msitu  mzuri wa Asili ukiwa kileleni.

Unaweza kupanda kwenye maporomoko ya maji Kisimbi  kuogelea kwenye maji safi,Kufika kwa chief Kingalu (Nyumbani kwake) Chief wa 15 wa Waluguru.

MWAMBA WA MATOMBO NA MAPANGO YA MATOMBO:Mwamba huu unapatikana eneo la matombo,ambapo historia inaelezea kuwa Katika Miamba ya Matombo kuna mawe yalioshikana  mithiri ya Matiti ya Mwanamke hujulikana kwa jina la Matombo.
Neno matombo asili yake  matiti ya Mwanamke kwa lugha ya Kiluguru Mapango haya yanafikika kwa urahisi yana mandhali nzuri na sehemu nadhifu ya kupumzikia kwa ndani. Wakazi wa eneo hilo hutumia mapango haya kwa shughuli za kimila.MILIMA YA KOLELO: Jina la mzimu maarufu sana Morogoro ,Asili ya jina la mwanamke Ajuza Bibi aliyepewa karamu na mwenyezimungu ya kutibu na kutatua   matatizo ya watu mbalimbali huko mlima Kolelo kwenye Pango ambalo mzimu wake ulifanya maajabu.

Alipofariki mzimu  wake uliendelea kuwachagua watoto wa kurithi mikoba.
Kaburi la bibi huyu lipo mpaka leo huko Lubasazi (Kolelo) ukitaka kufika waone walinzi wa milima Kolelo.
Zipo simulizi Lukuki  kwa miujiza ya Kolelo na Mlima wenyewe .Kubwa ni ile ya ufumbuzi wa matatizo ya kijamii, mfano magonjwa, kukosa  mtoto kwa muda mrefu.
Hii ni sehemu maarufu kwa shughuli za Kimila kama matambiko ambayo hufanyika kipindi cha Mwezi Disemba kwa kila Mwaka .
Katika mapango ya misitu ya Kolelo watalii wanaweza  kufika na kujionea desturi na Tamaduni za Makabila ya Kiluguru  na wakutu pindi wanapofanya maombi kwa mizimu.

MAPOROMOKO YA MAJI MLULU: Maporomoko ya maji ya Mlulu yapo katika Kata ya Mtombozi ni kivutio kikubwa cha Utalii.Maporomoko  hayo  yanapatikana umbali wa km 85 kutoka Morogoro Mjini na yanafikika kwa urahisi nyakati zote. utafiti uliofanywa na Shirika la Umeme TANESCO umeeleza kuwa maporomoko haya yanaweza kuzalisha umeme wa kilowati 2.

MSITU WA KIMBOZA ( BWAWA LA KIMBOZA): Msitu wa Kimboza ni miongozi mwa mali kale zinazotumika kuhifadhi historia na utamadui wa makabila Nchini.Msitu  huu una ukubwa wa Hekta 405 na upo umbali wa km 51 kutoka Morogoro barabara ya Matombo kuelekea Kisaki na umepakana  na vijiji vinne vilivyopo katika Tarafa ya Mkuyuni pamoja na Matombo.
Msitu huo una miti mingi inayotumiwa kwa ajili ya dawa za asili muhimu kwa kutunza vipepeo wenye rangi mbalimbali vya kuvutia.

WEUSI VIPEPEO MIJUSI –GECKO VINYONGA: Pia msitu huu una bainowai wa aina mbalimbali kama vile vinyonga wadogo na mijusi ambayo imeelezwa haipatikani sehemu nyingine duniani.

‘CHOKA WAHAWI’: Kwenye msitu kuna Mwamba wa jiwe ambao inaelezwa  lilitumika ,kutolea adhabu kali kwa wachawi.
Kwa mujibu wa taarifa za wazawa karne ya 19 msitu huu  ulitumiwa na machifu wa kabila la waluguru kama eneo maalumu la kutolea adhabu ya kuwachoma moto watu waliokuwa wamethibitika ni wachawi.
 Simulizi za kale zinasema watu wote ambao walibainika kuwa ni wachawi walipelekwa kwenye pango lenye jiwe maalumu kwa ajili ya kuwachoma ambapo hufungwa  kamba mikono na miguu halafu  anaingizwa ndani ya jiwe .
Machifu wa Kiluguru walitenga eneo hilo maalumu na kuliita “Choka wahawi” . Adhabu hizo ziliisha  baada yaTanganyika kupata Uhuru wake mwaka 1961.

PANGO LA NJIWA: Simulizi zinaeleza kwenye msitu huu kuna sehemu ya makumbusho ya kihistoria ya Kijadi  ya Kabila la Waluguru ambapo pia ndani ya Msitu  huo kuna maeneo yamepewa majina ya “Dago la Njiwa”ambalo wanajumuika njiwa pori ambao wanaoga kwa kutumia majivu .

MBEGA  WEUSI :Kadhalika Msitu wa Kimboza wanapatikana wanyama aina ya Mbegu na ndege wa kila aina wakiwemo njiwapori kabla ya mwaka 1922.

USOLO: Aina hii ya kivutio inapatikana eneo la  MVUHA (TAMBUU) Eneo hili liliwahi kutumiwa na viongozi wa jamii ya Kabila la Waluguru ,Chifu Kingalu wa kwanza na Hega kwa kile wanachosadikiwa kuonyesha umahili wao wa kuchonga juu ya sakafu ya Miamba ya Mawe kwa Kisigino karne kadhaa zilizopita huko kijiji cha Tambuu
Taarifa zimebainisha kuwa viongozi hao wa jadi walikuwa na ushindani wa kimadaraka na kupelekea kukutana katika makutano ya Mito ya Mtombozi na mngazi  na kuunda Mto-Mvuha.
Kiongozi wa jadi chifu Kingalu wa kwanza na Hega waliwahi kushindana nani mwenye uwezo na nguvu za kiutawala jamii inayoishi milima ya uluguru ambapo katika ushindani huo walilazimika kuoneshana  umwamba  wa kuchonga mwamba wa jiwe kwa kutumia visigino (Usolo /mchezo wa Bao)
Ukifika katika makutano ya Mto Mtombozi na mngazi na kuunda mto mvuha katika Mwamba wa jiwe uliochongwa katika kutumia ncha ya Kisigino.
Kitongoji cha Usolo kiko katika kijiji cha Tambuu na kushuhudia  vishimo vilivyosadikiwa kuchimbwa kwa kutumia ncha ya visigino vya viongozi wa jadi chief Kingalu na Chief Hega katika  ushindani wao.


Taarifa  zinasema Kingalu aliweza kumzidi mwenzake maarifa kwa kuchimba vishimo 36 huku Hega  akiambulia vishimo 16 pekee ambapo baada ya ushindani huo waliweka mipaka ya kiutawala Hega aliweza kumiliki eneo la ardhi kuelekea Kisaki ambapo  Kingalu aliendelea kutawala eneo la Kinole hadi leo,utawala wa sasa wa jamii ya waluguru ni wa chief Kingalu Mwanabanzi 15 ambaye  anaishi katika kijiji cha kinole  huku mila na desturi zikiendelea kuanziwa kwa kufanya Tambiko kila mwaka kwa kuomba ustawi wa jamii.

CHIEF KINGALU 15: Chief Kingalu Mwanabanzi wa 15 Mtawala wa waluguru wa Matombo anapatikana katika eneo la Kinole.Miaka 300 iliyopita waluguru waliingia katika milima ya Uluguru wakiongozwa na machifu watatu wakuu ni
Chifu  Mbagho wa Waluguru wa Mgeta ambaye alipiga Kambi yake vidighisi.
Wa pili Chifu Kingalu ambaye baadaye kwa namna ya ajabu mzimu wake yulisafiri hadi Turiani ambako Matambiko yanafanyika.
 Na watatu ni Hegga wa Waluguru wa Kisaki Chief Kingalu  mwanabanzi anafuata mstari wa Kingalu aliitisha  waluguru wenye koo zinazoheshimu utawala huo  hasa katika utamaduni wa Matambiko.
kumbukumbu zinaeleza kuwa Chifu Mbagho aliona ujio wa Wajerumani na waarabu  ndiye aliyetabiri kuwapo kwa kijana mdogo ambaye atawaondoa wageni katika Tanganyika  simulizi zinasadiki kijana huyo ni Mwalimu  Julius Kambarage Nyerere.

MZIMU WA WALUGURU: Mzimu huu unapatikana eneo la Kolelo, Eneo hili la Kolelo kwa miaka nenda miaka rudi ni alama moja muhimu ya temi takribani tatu zinazofanya kabila la waluguru.


Kolelo ni mzimu  ni jina  la mahali na alama katika mambo mengi na makubwa  ya kihistoria yaliyotokea Uluguru.Temi  zinazotumia ni zile  zilizoongezwa na  Hegga ,Mbagho  na Kingwalu.simulizi zinasema kulikuwa na wanawake wawili ndugu waliokwenda kusenya kuni msituni.Bila shaka  karibu na mlima Kolelo mmoja akapotea  inasadikiwa alibebwa na joka hadi pangoni  wakamtafuta wakakata tama.
Baada ya muda akatokea akiwa na mkoba wa uganga  .Mkoba huo alivyorudi nao kutoka Pango la Kolelo ndio uliotumika kuikomboa  jamii dhidi ya madhila mboka huu ukaarithiwa kutoka kizazi hazi kizazi.Kolelo ni mahali pasafi wachafu hawafiki huko ama sivyo wataumbika hasa uchafu wa Matendo na Tabia ujumbe wa Kolelo ni kuwataka watu wawe na matendo masafi na kurudia mila na Desturi.

CHEMCHEM YA MAJI:Uwepo chemchem ya maji moto Eneo linapatikana magharibi mwa Kisaki umbali  wa kutoka Stesheni km 5,chemchem hii ni kivutio kikubwaa cha utalii na shughuli za kimila hufanyika kwenye eneo hilo ikiwemo matambiko , hata hivho maji hayo hutumika kama dawa ya ngozi.

BWAWA LA VIBOKO: lipo katika eneo la Lukulunge bwawa hili lina viboko wengi ambapo wageni mbalimbali hufika  kwa  ajili ya kujionea viboko  walioko kwenye Bwawa hili .Shughuli za uvuvi  hufanyika na kuwapatia wananchi chakula na kujikwamua kiuchumi hasa wavuvi

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment