Breaking News

Aug 17, 2026

RAIS SAMIA KUZINDUA UMEME WA JNHPP AGOSTI 22,2026 RUFIJI

HISTORIA YAANDIKWA: JNHPP KUKAMILIKA, RAIS SAMIA KUZINDUA MRADI AGOSTI 22

Na Thadei Hafigwa

Hatimaye historia inaandikwa katika sekta ya nishati nchini Tanzania, baada ya Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kukamilika na kutarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Agosti 22, 2026, katika eneo la Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Mradi huo mkubwa wa kimkakati umejengwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme nchini, kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika na kuweka msingi wa kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya viwanda.

Kwa kujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma unaeleza kuwa mafanikio ya mradi huo ni matokeo ya nguvu za Watanzania na matumizi ya mapato ya Serikali, ikiwemo kodi zinazolipwa na wananchi na wafanyabiashara.

Kauli ya “Kwa kodi zetu, historia imeandikwa!” imebeba ujumbe wa umuhimu wa ulipaji kodi katika kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa kwa taifa.

Uzinduzi wa JNHPP unatarajiwa kuwa tukio muhimu katika historia ya maendeleo ya nishati nchini, huku Watanzania wakisubiri kwa hamu kuona mradi huo ukianza kutoa mchango wake katika kuongeza uwezo wa Taifa wa kuzalisha umeme.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wananchi wametakiwa “kukaa tayari” kushuhudia tukio hilo litakalofanyika Rufiji Agosti 22, 2026.

Mradi wa JNHPP ni sehemu ya jitihada za Tanzania kujenga mfumo imara wa nishati unaoweza kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na ukuaji wa uchumi, viwanda, biashara na ongezeko la matumizi ya umeme.

Uzinduzi huo pia unatarajiwa kutoa fursa ya kuangazia hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi, matarajio yake kwa uchumi wa Taifa na namna wananchi watakavyonufaika na ongezeko la upatikanaji wa umeme. 

No comments:

Post a Comment