Breaking News

Aug 21, 2026

FEASSA YARIDHISHWA NA MAZINGIRA YA UWANJA WA JAMHURI MOROGORO


FEASSA YARISHWA NA MAZINGIRA YA UWANJA WA JAMHURI MOROGORO 

Na Mwandishi wetu

 Uongozi wa Shirikisho la Michezo ya Shule za Msingi na Sekondari Afrika Mashariki (FEASSA) umeipongeza Serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa maandalizi bora ya mashindano ya michezo ya shule za msingi na sekondari Afrika Mashariki yanayoendelea mkoani humo.

Pongezi hizo zilitolewa Agosti 20, 2026, wakati viongozi wa FEASSA wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo, Justus Kamugisha, na Katibu Mkuu, Ngugi David, walipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, ofisini kwake.

Viongozi hao walisema maandalizi yaliyofanywa na Mkoa wa Morogoro yamewezesha mashindano hayo kufanyika katika mazingira salama na yenye utulivu, huku wakibainisha kuwa ushirikiano kati ya kamati ya maandalizi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa umechangia kufanikisha mashindano hayo.

Akizungumza baada ya kupokea pongezi hizo, Mhe. Malima alisema Morogoro itaendelea kutoa ushirikiano kwa FEASSA na wadau wengine wa michezo, akisisitiza kuwa mkoa huo una fursa kubwa za kuendeleza michezo na kukuza vipaji vya vijana.

“Morogoro ina fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuboresha mazingira ya michezo na kuongeza aina mbalimbali za michezo inayofanyika mkoani hapa,” alisema Malima.

Alisema mkoa una maeneo makubwa yanayoweza kutumika kwa shughuli za michezo, hivyo kuna haja ya kutumia fursa hizo kwa ufanisi ili kuibua vipaji vipya na kuongeza ushiriki wa vijana katika michezo mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Michezo, Utamaduni na Sanaa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Yusuph Singo Omari, alisema mashindano hayo yamefungua fursa muhimu za kiuchumi kwa Tanzania na maeneo yanayowahudumia washiriki.

Singo alisema ujio wa maelfu ya washiriki na wageni kutoka nchi za Afrika Mashariki unatoa fursa kwa wafanyabiashara, hususan wanaofanya biashara za hoteli, usafirishaji, chakula na huduma nyingine, kuongeza shughuli zao za kiuchumi.

Mashindano hayo yaliyoanza Agosti 12, 2026, yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti 23, 2026, yakishirikisha zaidi ya wanafunzi 6,000 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Lengo la mashindano hayo ni kukuza na kuibua vipaji vya michezo miongoni mwa wanafunzi, huku yakitoa fursa kwa vijana kutoka nchi za Afrika Mashariki kukutana, kushindana na kujenga urafiki na mshikamano kupitia michezo.

Baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo mwaka huu, Kigali, Rwanda, inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya FEASSA mwaka 2027.

No comments:

Post a Comment