WALIMU
950 WA SAYANSI,HISABATI WANOLEWA SINGIDA
Na Thadei Hafigwa
WALIMU 950 wa masomo ya Sayansi na Hisababiti kutoka mikoa 21 ya
Tanzania bara wametakiwa kutumia mbinu za kisasa zinazozingatia mabadiliko ya
sayansi na teknolojia ili kuwasaidia wanafunzi kuyapenda masomo hayo na kuelewa
mada ngumu kwa urahisi.
Mbinu hizo ni sehemu ya
juhudi zinazowekwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana
na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Mradi
wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP).
Winchslaus Balige ni
mratibu wa kituo cha Mafunzo akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa walimu wa masomo ya Sayansi na
Hisabati yanayofanyika mkoani Singida katika Shule ya Sekondari Mwenge, amesema
kuwa malengo ya mradi huo ni kuwawezesha walimu kutumia mbinu bora na za kisasa
katika ufundishaji na ujifunzaji.
Balige alisema kwamba mbinu
za ufundishaji watakazojifunza walimu zitahusisha namna ya kutumia Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji
wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
“Mafunzo haya endelevu ya
walimu kazini yatasaidia walimu kufahamu namna ya kuandaa zana mbalimbali za
kufundishia. Watafundishwa jinsi ya kutumia vishkwambi wakati wa kuandaa masomo
kwa kuzingatia maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye wakati wa kugawa
vifaa hivyo kwa walimu aliwahimiza vikatumike kwa ufanisi ili kurahisisha kazi
ya ufundishaji,” amesema Balige.
Kwa upande wake,Mwenyekiti
wa Wawezeshaji wa mafunzo hayo, Dk. Emmanuel Sulungu, ambaye pia ni Mhadhiri
kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Idara ya Fizikia, amewasisitiza walimu
kubadilisha mbinu zao za ufundishaji baada ya mafunzo, ili kuwasaidia wanafunzi
kufanya vizuri katika masomo yao.
Mafunzo hayo yalifunguliwa na
Ofisa Taaluma Mkoa wa Singida, Lago Sillo, amewataka walimu wanaoshiriki mafunzo
hayo kuyapa thamani ili yawanufaishe katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa
kuzingatia Sera ya Elimu ya mwaka 2014, Toleo la 2023, ambayo inasisitiza
matumizi ya teknolojia katika ufundishaji.
Miongoni mwa walimu
wanaoshiriki mafunzo hayo ni pamoja na Jesca Matezi kutoka Shule ya Sekondari
Buhingo, Wilaya ya Chato, mkoani Geita, ambaye amesema anatarajia kufundishwa
mbinu mpya za ufundishaji katika somo la Fizikia.
Amesema somo hilo linaogopwa na wanafunzi
wengi, wakidhani ni gumu, lakini kupitia mafunzo atapata mbinu mpya za kisasa
ambazo atazitumia ili kuwafanya wanafunzi walielewe somo na kulipenda.
"Ninayofuraha kupata
fursa ya kushiriki mafunzo haya, yataniwezesha kuzalisha wanafunzi wengi
watakaopenda Fizikia na kuisaidia nchi yangu kuwa na wanasayansi wengi, ambao
wataweza kusaidia taifa katika nyanja mbalimbali," amesema Mwalimu Jesca.
Mwalimu Victorian Dominic
kutoka Shule ya Sekondari Dareda, mkoani Manyara, anayefundisha somo la
Hisabati, alisema ana shauku kubwa ya kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu
mtaala mpya, matumizi ya lugha ya Kiingereza katika ufundishaji wa Hisabati.
Bahati Kisaka,
anayefundisha somo la Biolojia katika Shule ya Sekondari Mwinyi, mkoani Pwani,
amesema kupitia mafunzo hayo atawasaidia wanafunzi wengi kuvutiwa na somo hilo.
Hassan Kalilo,
anayefundisha somo la Kemia katika Shule ya Sekondari Isela, mkoani Shinyanga,
ameishukuru Wizara kwa kuandaa mafunzo hayo, akidai kuwa yatawasaidia walimu
kupata maarifa mapya yanayohusiana na mabadiliko ya kisasa na mahitaji ya
dunia.

No comments:
Post a Comment