SERIKALI KUONGEZA BILIONI 1.5 MIRADI YA ELIMU NA AFYA MVOMERO
Na Mwandishi wetu
WILAYA ya Mvomero imeendelea kushuhudia mageuzi makubwa katika sekta za elimu na afya baada ya Serikali kutumia zaidi ya shilingi bilioni moja kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema hayo Julai 18, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi iliyokamilika tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Prof. Shemdoe amesema miradi hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha huduma za kijamii kupitia uwekezaji mkubwa katika elimu na afya.
Miongoni mwa miradi iliyokamilika ni Shule ya Msingi Miembeni, iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 115 kwa ajili ya madarasa na vyoo, Shule ya Sekondari Mkindo iliyogharimu shilingi milioni 528, pamoja na jengo la upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Mvomero lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 500.
Waziri huyo aliwapongeza viongozi wa halmashauri, wataalamu na wasimamizi wa miradi kwa kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika ipasavyo na miradi inakamilika kwa wakati, akisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi bora unaongeza imani ya wananchi kwa Serikali.
Katika kuendeleza uwekezaji kwenye elimu, Prof. Shemdoe alitangaza kuwa Serikali imeidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za sekondari za sayansi katika kata za Dakawa na Mzumbe. Alisema hatua hiyo itapanua fursa za wanafunzi kupata elimu ya sayansi na kuchochea uzalishaji wa wataalamu watakaohitajika katika maendeleo ya taifa.
Aidha, aliwataka wenyeviti wa halmashauri na wakurugenzi watendaji kubuni mikakati ya kuvutia wawekezaji kutoka sekta binafsi, hususan katika sekta za elimu na afya, ili kusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi, kuboresha mazingira ya utoaji huduma na kufungua fursa zaidi za ajira na ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Sara Msafiri, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo wilayani humo. Pia aliomba Serikali itoe fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika Shule ya Sekondari Mkindo, akieleza kuwa wanafunzi wengi hutembea umbali mrefu kufika shuleni, hali inayoweza kuathiri mahudhurio na ufaulu wao.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Koira Majuka, alisema ujenzi wa Shule ya Sekondari Mkindo umeleta matumaini makubwa kwa wananchi, huku akiishukuru Serikali kwa kutoa shilingi milioni 528 kwa ajili ya mradi huo.
Pia, aliipongeza Benki ya CRDB kwa
kukubali kutoa kompyuta 50 ambazo zitasaidia kuimarisha matumizi ya TEHAMA na
kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Miradi hiyo inaendelea kuonyesha dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma za msingi kwa wananchi kupitia uwekezaji katika elimu na afya, huku ikiweka msingi wa maendeleo endelevu ya Wilaya ya Mvomero na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla.


No comments:
Post a Comment