Breaking News

Jul 17, 2026

Waandishi wa habari watakiwa kuondoa dhana potofu Nishati safi ya kupikia

                       NAIBU WAZIRI WA NISHATI,SALOME MAKAMBA

Waandishi wa habari watakiwa kuondoa dhana potofu

Na Mwandishi wetu

WAANDISHI wa habari wametakiwa kutumia taaluma yao kuandaa maudhui yenye ushahidi yatakayosaidia kuondoa dhana potofu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwajengea wananchi uelewa kuhusu faida zake kwa afya, uchumi wa familia na mazingira.

Wito huo umetolewa mjini Morogoro na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, Julai 15, 2026, wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari pamoja na maafisa mawasiliano kutoka wizara, taasisi za Serikali na sekretarieti za mikoa kuhusu uandishi na uhamasishaji wa masuala ya nishati safi ya kupikia.

Akizungumza katika warsha hiyo, Makamba alisema mafanikio ya ajenda ya nishati safi ya kupikia hayatapatikana kwa uwekezaji wa teknolojia pekee, bali yatachangiwa kwa kiwango kikubwa na mawasiliano yenye tija yatakayobadili mtazamo na tabia za wananchi.

Alieleza kuwa taarifa sahihi na zinazoeleweka kwa umma ndizo zitakazosaidia kuongeza matumizi ya nishati safi katika kaya za Watanzania na kuharakisha utekelezaji wa mkakati wa taifa.

"Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kujenga uelewa wa wananchi. Kupitia habari, vipindi vya redio na televisheni pamoja na majukwaa ya kidijitali, wanaweza kuhamasisha mabadiliko makubwa ya kijamii," alisema

Alisema maudhui yanayotolewa kupitia magazeti, redio, televisheni na mitandao ya kijamii yana uwezo mkubwa wa kuathiri maamuzi ya wananchi na hivyo yanaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko ya tabia.

Naibu Waziri wa Nishati,Salome Makamba kulia akipokea taarifa kutoka kwa mdau namna bora ya matumizi ya nishati safi ya kupikia,katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira inayotokana na 

Alielezea pia uuhimu wa sekta ya habari kwamba ina nafasi kubwa katika kufanikisha kimkakati katika kuongoza mapinduzi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, kwamba vyombo vya habari na maafisa mawasiliano kutumia taarifa sahihi kuhamasisha wananchi kubadili tabia za matumizi ya nishati na kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia..

Naibu Waziri huyo alisema hadi sasa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yamefikia asilimia 28.6 ya kaya, hatua aliyoitaja kuwa ni mafanikio yanayotoa matumaini, lakini akasisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha Tanzania inafikia lengo la asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Alisema kufikiwa kwa lengo hilo kunahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo, asasi za kiraia pamoja na vyombo vya habari.

Aidha, aliwataka maafisa mawasiliano wa Serikali kuhakikisha ujumbe wa nishati safi ya kupikia unaingizwa katika mipango ya mawasiliano ya taasisi zao na kuimarisha ushirikiano na Wizara ya Nishati katika kampeni mbalimbali za kitaifa.

Kwa mujibu wa Mhe. Makamba, matumizi ya nishati safi ya kupikia yanachangia kuboresha afya za wananchi kwa kupunguza magonjwa yanayosababishwa na moshi wa kuni na mkaa, kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti, kuchochea uwekezaji, kuongeza ajira na kuimarisha ustawi wa familia.

Naibu Waziri huyo aliwahimiza washiriki wa warsha kutumia maarifa watakayopata kuandaa habari na maudhui yenye ubora yatakayochochea matumizi ya nishati safi ya kupikia katika jamii.

Alisisitiza kuwa kila mwandishi wa habari na afisa mawasiliano anapaswa kuwa balozi wa mabadiliko kwa kutumia kalamu, kamera na majukwaa ya kidijitali kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa nishati safi kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.

 

No comments:

Post a Comment