Breaking News

Jul 17, 2026

Ziara ya Waziri wa Ujenzi yaonyesha dhamira ya Serikali kumaliza kero za barabara na madaraja Morogoro


 Ziara ya Waziri wa Ujenzi yaonyesha dhamira ya Serikali kumaliza kero za barabara na madaraja Morogoro

Na Thadei Hafigwa

Kwa miaka mingi, wakazi wa Mlimba, Malinyi na Ulanga mkoani Morogoro wameendelea kuishi na changamoto ya miundombinu duni ya barabara, hali inayokwamisha shughuli za kiuchumi, huduma za afya, elimu na usafirishaji wa mazao. Kipindi cha mvua kimekuwa kikiambatana na adha ya kukatika kwa mawasiliano kutokana na ubovu wa barabara na ukosefu wa madaraja ya kudumu.

Hata hivyo, ziara ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Hamis Ulega, katika maeneo hayo imeibua matumaini mapya kwa wananchi baada ya Serikali kuonyesha msimamo mkali dhidi ya ucheleweshaji wa miradi ya ujenzi na kusisitiza utekelezaji wa haraka wa miradi ya kimkakati.

Miongoni mwa miradi iliyozua mjadala mkubwa ni ujenzi wa barabara ya Ifakara–Mbingu yenye urefu wa kilometa 62.5, ambayo ni kiungo muhimu cha uchumi katika Jimbo la Mlimba.

Licha ya Serikali kusaini mkataba na kampuni ya Henan Railway Group takribani miaka miwili iliyopita na kutoa malipo ya awali ya zaidi ya Shilingi bilioni 9.58, utekelezaji wa mradi huo umekuwa wa kusuasua, jambo lililozua maswali mengi kutoka kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Morogoro.

Barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa inapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mpunga, mahindi, ufuta, mbao na mazao mengine ya biashara yanayochangia uchumi wa Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa ujumla.

Mbunge wa Mlimba apaza sauti

Katika ziara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Dkt. Kellen Rosemary Rwakatare, aliwasilisha kwa Waziri changamoto zinazowakabili wananchi kutokana na kuchelewa kwa mradi huo.

Alieleza kuwa wananchi wameendelea kupata hasara kubwa kutokana na ubovu wa barabara, huku gharama za usafiri zikiongezeka na usafirishaji wa mazao kwenda masokoni kuwa mgumu.

Mbunge huyo aliiomba Serikali kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuondoa adha ambayo wananchi wameivumilia kwa muda mrefu.

Serikali yatoa onyo kali kwa mkandarasi

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alionyesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa kazi licha ya Serikali kutimiza wajibu wake wa kifedha.

Alisema Serikali haiwezi kuvumilia hali ya kucheleweshwa kwa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi.

"Hivi hamuoni namna wananchi wanavyoumia? Serikali imeshatoa fedha lakini maendeleo ya mradi hayaendani na makubaliano ya mkataba. Hili hatuwezi kulivumilia."

Waziri Ulega alisema utekelezaji wa mradi huo umefikia takribani asilimia tano pekee, kiwango ambacho hakilingani na fedha zilizokwisha kulipwa.

Kutokana na hali hiyo, alitoa muda wa wiki moja kwa wataalamu wa Wizara ya Ujenzi na TANROADS kufanya kikao na viongozi wa kampuni ya Henan Railway ili kujadili hatma ya mradi huo.

Alisisitiza kuwa iwapo mkandarasi hataonyesha uwezo wa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba, Serikali haitasita kuuchukua hatua ikiwemo kuvunja mkataba na kuifungia kampuni hiyo kushiriki miradi mingine nchini.

Serikali ya Samia yaongeza kasi ya uwekezaji

Ziara ya Waziri Ulega imekuja wakati Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiendelea kuongeza uwekezaji mkubwa katika sekta ya miundombinu.

Katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi ya mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imeweka kipaumbele katika kujenga na kukarabati barabara za kitaifa, kujenga madaraja ya kudumu pamoja na kuhakikisha barabara zinapitika katika kipindi chote cha mwaka.

Mkakati huo unalenga kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko, kupunguza gharama za usafiri, kuongeza biashara na kuvutia wawekezaji.

Changamoto za Ulanga na Malinyi

Mbali na Mlimba, Waziri Ulega alitembelea pia wilaya za Ulanga na Malinyi kukagua maeneo yatakayojengwa madaraja.

Katika ziara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Salim Alaudin Hasham, aliwasilisha changamoto za wananchi zinazotokana na ubovu wa barabara na madaraja, hususan katika kipindi cha mvua ambapo baadhi ya vijiji hukatika mawasiliano kwa siku kadhaa.

Alieleza kuwa wananchi wanaendelea kuiunga mkono Serikali lakini wanatarajia kuona utekelezaji wa miradi ukienda kwa kasi zaidi ili kuondoa changamoto hizo.

Adam Malima: Morogoro ni mkoa wa kimkakati

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, alisema Morogoro ni miongoni mwa mikoa muhimu zaidi kiuchumi nchini kutokana na kuunganisha maeneo mengi ya uzalishaji wa kilimo na mtandao wa barabara za kitaifa.

Alisema Serikali imeendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, TANROADS na TARURA kuhakikisha changamoto za miundombinu zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, ujenzi wa madaraja katika maeneo yenye mito mikubwa utamaliza tatizo la kukatika kwa mawasiliano na kuboresha usalama wa wananchi pamoja na huduma za kijamii.

Miundombinu ni injini ya uchumi

Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa uwekezaji katika barabara na madaraja huongeza uzalishaji wa kilimo, hupunguza gharama za usafirishaji, huvutia uwekezaji na kuongeza ajira.

Kwa Mkoa wa Morogoro, ambao ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo nchini, barabara bora zina maana ya kuongeza ushindani wa mazao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Matumaini mapya

Ziara ya Waziri Abdallah Ulega imeonyesha kuwa Serikali haitaki kuona miradi ya maendeleo ikikwama kutokana na uzembe wa wakandarasi.

Hatua ya kutoa onyo kali kwa mkandarasi wa barabara ya Ifakara–Mbingu pamoja na kuendelea kusimamia ujenzi wa madaraja katika Ulanga na Malinyi imeongeza matumaini kwa wananchi kuwa kero za muda mrefu za miundombinu zinaelekea kupata ufumbuzi.

Iwapo maelekezo yaliyotolewa yatatekelezwa kwa wakati, siyo tu kwamba Mlimba, Malinyi na Ulanga zitafunguka kiuchumi, bali Mkoa wa Morogoro utaendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha uzalishaji wa kilimo, biashara na uwekezaji nchini.

No comments:

Post a Comment