Breaking News

Dec 9, 2021

WALIMU KILOSA WALIA NA MFUMO WA KIKOKOTO KWA WASTAAFU

 MWENYEKITI WA CWT MKOA WA MOROGORO,JUNANNE NYAKIRANG'ANI

WALIMU KILOSA WALIA NA MFUMO WA KIKOKOTO KWA WASTAAFU

Na Thadei Hafigwa                 

CHAMA cha walimu Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro kimesema hakiitaji sheria ya kikokotoo ambacho kinatarajiwa  kuletwa na serikali kwa wastaafu kama ambavyo hawakuhitaji bodi ya kitaaluma ya walimu kwa sababu sheria na kanuni zake ni kandamizi na mapungufu makubwa kwa walimu.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa chama cha Walimu CWT Wilaya ya Kilosa, Richarld Shagugu katika Mafunzo ya kuwajengea uwezo makatibu Tawi  CWT Wilayani humo  ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi  kwenye maeneo yao.

Mwalimu Shagungu amesema kuwa Walimu hawako tayari kuipokea  sheria hiyo kwa sababu hawajashirikishwa na kupewa elimu ya kutosha juu ya kikokotoo hicho kinachohusu mafao ya kustaafu.

Pamoja na hayo  amesema kuwa walimu wanachama  wanayo matarajio makubwa sana na chama chao  ikiwa ni pamoja na   kupata katiba mpya ya chama na mabadiliko ya mfumo wa chama kwa ujumla na kuongeza kuwa wanachama hawana matatizo katika utendaji wao wanachotaka ni kupewa elimu juu ya chama chao, kupewa huduma toshelezi  na kupata taarifa kwa uwazi bila kufichaficha.

 Mwenyekiti wa Chama cha Walimu CWT Wilaya ya Kilosa, Richarld Shagugu

hivyo,Shagungu ameipongeza serikali kwa kazi nzuri ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali Wilayani humo ambapo ameiomba serikali kujenga na Nyumba za walimu katika shule hizo.

Ameongeza kuwa,  CWT Kilosa imejipanga katika kutoa huduma bora kwa wanachama wakati wa shida na raha  na sasa kinachohitajika ni  usafiri wa Basi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanachama.

Naye, Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Morogoro, Mwalimu Jumanne Nyakirang’ani ambaye ndiye aliyekuwa Mgeni rasmi katika mafunzo hayo amewataka Makatibu tawi ambao ni wawakilishi wa cwt katika maeneo yao ya kazi kutimiza wajibu wao kwa kutekeleza majukumu waliyopewa ili chama kiendelee kuwa imara kwa mustabali wa taasisi hiyo.

Washiriki wa mafunzo  kwa makatibu tawi wa Chama cha Walimu(CWT KILOSA),wanaotoka katika Tarafa ya Kilosa mjini, Kimamba,Kidete, na Masanze wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wa chama hicho ngazi ya Wilaya na Mkoa wa Morogoro

Nyakirang’ani amesema kuwa walimu wanatakiwa  kujitetea, kujibrandi  kuwa bora zaidi na kutembea kifua mbele kwani taaluma waliyo nayo ni muhimu duniani kote kwa kuwa hakuna kiongozi yeyote ambaye hajapitia kwa walimu   huku akiwasihi kuacha mara moja tabia ya kutengeneza nyuso za kukoromewa  na watendaji ngazi ya kijiji na kata  hatimaye kukimbilia kwenda kushtaki  kwa katibu.

Mwalimu Nyakirang’ani,  amempongeza Waziri wa Elimu Ummy Mwalimu kwa kuzuia  walimu kufundisha nyakati za likizo na kuwashusha vyeo walimu wakuu na  waratibu ambao shule zao zimefelisha.

Aidha, Katibu wa CWT Wilaya  Kilosa Mwalimu Flola Malomele amewataka makatibu tawi  kuzingatia mafunzo hayo na kuwafundisha walimu ili waweze kujuwa wajibu wao wanapo kuwa  kazini.

Katibu wa CWT Wilaya  Kilosa, Mwalimu Flola Malomele

Mwalimu Malomele amesema mafunzo hayo ni ya awamu ya tatu katika mwendelezo wa mafunzo ikiwa katika utekelezaji wa maagizo ya uongozi wa Chama Taifa kwa  lengo la kujifunza.

Alisema kuwa mafunzo hayo yamefanyika kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza yalifanyika  mwezi oktoba katika  tarafa ya Magole, awamu ya pili yalifanyika mwezi Novemba tarafa ya Mikumi na ulaya  na awamu ya tatu  ni mwezi huu Disemba ambayo yamejumuisha  Tarafa ya Kilosa mjini, Kimamba,Kidete, na Masanze kwamba atahakikisha anakisimamia chama kuhakikisha kinatimiza malengo yake kwa maslahi mapana ya wanachama.

No comments:

Post a Comment