TAKUKURU YAGAWA VIFAA TIBA KUOKOA MAISHA YA WATOTO NJITI MOROGORO
Na Thadei Hafigwa
KUTOKANA na changamoto zinazoikabili sekta ya afya nchini, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeazimia kufanya matendo ya huruma kwa kugawa vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya kusaidia watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti) katika hospitali zote za rufaa nchini.
Hatua hiyo ilidhihirishwa mjini Morogoro wakati wa hafla ya kukabidhi mashine mbili za Phototherapy na Neonatal Radiant Warmer kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa hospitali hiyo pamoja na maafisa wa TAKUKURU kutoka ngazi ya mkoa na taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila, alisema msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha huduma za afya nchini, hususan huduma za mama na mtoto.
Chalamila alisema kuwa, menejimenti ya TAKUKURU ilifanya uamuzi huo kwa misingi ya utu, busara na hekima baada ya kubaini kuwa kuna uhitaji mkubwa wa vifaa tiba katika hospitali mbalimbali nchini, hususan vifaa vya kuwahudumia watoto njiti.
“Taarifa tulizozipata kutoka vituo vya kutolea huduma za afya zinaonesha kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa vifaa tiba, hasa mashine za kuwasaidia watoto njiti ili kunusuru maisha yao,” alisema Chalamila.
Alifafanua zaidi kwamba, ununuzi wa mashine hizo umewezeshwa na michango ya hiari kutoka kwa watumishi wa TAKUKURU, waliotoa sehemu ya mishahara yao, akibainisha kuwa taasisi hiyo haina mfuko maalumu wa uwajibikaji kwa jamii kama ilivyo kwa baadhi ya taasisi nyingine.
“Tupo katika zoezi la kugawa mashine za kuwasaidia watoto njiti katika hospitali zote za rufaa nchini. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ni hospitali ya kumi kufikiwa, na tunaendelea kufikia mikoa mingine hivi karibuni,” alisema Chalamila.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa Takukuru, hatua hiyo ni matendo ya huruma na hiyari kwa watumishi wa TAKUKURU, ambao wameguswa na uhitaji mkubwa uliopo katika jamii, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.
Naye, Kaimu Mratibu wa Huduma za Tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Azael Haward Kyando, alisema hospitali hiyo hupokea mara kwa mara idadi ya watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati, wakiwemo wenye uzito mdogo na wanaohitaji uangalizi wa karibu mara tu baada ya kuzaliwa jambo linaloashiria uwepo mkubwa wa tatizo hilo.
“Watoto njiti hukumbwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo kushindwa kudhibiti joto la mwili, hatari ya maambukizi, matatizo ya kupumua na changamoto za lishe. Endapo huduma sahihi haitapatikana kwa wakati, hatari ya vifo huongezeka,” alisema Dk. Kyando.
Kutokana na uwepo wa hali hiyo, alisema hospitali inahitaji kuongezewa mashine za Neonatal Radiant Warmer na Phototherapy ili kuongeza uwezo wa kuhudumia watoto wachanga, kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za mikoa jirani na kuboresha ubora wa huduma kwa ujumla.
kwa upande wake,Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Kessy Ngalawa, alisema mashine za Phototherapy na Radiant Warmer ni muhimu katika kudhibiti joto la mwili wa mtoto mchanga na kutibu homa ya manjano (jaundice), hali inayoweza kuhatarisha maisha endapo haitashughulikiwa kwa wakati.
Dk Ngawala alitaja kauli mbiu ya hospitali ya “Huduma Bora ni Kipaumbele Chetu.”,jambo linalowasukuma kuhakikisha wanawahudumia wananchi licha ya changamoto za kifedha na miundombinu, hospitali inaendelea kuboresha huduma kwa kuhakikisha watumishi wa afya wanafanya kazi kwa ufanisi na kuzingatia viwango vya kitaaluma.



No comments:
Post a Comment