TAKUKURU YAOKOA SH BILIONI 60.2, YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA
Na Thadei Hafigwa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imefanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 60.2 katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2025, kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi wa vitendo vya rushwa nchini.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila, wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika mkoani Morogoro, Januari 26, 2026.
Bw. Chalamila alisema fedha hizo zilirejeshwa Serikalini na nyingine kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ilivyokusudiwa, hatua iliyochangia kuimarisha ustawi wa wananchi na kulinda rasilimali za umma.
Alifafanua kuwa, katika kipindi hicho hicho, TAKUKURU ilifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 619 yenye thamani ya Shilingi bilioni 553.45 na kuokoa Shilingi milioni 173.5 zilizokuwa hatarini kupotea kutokana na vitendo vya rushwa.
“Mafanikio haya yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi pamoja na uwezeshaji mkubwa unaotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Bw. Chalamila.
Aliongeza kuwa TAKUKURU imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuzingatia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, inayotaka taasisi hiyo kushirikiana na wadau mbalimbali ili kutokomeza rushwa na kukuza utawala bora nchini.
Katika hatua ya kuimarisha uelewa wa jamii, TAKUKURU imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa kupitia mikutano ya hadhara, maonesho, vipindi vya redio na televisheni, semina, warsha pamoja na machapisho mbalimbali kuanzia vijijini hadi mijini.
Bw. Chalamila pia alisema TAKUKURU, kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), imefanikiwa kuingiza maudhui ya mapambano dhidi ya rushwa katika mitaala ya shule na vyuo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujenga kizazi chenye misingi ya uadilifu na uwajibikaji.
Kuhusu utekelezaji wa haki, alisema katika kesi 489 zilizoendeshwa mahakamani, Jamhuri ilishinda kwa asilimia 68.8 ya kesi zilizotolewa uamuzi, huku akieleza matumaini kuwa kiwango hicho kitaongezeka ifikapo Juni 2026.
Aidha, TAKUKURU iliendelea kujiimarisha kimataifa kupitia ushiriki wake katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambapo Tanzania iliongoza Kamati Ndogo ya Kupambana na Rushwa (SACC) na kushiriki katika ufuatiliaji wa chaguzi katika baadhi ya nchi wanachama.
Katika hotuba yake, Bw. Chalamila pia alieleza kuwa TAKUKURU inaendelea kutekeleza Programu ya TAKUKURU Rafiki inayolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika utoaji wa huduma za umma, ili kuzuia mianya ya rushwa kabla haijatokea.
Kwa upande wa uwajibikaji wa kijamii, alisema taasisi hiyo imeendelea kutoa msaada wa vifaa tiba kwa hospitali za rufaa, ikiwemo mashine za kuwahudumia watoto njiti, hatua inayolenga kuimarisha afya ya jamii na kudumisha uhusiano mwema kati ya TAKUKURU na wananchi.
Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la kila mmoja, akiwataka wananchi, vyombo vya habari, sekta binafsi na taasisi za umma kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kuzingatia kaulimbiu ya taasisi hiyo isemayo: “Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”


No comments:
Post a Comment