Breaking News

Jan 26, 2026

Serikali ya Awamu ya Sita inachukua Rushwa-Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU DKT.MWiGULU NCHEMBA

Serikali ya Awamu ya Sita Inachukia Rushwa-Waziri Mkuu

Na Mwandishi wetu,Morogoro

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma kwa kusisitiza misingi ya uadilifu, uwajibikaji na uwazi katika utendaji wa kazi serikalini.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka 2024/2025 wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) uliofanyika mkoani Morogoro, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Askofu wa Kanisa katoliki,jimbo la Morogoro,Mhashamu Lazarus Nsimbe(SDS) akisalimiana na mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Crispin Chalamila,muda mfupi baada ya mkutano mkuu wa mwaka 2024/2025 kufunguliwa mjini Morogoro.

Alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa TAKUKURU katika kudhibiti vitendo vya rushwa nchini, akibainisha kuwa bila uwepo wa taasisi hiyo, rushwa ingeathiri kwa kiwango kikubwa utoaji wa huduma muhimu za kijamii kwa wananchi.

“Watanzania tunawapenda TAKUKURU. Ni taasisi muhimu katika kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha haki inatendeka,” alisema Dkt. Nchemba, huku akiwataka wananchi kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa wakati
Aidha, aliwataka viongozi na watumishi wa TAKUKURU kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na ujasiri, akisisitiza kuwa kazi wanayoifanya ni kwa maslahi mapana ya taifa.

Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa viongozi wa TAKUKURU nchini wakifuatilia kwa karibu hotuba ya Mgeni Rasmi,Waziri Mkuu Dkt.Mwibulu Lameck Mchumba(hayupo pichani)

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliipongeza TAKUKURU kwa mafanikio makubwa ya kuokoa shilingi bilioni 60.2 za fedha za umma katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025. Alisema kati ya kesi 489 zilizofikishwa mahakamani, asilimia 68.8 Jamhuri imeshinda, jambo linaloonesha ufanisi wa taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwezeshaji wa Serikali pamoja na msukumo wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia misingi ya uwajibikaji na utawala bora.

Dkt. Nchemba alionya kuwa rushwa inadhalilisha utu wa mwananchi, inadhoofisha utoaji wa huduma za kijamii na kuinyima nchi rasilimali muhimu kwa maendeleo. Kutokana na hali hiyo, aliwahimiza wadau wa elimu kuwajengea watoto mashuleni maadili ya kuchukia rushwa tangu wakiwa wadogo.

Pia aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuharakisha usikilizwaji wa mashauri ya rushwa na kutoa maamuzi kwa wakati, hali inayochangia kuongeza imani ya wananchi katika mfumo wa haki.

Akizungumzia mianya ya rushwa, Waziri Mkuu alisema upotevu mkubwa wa fedha za umma unatokea katika maeneo ya makusanyo na matumizi ya fedha, hasa pale ambapo kunakuwa na mwingiliano wa moja kwa moja kati ya watu na fedha. Alisisitiza umuhimu wa kuziba mianya hiyo kwa kuboresha mifumo na kurekebisha sheria.

Aliitaka pia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kushirikiana kwa karibu na TAKUKURU ili kudhibiti rushwa na kuimarisha uwajibikaji miongoni mwa viongozi wa umma.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, baadhi ya miradi ya maendeleo husuasua kutokana na fedha kugawanywa kabla ya utekelezaji, akibainisha kuwa suluhisho ni kuimarisha mifumo ya kisheria na kiutawala ili kuboresha utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya, maji na miundombinu ya barabara.

Mkutano huo umehudhuriwa na washiriki 282 kutoka Tanzania Bara pamoja na viongozi saba kutoka Ofisi ya TAKUKURU Zanzibar, hatua inayolenga kuimarisha mshikamano na ufanisi wa mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,  Crispin Chalamila, alisema mkutano huo unawakutanisha jumla ya viongozi 234 wa TAKUKURU kutoka Makao Makuu, mikoa, wilaya na vituo maalum, pamoja na viongozi saba kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA).

Chalamila alitumia fursa hiyo kumtambulisha mgeni rasmi na viongozi mbalimbali wa TAKUKURU, akibainisha kuwa taasisi hiyo pia inashirikiana na wadau wa kikanda na kimataifa katika mapambano dhidi ya rushwa.

Naye Waziri wa nchi,ofisi ya Rais,utumishi na utawala bora,Ridhiwan Kikwete alisema ya kuwa TAKUKURU imekuwa ikiwezeshwa mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba kasi ya utendaji wao wa kazi inakuwa na tija kwa nchi kwa kila wilaya kupatiwa gari moja na magari mawili kwa kila mkoa. 
Kikwete alisema kuwa hatua ya serikali kuweka nguvu katika kuimarisha utendaji wa kazi takukuru ni wazi kilichopo ni kusubiri matokeo chanja kutokana na uwekezaji wa miundombinu ya majengo,na kuongeza rasilimali watu uweze kuleta matokeo chanja na tija kwa taifa.

No comments:

Post a Comment