MATULI CBO YAZINDULIWA RASMI, YAAHIDI KUHAMASISHA MAENDELEO YA JAMII NA UHIFADHI WA MAZINGIRA
Na Mwandishi Wetu
Hatua mpya ya kuhamasisha maendeleo ya jamii imeanza kushika kasi kufuatia uzinduzi rasmi wa Matuli Community Based Organization (Matuli CBO),iliopo Kata ya Matuli, Halmashauri ya Wilaya Morogoro, taasisi ya kijamii inayolenga kutumia fursa zilizopo katika hilo, ikiwemo rasilimali za misitu, kukuza ujasiriamali kwa vijana na kuendeleza miradi ya uhifadhi wa mazingira.
Uzinduzi huo ulifanyika kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo, huku mgeni rasmi akiwakilishwa na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Matuli, Mohaned Rashid Chenga, ambaye alipongeza uanzishwaji wa taasisi hiyo kwa kueleza kuwa ni jukwaa muhimu la kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana pamoja na kuinua kipato cha wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Matuli CBO, Moses Chunga, alisema taasisi hiyo imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira, ujasiriamali, kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi pamoja na lishe bora mashuleni kwa njia ya jamii jumuishi.
Alifafanua kuwa Matuli CBO itaongozwa na dira ya kuunga mkono malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kwa kuhakikisha jamii inatumia rasilimali zake kwa tija bila kuharibu mazingira.
“Tutahamasisha vijana kuunda vikundi vya uzalishaji mali na kuomba mizinga kwa ajili ya ufugaji nyuki katika msitu wa Matuli, kama sehemu ya kuongeza kipato na kulinda misitu yetu. Pia tuna mpango wa kuanzisha mradi wa kaboni utakaosaidia kuhifadhi mazingira na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” alisema Chunga.
Kwa upande wake, Deograsia Mallya Mratibu wa Miradi wa Matuli CBO aliwataka vijana kutumia fursa hiyo kwa kujiunga na vikundi vitakavyowezeshwa kupata mafunzo na mitaji midogo, akisisitiza nidhamu, uwajibikaji na mshikamano kama msingi wa mafanikio ya miradi ya kijamii.
Katika hafla hiyo, Matuli CBO pia ilinadi sera yake ya kusaidia vijana katika sekta ya sanaa, ujasiriamali na utunzaji wa mazingira. Aidha, taasisi hiyo imeahidi kumleta mdhamini wake, kampuni ya Farmer Center Limited, inayojihusisha na viuatilifu, ili kutoa elimu bure kwa wakulima na wafugaji wa Matuli kuhusu kilimo bora, matumizi sahihi ya viuatilifu na mbinu bora za ufugaji.
Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo walieleza matumaini yao kuwa taasisi hiyo itakuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa vijana na wakulima, hasa katika kipindi ambacho changamoto za ajira na mabadiliko ya tabianchi zimeendelea kuathiri uzalishaji na kipato cha kaya nyingi.
Kwa uzinduzi huo, Matuli CBO imeanza safari ya kuhamasisha maendeleo ya jamii kwa vitendo, kwa lengo la kujenga jamii yenye uchumi imara, mazingira salama na kizazi chenye maarifa ya kujitegemea.




Kazi nzuri sana nawapongeza CBO Matuli
ReplyDelete