Na Hawa
Mikidadi
Baadhi ya maeneo nchini Tanzania kumekuwa na mila na tamaduni
ambazo zimekuwa kikwazo katika elimu hasa kwa watoto wa kike ambazo zinaleta
athari chanya kwa jamii inayomzunguka
mtoto wa kike.
Katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.Samia
Suluhu Hassan mikoa ya Lindi na
Mtwara iliyofanyika septemba 26,2023 moja ya mambo yaliyomgusa ni pamoja na
hali duni ya elimu kwa watoto wa kike na kuwataka wananchi wa mikoa ya kusini
kuwaacha watoto wasome na kutilia mkazo watoto wa kike.
Licha ya kuwepo sababu nyingi zinazowasukuma wasichana
kukatisha masomo katika mikoa ya kusini ,mila na desturi zimekuwa zikichangia
kwa kiasi kikubwa kutokea kwa hali hiyo,utamaduni wa jamii kuwacheza ngoma
wasichana wakiwa katika umri mdogo ni moja ya mambo yanayosababisha mimba kwa
wanafunzi.
Aidha,ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za
serikali kwa mwaka wa fedha 2021-2022 inaonyesha uwepo wa idadi kubwa ya
wanafunzi wanaokatisha masomo katika mikoa hiyo ya kusini mwa nchi, ya elimu
msingi (BEST2023),inaonyesha jumla ya wanafunzi wa sekondari 5736 walikatisha
masomo mkoani Mtwara na wanafunzi 4875 mkoani Lindi.
Rais Samia alitumia ziara hiyo kuwataka wananchi wa mikoa ya
kusini kuwaacha watoto wa kike wasome ambao ndiyo wamekuwa waathirika wa
kukatishwa masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ndoa na mimba utotoni.
“Niwaombe sana waacheni wasichana wasome ,shule ile ya
wasichana ni maalumu kwa wenye vipaji vya sayansi huko ndipo tutapata walimu
,madaktari na wataalamu mbalimbali “alisema.
Akizungumzia hilo mkurugenzi wa chama cha wanahabari wanawake
Tanzania(Tamwa) Dk Rose Reuben,anasema kinachofanywa na Rais ni uwajibikaji wa
wazi katika kuhakikisha serikali inamuondolea mwanamke utegemezi.
Mbali na kuondoa utegemezi kwa wanawake Dk Rose anasema hatua
hizo zinazoendelea kuchukuliwa na Rais Samia ,zinalenga kumsaidia mtoto wa kike
kupata elimu katika mazingira bora bila kukumbana na vikwazo.
Kwa upande mwingine ,Mkuu wa kitengo cha mawasiliano shirika
la msichana Initiative Sara Beda,hivi karibuni alinukuliwa na vyombo vya habari
akisema upo umuhimu kwa jamii kutumia fursa zinazotolewa na serikali katika
kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu .
“Msichana Initiative tunapongeza jitihada zinazofanywa na
serikali kumkomboa mtoto wa kike katika elimu ,kwa kuwa tunaamini kwamba ndiyo
njia ya kumwezesha kutimiza ndoto zao.”anasema Sara Beda.
Viongozi na vyombo mbalimbali wanatilia mkazo mila na tamaduni potofu
zinazomnyima haki ya elimu mtoto wa kike zinaondolewa katika jamii, ambapo
baadhi ya kampeni zilizoanzishwa ni kama Muache asome iliyosaidia jamii kuamka
kupeleka mtoto wa kike shuleni badala ya kumuozesha katika umri mdogo.
Aidha, ripoti ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inaonyesha
mkoa wa Mtwara una jumla ya watu 1,634,947 kutoka 1,270,854 wa sensa ya mwaka 2012 na mkoani Lindi ina idadi ya watu 1,194,028
kutoka watu 864,652 sensa ya mwaka 2012.
Pia, katika hali ya kielimu mkoani Mtwara na Lindi kumekuwepo tamaduni za kuozesha watoto wa
kike na kutoipa kipaumbele elimu ya
mtoto wa kike ,uhamasishaji wa wazazi kuhusu elimu bado upo chini.
Kupitia mila na tamaduni za mikoa ya kusini kumekuwa na
athari mbalimbali zinazotokana na tamaduni hizo ambazo moja kwa moja
zinamuathiri mtoto wa kike ikiwepo ndoa na mimba za utotoni,kuhamasisha mapenzi
ya mapema kwa kujijua washakuwa watu wazima .
Kwa mujibu wa sera elimu ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023
inasema wazazi na walezi ni wadau muhimu katika kuimarisha maendeleo ya elimu
kwa wanafunzi ili kufanikisha hilo ushirikiano kati ya mzazi,mlezi,walimu na
uongozi wa shule ni muhimu kufuatilia nidhamu maadili na mwenendo wa kitabia wa
mtoto wake.
Kwa mujibu wa ilani ya chama cha mapinduzi ,serikali
imeimarisha miundombinu ya shule za sekondari kwa kujenga shule 26 za sekondari
za wasichana za kidato cha tano na sita katika mikoa 26 nchini ili kuhakikisha
wanafunzi wa kike wanapata elimu bora.
Ilani ya chama cha mapinduzi pia imeongeza nafasi za
wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi na hisabati katika shule za sekondari
hususani watoto wa kike.
Sanjari na kuboresha
mbinu na mikakati ya utoaji wa elimu nje ya mfumo rasmi (MEMKWA)ili kuwawezesha
waliokosa fursa au kupoteza sifa za kusoma katika mfumo rasmi kuweza kutimiza
ndoto zao za kielimu na kuchangia ipasavyo katika ujenzi wa Taifa.
Vile vile, kuhahikisha mfumo mzima wa elimu unajengwa kwa
umadhubuti na kuzingatia utamaduni,mila na desturi za kitanzania na kuimarisha
masomo ya maadili ,uzalendo wa kitaifa na uraia kwa shule zote nchini.

No comments:
Post a Comment