Breaking News

May 28, 2025

SUGECO YABAINISHA VIJANA 850 WANUFAIKA NA USHIRIKIANO NA NCHI ZA NORDIC

 Maafisa Ubalozi wa Nchi za NORDIC wakiwa katika ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA),Prof.Raphael Kibunda akiongea na wageni wake,waliotembelea ofisini kwake na kufanya mazungumzo.

SUGECO YABAINISHA VIJANA 850 WANUFAIKA NA USHIRIKIANO NA NCHI ZA NORDIC


Na Thadei Hafigwa,Morogoro

TAASISI ya  Wajasiriamali Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO) kimefungua ukurasa mpya wa maendeleo kwa vijana na wanawake nchini kupitia mpango kabambe wa ushirikiano kati yake na nchi za Nordic ambazo ni Denmark, Finland, Norway, na Sweden.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA),Prof.Raphael Kibunda ameonesha shukran zake kwa nchi za Nordic kwa kusaidia Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo katika ukuzaji na uendelevu wa kitaaluma katika programu mbalimbali za kubadilishana uzoefu.

Prof.Kibunda ametaja nchi ya Denmark imekuwa ni nchi ya kwanza kufadhili ndaki ya tiba ya mifugo,ambapo kwa walikuwa wakileta walimu kwenye tiba ya wanyama kwa kuwafundisha wanafunzi chuoni hapo,ambapo kwa sasa wanaendelea vizuri.

"tunawashukuru kwa kipindi chote hicho,kwa sasa tumesimama wenyewe,tuna walimu wetu wenyewe,tumekubaliana tuwe na uwezo wa kubadilishana wanafunzi na pia kubadilishana walimu."alisema Prof.Kibunda.

kwa upande wake,Balozi wa Denmark Nchi Tanzania,Jesper Kammersgaard,alisema kuwa Nchi za Nordic zimekuwa na utarabu wa kukuza ujasiriamali katika kilimo,ambapo wameweza kukutana na vijana 20 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA) ambao waliwahi kujifunza ujuzi nchini Denmark ambao wamerudi Tanzania ili kujua namna wanavyotumia ujuzi na maarifa waliyapata wakiwa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa SUGECO, Revocatus Kimario kwa Ubalozi wa Nchi za Nordic waliotembelea Taasisi hiyo iliopo ndani ya Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) ambayo inafadhiliwa na  nchi hizo za Nordic ambapo katika kipindi cha miaka miwili,jumla ya vijana 850 kutoka chuo kikuu wamenufaika na Programu ya kujifunza nje ya nchi katika nchi hizo.

Kimario alibainisha kuwa SUGECO inalenga kushirikiana na taasisi na vyuo vikuu kutoka nchi hizo katika maeneo mbalimbali muhimu ya maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na elimu, ujasiriamali, uhifadhi wa mazingira, na teknolojia ya kisasa ya kilimo na mifugo.

Mikakati ya Kuwezesha Vijana na Wanawake

SUGECO inatilia mkazo ushirikiano katika nyanja ya elimu kwa kupendekeza mpango wa kubadilishana wanafunzi na programu za mafunzo kwa vitendo (internship), pamoja na kuanzisha shahada ya pamoja ya "sandwich" kati ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na vyuo vya Nordic. Lengo ni kuongeza ujuzi na uzoefu wa kimataifa miongoni mwa vijana wa Kitanzania katika sekta ya kilimo, misitu, na biashara endelevu.

Aidha, taasisi hiyo inapendekeza kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo kwa wajasiriamali vijana na wanawake kwa kushirikiana na taasisi za maendeleo kutoka Nordic. Mfuko huo utasaidia vijana waliomaliza mafunzo kwa vitendo kuingia katika biashara zenye tija, huku pia ukianzisha mfumo wa kifedha wa mzunguko kwa ajili ya biashara zinazoongozwa na vijana.

Mkurugenzi Mtendaji wa SUGECO, Revocatus Kimario akitoa maelezo kwa Baadhi ya Maafisa Ubalozi wa Nchi za Nordic,juu ya miradi inayofadhiliwa na nchi hizo.

Mfumo wa Kizimba na Programu ya Kuendeleza Biashara

Kupitia Kizimba Business Model, SUGECO imeanzisha mfumo maalum wa kuwasaidia vijana wajasiriamali kukuza miradi endelevu kupitia ushauri, msaada wa kiufundi, na upatikanaji wa masoko. Taasisi hiyo sasa inatafuta ushirikiano kutoka Nordic ili kupanua mfumo huu na kuwaunganisha vijana na masoko ya kimataifa pamoja na mbinu bora za biashara endelevu.

Katika hatua nyingine, Youth Acceleration Program ya SUGECO inalenga kusaidia biashara changa zinazoongozwa na vijana kwa kuzikuza, kuzilea na kuzihusisha na masoko, kwa kushirikiana na makampuni ya Nordic katika kutoa msaada wa kifedha, kiufundi na kiushauri.

Uhifadhi wa Mazingira na Teknolojia ya Kisasa ya Mifugo

Katika kuunga mkono jitihada za kimataifa za uhifadhi wa mazingira, SUGECO inakusudia kushirikiana na Bamboo Village Trust kutoka Indonesia pamoja na wataalamu wa Nordic kuendeleza mradi wa uhifadhi wa mianzi nchini. Mradi huu pia utahusisha kubadilishana wanafunzi kati ya SUA na vyuo vya Nordic katika masuala ya misitu na usimamizi wa rasilimali endelevu.

Kwa upande wa teknolojia ya kisasa ya mifugo, SUGECO imeingia ubia na kampuni ya Danben kutoka Denmark kuanzisha kituo cha kisasa cha uhimilishaji bandia wa nguruwe. Mradi huu utasaidia kuongeza tija kwa wakulima wadogo, kuboresha vinasaba vya mifugo, na kutoa ajira na mafunzo kwa vijana katika teknolojia za kisasa za ufugaji.

Manufaa kwa Nchi Washirika

Kwa mujibu wa SUGECO, nchi za Nordic zitafaidika kwa kuimarisha uhusiano wa kielimu na kiteknolojia na Tanzania, kupata fursa za uwekezaji katika masoko yanayoibukia, na kushiriki moja kwa moja katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu duniani.

“Tunayo matumaini makubwa kwamba ushirikiano huu utaleta mabadiliko chanya ya muda mrefu kwa vijana, wanawake, jamii, na mazingira kwa ujumla,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo. “Tunasubiri kwa hamu kujadiliana kwa kina juu ya fursa hizi na kupata msaada wa wenza wetu ili kufanikisha malengo haya ya pamoja.”

Kwa mafanikio haya, SUGECO inaendelea kudhihirisha kuwa taasisi muhimu katika kuibua na kukuza vipaji vya vijana wa Kitanzania na kuwaunganisha na fursa za kimataifa kwa maendeleo jumuishi na endelevu.

No comments:

Post a Comment