Serikali
Yapongeza CAMFED Tanzania kwa Uwekezaji Madhubuti katika Maendeleo ya Wasichana
Na
Thadei Hafigwa, Morogoro
Serikali
kupitia Ofisi ya Elimu Mkoa wa Morogoro imepongeza Shirika la CAMFED Tanzania
kwa mchango mkubwa katika kuwawezesha wasichana kielimu, kijamii na
kiuchumi—juhudi zinazotajwa kuwa nguzo muhimu katika ustawi wa taifa.
Pongezi
hizo zilitolewa kupitia hotuba ya Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro, iliyosomwa
kwa niaba yake na Bi. Rhoda Sheba, Afisa Elimu wa Watu Wazima, Elimu Nje
ya Mfumo Rasmi na Elimu Maalum,Mkoa wa Morogoro wakati wa ufunguzi wa Kongamano la mafunzo maalum kwa wasichana waliomaliza
sekondari na kufadhiliwa na CAMFED,iliyojumuisha Wilaya za Iringa,KILOLO,Chamiwino,Morogoro
vijijini,Mlimba ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kujiunga na vyuo vya kati na
vyuo vikuu.
“CAMFED
siyo tu inatoa ufadhili wa masomo, bali inajenga mfumo wa ufuatiliaji wa
maendeleo ya kielimu na maisha ya baadaye ya wanufaika wake. Huu ni mfano wa
kuigwa katika kujenga kizazi imara cha wasomi na viongozi wa kesho,” alisema
Bi. Sheba.
Aliongeza
kuwa amewahi kushuhudia mnufaika wa CAMFED aliyekuwa likizo kutoka chuo kikuu
akijitolea kuwahamasisha na kuwaelekeza wasichana walioko sekondari—ishara ya
ushawishi chanya wa mpango huo katika kuendeleza mnyororo wa mafanikio.
Takwimu
za mwaka 2024 zinaonesha kuwa CAMFED Tanzania imefadhili zaidi ya wasichana 154,201,
na idadi hiyo imeokwenda sambamba na ngezeko la ufaulu katika mitihani yao ya
kidato cha nne katika elimu ya sekondari, hatua iliyopokelewa kwa shangwe na
pongezi kutoka kwa washiriki wa Kongamano hilo.
“Ni jambo la kujivunia kuona idadi kubwa ya watoto wa kike wakifanikiwa licha ya changamoto lukuki zinazowakabili. Mafanikio haya yanaonesha wazi kuwa uwekezaji kwa mtoto wa kike ni uwekezaji wenye tija kwa taifa,” aliongeza Bi. Sheba.
Washiriki wa Kongamano la Mafunzo maalum kwa Wanachuo tarajali,lilikofanyika katika shule ya Sekondari ya Kilakala,Morogoro wakifuatilia kwa umakini hotuba ya Mgeni Rasmi.Mafunzo na Uwezeshaji wa Viongozi wa Baadaye
Mbali
na ufadhili wa masomo, CAMFED Tanzania inatekeleza programu mbalimbali za
kuwajengea uwezo wasichana katika uongozi, ujasiriamali, na stadi za maisha
kupitia kwenye shule za sekondari.
Akizungumza
katika Kongamano hilo la mafunzo, Mkuu wa Idara ya Miradi wa CAMFED Tanzania, Bi.
Dominica Lyambo, alibaisha program ya kuwajengea uwezo wasichana uwezo
kuelekea kujiunga na vyuo ni shule ya sekondari Kilakala (Morogoro), Ng’anza
(Mwanza), na Shule ya wasichana ya Mkoa wa Pwani.
Lyambo alisema shirika hilo linafanya kazi katika nchi tano za Afrika ambazo ni Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Ghana, na Malawi.
Mkuu wa Idara ya Miradi wa CAMFED Tanzania, Bi. Dominica Lyambo akiwasilisha taarifa yake,Mjini Morogoro katika Kongamano la wasichana ambao ni wanachuo tarajali wanaofadhiliwa na shirika lake“Tanzania
tulianza mwaka 2005 na tumesajiliwa rasmi mwaka 2006. Kwa sasa tunafanya kazi
katika mikoa 10 na halmashauri 35, huku lengo la mwaka 2025 likiwa ni kufikia
halmashauri 41,” alisema Bi. Lyambo.
Aliongeza
kuwa CAMFED tayari imefikia halmashauri zote katika mikoa ya Dar es Salaam na
Morogoro, na kazi inaendelea katika mikoa mingine ili kufanikisha lengo la
kufikia halmashauri zote 76 zilizopo kwenye mikoa hiyo 10.
Uwajibikaji na Ulinzi wa Mtoto
Kwa
mujibu wa Bi. Lyambo, utekelezaji wa miradi ya CAMFED unazingatia misingi ya
utawala bora, ikiwemo sera ya ulinzi wa mtoto, usimamizi wa rasilimali, na
uwajibikaji wa kifedha. Aidha, shirika hilo linafanya kazi kwa karibu na wadau
kutoka ngazi ya kijiji hadi wizara, wakiwemo maafisa ustawi wa jamii, kamati za
shule, na maafisa elimu kata.
“Tunaamini
mtoto wa kike akipewa mazingira salama ya kusoma, akiheshimiwa na kuthaminiwa,
ana nafasi kubwa ya kufikia ndoto zake na kuondokana na umaskini,” alieleza.
Bi.
Lyambo pia alibainisha kuwa mafanikio ya CAMFED yametokana na ushirikiano mzuri
na wanachama wa CAMFED Association—ambao ni wanufaika waliorejea kuleta
mabadiliko katika jamii zao.
Sauti za Wanufaika
Mmoja
wa wanufaika wa mpango huo, Salma Salum, alieleza kuwa CAMFED imekuwa
msaada mkubwa katika maisha yake kwa kumwezesha kielimu na kumwandaa kiakili na
kisaikolojia kwa safari ya elimu ya juu.
“Ninaishukuru
CAMFED kwa kutuwezesha siyo tu kielimu, bali pia kwa kutujengea uwezo wa
kukabiliana na changamoto tunazokutana nazo tunapoingia vyuoni,” alisema.
Je, Wavulana Watasahaulika?
CAMFED ilifafanua kuwa kwa sasa mpango huo umejikita kwa wasichana kutokana na changamoto maalum wanazokumbana nazo, lakini mjadala huo umefungua fursa ya kutafakari upanuzi wa wigo wa mnufaika katika siku zijazo.



No comments:
Post a Comment