Waandishi wa Habari Wanawake Wajengewa Uwezo wa Kujilinda Mtandaoni na Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia
Na Mwandishi wetu, Morogoro
WAANDISHI wa habari wanawake kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar wanapatiwa mafunzo ya siku nne kuhusu usalama wa kidijitali na mbinu za kukabiliana na ukatili wa kijinsia mtandaoni, lengo likiwa ni kuwawezesha kujilinda na kutekeleza majukumu yao kwa usalama katika mazingira ya kidijitali yanayoendelea kubadilika kwa kasi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo mjini Morogoro, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari wanawake kufanya kazi kwa weledi ili kuhimili ushindani katika soko la habari linaloongozwa na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Teknolojia imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya habari. Sasa mwandishi anaweza kuripoti kutoka mahali popote kupitia majukwaa ya kidijitali. Ni muhimu waandishi wanawake nao wawe sehemu ya mapinduzi haya kwa kumiliki na kuendesha vyombo vya habari vya mtandaoni,” alisema Simbaya.
Ameongeza kuwa, licha ya hofu za awali kuhusu matumizi ya intaneti, hivi sasa teknolojia hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya kurahisisha upashanaji wa taarifa, huduma za kifedha, na mawasiliano kwa ujumla. UTPC itaendelea kuhakikisha kuwa klabu za waandishi nchini zinaendelea kwenda sambamba na kasi ya maendeleo hayo ya kidijitali.
Baadhi ya Washiriki wa mafunzo kwa Waandishi wa Habari Wanawake juu ya athari za ukatili wa kijinsia mitandaoni yaliondaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)Kwa upande wake, Lilian Lucas, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mjumbe wa Bodi ya UTPC, alisema kuwa mafunzo hayo yamewaleta pamoja waandishi wa habari wanawake kutoka mikoa 25 ya Tanzania, yakiwa na lengo la kuongeza uelewa kuhusu changamoto na athari za ukatili wa kijinsia mtandaoni.
“Ukatili wa kijinsia mtandaoni ni kikwazo kikubwa kwa uhuru wa kujieleza, ushiriki wa wanawake katika mchakato wa kidemokrasia, na heshima ya wanawake na wasichana katika jamii. UTPC ina jukumu la kuhakikisha kuwa waandishi wanawake wanakuwa na maarifa ya kutosha ya usalama wa kidijitali. Hili si jambo la hiari tena, bali ni hitaji la lazima,” alisema Lilian.
Lilian Lucas, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mjumbe wa Bodi ya UTPC.
Alisisitiza kuwa washiriki wa mafunzo hayo wanapaswa kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya, si tu katika maisha yao binafsi, bali pia katika namna wanavyoripoti habari zinazogusa sera, maisha ya watu, na kuleta mabadiliko katika jamii.
Victor Maleko, Afisa Programu wa Mafunzo na Machapisho kutoka UTPC, alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha waandishi wanawake kutambua hatari zilizopo katika mazingira ya mtandaoni na kujifunza mbinu mbadala za kujilinda.
“Usalama wa mwandishi unaanzia kwake mwenyewe. Mwandishi anaposhiriki kuripoti, hususan katika muktadha wa uchaguzi au maandamano, ni muhimu kuvaa mavazi yasiyoonesha upendeleo wa kisiasa na kuwa katika maeneo salama yanayowezesha kuondoka haraka endapo hali ya usalama itakuwa hatarishi,” alisema Maleko.
Mafunzo haya yameandaliwa na UTPC kwa ushirikiano na mashirika ya International Media Support (IMS), Jamii Forums, Nukta Africa, na TAMWA. Maleko alitoa wito kwa vyombo vya usalama na vyama vya siasa kutambua wajibu wao katika kuwalinda waandishi wa habari, hasa wanawake ambao mara nyingi hukumbana na madhila zaidi wanapotekeleza majukumu yao ya kitaaluma.
Kwa mujibu wa takwimu za UTPC, mwaka 2024 kulirekodiwa matukio 20 ya ukatili dhidi ya waandishi wa habari, yakiwahusisha waandishi 28. Mwaka 2023, matukio yalipungua hadi 18, huku mwaka 2021/2022 yakifikia 23. Upungufu huo unahusishwa na ongezeko la mafunzo kuhusu ulinzi na usalama kwa wanahabari.
Hata hivyo, taarifa kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) zinaonesha kuwa mwaka 2023 pekee, asilimia 77 ya waandishi wa habari wanawake waliripoti kukumbwa na aina fulani ya ukatili, hususan kupitia mitandao ya kijamii.



No comments:
Post a Comment