Breaking News

Jun 5, 2026

TAKUKURU MOROGORO YAFUATILIWA MIRADI YA MAENDELEO YA BILIONI 15.7

Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga

Na Thadei Hafigwa

NAIBU Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga, amesema katika eneo la ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma, TAKUKURU Morogoro imeendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.

Mwakajinga amebainisha hayo wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake,akitoa taarifa ya miezi mitatu,mwezi Januari hadi Machi,2026 katika kipindi hicho, taasisi hiyo ilifuatilia matumizi ya zaidi ya Shilingi Bilioni 15.7 zilizotumika katika utekelezaji wa miradi 34 ya maendeleo katika sekta za elimu, afya na maji.

Aidha, TAKUKURU ilifuatilia miradi minane yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2.7, ambapo mapungufu mbalimbali yalibainika na ushauri wa kitaalamu kutolewa kwa mamlaka husika ili kurekebisha changamoto hizo kabla hazijaleta hasara kwa Serikali. 

“Lengo letu ni kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi zinatumika kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha,” alisema.

 Baadhi ya waandishi wa habari wa Morogoro wakifuatilia taarifa ya TAKUKURU . 

Katika jitihada za kuzuia rushwa kabla haijatokea, TAKUKURU Morogoro imeendelea kutoa elimu kwa wananchi, watumishi wa umma, sekta binafsi, vijana na makundi mbalimbali ya kijamii kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa kuzingatia maadili.

Mwakajinga alisema katika kipindi hicho taasisi hiyo ilifanya semina 74, mikutano ya hadhara 19, pamoja na kuimarisha na kufungua klabu za wapinga rushwa 100 katika shule na taasisi mbalimbali.

Aliongeza kuwa vipindi vya redio na ushirikiano na wadau mbalimbali vimeendelea kutumika kama njia muhimu ya kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuongeza mwamko wa kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.

Kuhusu uchunguzi wa malalamiko, Mwakajinga alisema TAKUKURU Morogoro imepokea jumla ya malalamiko 94 katika kipindi hicho.Alifafanua kuwa kati ya malalamiko hayo, 65 yalihusu tuhuma za rushwa na yanaendelea kufanyiwa kazi katika hatua mbalimbali za uchunguzi, huku 29 yakihusu masuala yasiyo ya rushwa na hivyo kupelekwa katika mamlaka husika kwa hatua stahiki.

“Tunaendelea kuwahimiza wananchi kutoa taarifa za viashiria vya rushwa mapema ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wakati,” alisema.

 Mwakajinga alisema TAKUKURU Morogoro imejipanga kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kuandaa vipindi vya elimu kwa umma vitakavyosaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya rushwa na wajibu wao katika kuzuia vitendo hivyo. 

Pia taasisi hiyo imepanga kuanzisha klabu zaidi za wapinga rushwa katika taasisi za elimu ili kujenga kizazi chenye maadili, uwajibikaji na uzalendo.

Akihitimisha taarifa yake, Mwakajinga aliwataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa za viashiria vya vitendo hivyo kwa wakati.

Alisema kuwa Mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi. Kila mmoja ana wajibu wa kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha haki inatendeka.

No comments:

Post a Comment