Na Thadei Hafigwa
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amezitaka Kamati za Usimamizi wa Maafa kuimarisha maandalizi na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa kunyesha mwishoni mwa mwaka 2026.
Kilakala ametoa agizo hilo Septemba 7, 2026, wakati akizungumza katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Morogoro, akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kuwakumba wananchi endapo mvua hizo zitakuwa kubwa.
Amesema maandalizi hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Niño.
Mkuu huyo wa Wilaya amezitaka kamati za maafa katika ngazi mbalimbali kuhakikisha maeneo yote yanayoweza kuwa hatarishi yanabainishwa mapema na wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuhamishwa kwa wakati, kabla ya mvua kubwa kuanza.Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mifumo ya maji, mitaro na njia za kupitisha maji ya mvua inakuwa katika hali nzuri ili kuwezesha maji kupita kwa usalama na hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko.
Kilakala pia amezitaka mamlaka husika kuimarisha utoaji wa elimu na tahadhari kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na athari za mvua kubwa na mafuriko, huku akisisitiza matumizi ya vyombo vya habari katika kuwafikishia wananchi taarifa za tahadhari kwa wakati.
Vilevile, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya kukabiliana na maafa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nyumba na miundombinu mingine inajengwa kwa kuzingatia usalama na uwezo wa kukabiliana na athari za mafuriko.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kilakala amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya milipuko ya magonjwa inayoweza kusababishwa na matumizi ya maji machafu na mazingira yasiyo salama baada ya mvua kubwa na mafuriko.
Amesisitiza pia umuhimu wa familia kujiandaa kwa dharura kwa kuhifadhi chakula na mahitaji muhimu yatakayoweza kusaidia kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Mwanza, Pwani na Morogoro inahitaji kuimarisha maandalizi na kuchukua tahadhari mapema kutokana na jiografia na uwezekano wa maeneo hayo kuathiriwa na mvua kubwa na mafuriko.
Hatua hizo zinatarajiwa kusaidia kuimarisha utayari wa mamlaka na jamii, kupunguza madhara kwa maisha na mali za wananchi, pamoja na kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kutolewa wakati wa dharura.

No comments:
Post a Comment