Breaking News

Sep 3, 2026

SENDIGA AWATAKA WATUMISHI MOROGORO KUSIMAMIA MAJUKUMU, KUSUKUMA MAENDELEO

SENDIGA AWATAKA WATUMISHI MOROGORO KUSIMAMIA MAJUKUMU, KUSUKUMA MAENDELEO

Na.Mwandishi wetu

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, amewataka watumishi wa umma mkoani humo kusimamia kwa uadilifu na uwajibikaji majukumu yao, ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi na miradi ya maendeleo zinafanyika kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi.

Mhe. Sendiga ametoa wito huo Septemba 3, 2026, wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Mhe. Malima kwa sasa amehamishiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, huku Mhe. Sendiga akichukua jukumu la kuongoza Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sendiga alisema Mkoa wa Morogoro una wilaya saba na halmashauri tisa, huku ukiwa na fursa na shughuli mbalimbali za kiuchumi, zikiwemo kilimo, biashara, utalii, madini pamoja na utekelezaji wa miradi ya miundombinu, hususan barabara.

Alisema mafanikio ya sekta hizo yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya viongozi, watumishi wa umma na wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


"Kila mtumishi asimame kwenye majukumu yake,” alisema Mhe. Sendiga.

Katika hatua nyingine, Sendiga ameahidi kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vitendo, hususan katika utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo, kwa lengo la kuhakikisha wananchi na Taifa kwa ujumla wananufaika.

Aidha, amewaagiza Wakuu wa Wilaya mkoani Morogoro kuhakikisha suala la usafi wa mazingira linasimamiwa kwa umakini kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, mitaa, kata, tarafa hadi wilaya.

Amesema usafi wa mazingira ni miongoni mwa hatua muhimu za kujikinga na kudhibiti magonjwa ya mlipuko, ikiwemo kipindupindu.

Sendiga pia ameahidi kuendeleza kasi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo zilizokuwa zimeanzishwa na mtangulizi wake, Mhe. Malima, akisisitiza kuwa dhamira yake ni kuhakikisha “kazi inaendelea” kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro.

Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, Mkuu huyo wa Mkoa amesema bado kuna changamoto katika baadhi ya maeneo, huku akibainisha kuwa baadhi ya migogoro hiyo inachangiwa na viongozi wasioweka mbele maslahi ya wananchi.

Amesema uongozi wake utaweka mkazo katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa migogoro hiyo kwa kushirikisha wadau mbalimbali, ili kuhakikisha amani, usalama na shughuli za uzalishaji zinaendelea bila vikwazo.

Sendiga aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Agosti 27, 2026.Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.

No comments:

Post a Comment