Breaking News

Aug 10, 2026

KILOSA YATOA SH. BILIONI 1.6 KWA WANAWAKE, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU

KILOSA YATOA SH. BILIONI 1.6 KWA WANAWAKE, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU

Na Thadei Hafigwa

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro imetoa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 1.6 kwa vikundi 127 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mwaka wa fedha 2025/2026, hatua inayolenga kuongeza ajira, kukuza ujasiriamali na kuinua kipato cha wananchi.

Mikopo hiyo imetolewa kupitia mpango wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mpango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Beatrice Mwinuka, amesema mikopo hiyo imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuwawezesha wananchi kujiajiri na kuendesha shughuli mbalimbali za uzalishaji na biashara.

Amesema mpango huo pia unalenga kuboresha ustawi wa makundi hayo kwa kuwawezesha kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi, hivyo kuongeza kipato cha kaya na kuchangia maendeleo ya jamii.

Mwinuka ameeleza hayo wakati wa shughuli za ufuatiliaji wa vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo katika kata za Dumila na Magole, ambapo viongozi walipata fursa ya kuona namna wanufaika wanavyotumia fedha walizokopeshwa.

Katika ziara hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko, amesisitiza umuhimu wa wananchi kulinda amani na utulivu, akieleza kuwa mazingira salama ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Sekiboko amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa kuwekeza katika shughuli zenye tija, huku wakizingatia mshikamano na ushirikiano katika jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Serikali, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha wananchi kupata mitaji kupitia mpango huo.

Wamesema mikopo hiyo imewasaidia kupanua biashara, kununua vifaa vya uzalishaji na kuongeza kipato cha familia, huku wakieleza kuwa fursa hiyo imewapa uwezo wa kujitegemea na kuboresha maisha yao.

Aidha, wanufaika hao wameviomba vikundi vingine vinavyopata mikopo kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, pamoja na kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa wakati ili kuwawezesha wanachama wengine kunufaika na fursa hiyo.

Utekelezaji wa mpango wa asilimia 10 ya mapato ya ndani unaendelea kuwa miongoni mwa hatua zinazolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kujenga msingi wa maendeleo endelevu katika halmashauri.

No comments:

Post a Comment