PROF. KABUDI AITAKA NSSF KUWAFIKIA WANANCHI SEKTA ISIYO RASMI
Na Thadei Hafigwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Prof. Palamagamba Kabudi, ameitaka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kushirikiana na viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wanaofanya shughuli katika sekta isiyo rasmi kujiunga na Hifadhi Skimu.
Prof. Kabudi amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuwawezesha wananchi hao kuwa na mfumo wa kujilinda kiuchumi na kuhakikisha wanakuwa na uhakika wa maisha yao ya sasa na baadaye kupitia hifadhi ya jamii.
Waziri huyo alitoa wito huo wakati wa kilele cha Maonesho ya 33 ya Nanenane 2026,Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, Manispaa ya Morogoro.Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima.
Amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inalenga kuhakikisha wananchi wengi zaidi, wakiwemo wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali katika sekta isiyo rasmi, wanapata fursa ya kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii kupitia Hifadhi Scheme inayosimamiwa na NSSF.
Prof. Kabudi ameitaka NSSF kuongeza nguvu katika kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo wanakofanyia shughuli zao za kiuchumi, badala ya kusubiri wananchi wafike katika ofisi za mfuko huo.
“NSSF shirikiana na viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri tuhakikishe tunakwenda kuwafuata wananchi mahali walipo katika maeneo yao ya uzalishaji, maeneo yao ya masoko, maeneo yao ya shughuli mbalimbali ili kuhakikisha Watanzania wengi ambao wapo katika sekta isiyo rasmi wanajiunga na Hifadhi Scheme,” amesema Prof. Kabudi.
Amesema sekta isiyo rasmi ina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa, hivyo ni muhimu wananchi wanaojishughulisha na shughuli hizo kutambua umuhimu wa kuwa na mfumo wa hifadhi ya jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kulenge.Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha na kupata mafao yanayostahili kwa mujibu wa masharti ya skimu.
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amepongeza Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu akisema yameendelea kuwa jukwaa muhimu la wananchi, wakulima, wafugaji, wavuvi, wataalamu na wadau mbalimbali kuonesha teknolojia na ubunifu unaoweza kuongeza tija katika uzalishaji.
Amesema ongezeko la teknolojia zinazoibukia katika maonesho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi wenye tija, ushindani na unaotumia maarifa na teknolojia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amesema Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu yameonesha ongezeko la teknolojia na ubunifu unaolenga kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji.
Amesema teknolojia hizo zinatoa fursa kwa wananchi kujifunza mbinu bora za uzalishaji katika sekta mbalimbali, hususan kilimo, mifugo na uvuvi.
Malima amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa zinazotokana na maonesho hayo kwa kujifunza teknolojia zinazofaa, kuzitumia katika shughuli zao za uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.Mkuu wa Mkoa wa Twanga,Dkt.Matrida Buriani
Maonesho ya Nanenane yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta mbalimbali za uzalishaji, kutoa elimu na kuonesha teknolojia, bidhaa na huduma zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza tija katika uchumi.




No comments:
Post a Comment