Breaking News

Aug 14, 2026

GAIRO WAFUNGUA MNADA WA ZAO LA TUMBAKU


MNADA WA KWANZA WA TUMBAKU GAIRO WAFUNGUA SOKO LA TANI 117

Na Mwandishi wetu

Katibu Tawala wa Wilaya ya Gairo, Jeremia Mapogo, amezindua rasmi mnada wa kwanza wa zao la tumbaku kwa msimu wa 2025/2026, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za soko na kipato kwa wakulima wa wilaya hiyo.

Uzinduzi huo uliofanyika hivi karibuni umefungua umefungua rasmi mchakato wa uuzaji wa tumbaku kwa msimu huu, huku zaidi ya tani 117 za tumbaku zikiwa zimewasilishwa kwa ajili ya kuuzwa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa wakati wa uzinduzi huo, mauzo ya tumbaku hiyo yanatarajiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 600, fedha ambazo zitakwenda kuongeza kipato cha wakulima na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi katika maeneo yanayolima zao hilo.


Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Gairo inatarajiwa kukusanya zaidi ya Sh milioni 18 kutokana na ushuru unaotokana na zao hilo, hivyo kuongeza uwezo wa Halmashauri katika kutekeleza shughuli za maendeleo kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mnada huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Gairo, Jeremia Mapogo, alisisitiza umuhimu wa zao hilo katika kukuza shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato cha wananchi, huku akieleza umuhimu wa wakulima kuendelea kuzingatia ubora na kuongeza uzalishaji.

Mnada huo pia unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuwawezesha wakulima kupata soko rasmi la mazao yao, jambo linaloweza kuongeza uhakika wa mapato na kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la tumbaku wilayani Gairo.


Tumbaku imeanza kuchukua nafasi muhimu katika kilimo cha biashara wilayani Gairo baada ya kuanzishwa kwa kilimo cha majaribio katika msimu wa 2024/2025.

Matokeo yaliyopatikana katika msimu huo yameendelea kuimarisha uamuzi wa kuitambua tumbaku kama moja ya mazao ya biashara yenye umuhimu kwa uchumi wa wilaya hiyo.

Kwa kuingia katika msimu wa 2025/2026, wadau wa kilimo wanatarajia zao hilo kuendelea kutoa fursa kwa wakulima kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora na kunufaika zaidi na soko la zao hilo.

Wakati huo huo, ongezeko la shughuli za kilimo na biashara ya tumbaku linatarajiwa kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi, ikiwamo usafirishaji, biashara na huduma mbalimbali zinazohusiana na mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Kwa wakulima wa Gairo, kuanzishwa kwa minada rasmi ya tumbaku kunaonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha kilimo cha kibiashara na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa kaya na maendeleo ya Wilaya ya Gairo kwa ujumla. 

No comments:

Post a Comment