Tanzania na Ujerumani Kuimarisha Ushirikiano wa Maendeleo, Waweka Mkazo Uchumi na Uwekezaji
Na Mwandishi wetu
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani zimeanza mazungumzo ya pande mbili kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, huku zikielekeza nguvu katika miradi yenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi na inayochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mazungumzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Fedha, Mtumba jijini Dodoma, yamejikita katika maeneo ya kimkakati yakiwemo maji na usafi wa mazingira, afya, nishati, matumizi endelevu ya rasilimali za asili, uhifadhi wa mazingira, upatikanaji wa haki, usimamizi wa fedha za umma na usawa wa kijinsia.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Elijah Mwandumbya, alisema mazungumzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Ujerumani wenye historia ya zaidi ya miongo sita.
Mwandumbya alisema ushirikiano huo ulianza katika miaka ya 1960 na kuendelea kuimarishwa kupitia Mkataba wa Mfumo wa Ushirikiano uliosainiwa mwaka 1975, ulioweka misingi ya kuendeleza mahusiano ya maendeleo kati ya nchi hizo mbili.
“Ujerumani imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa Tanzania katika sekta mbalimbali, zikiwemo maji, mawasiliano, utalii, maendeleo ya watu na ustawi wa jamii,” alisema Mwandumbya.
Alisema mazungumzo hayo yanatoa fursa kwa wataalamu kutoka pande zote mbili kutathmini mafanikio ya ushirikiano uliopo, kubaini changamoto na kuweka vipaumbele vya miradi na maeneo yatakayotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Kwa mujibu wa Mwandumbya, baada ya wataalamu kukamilisha majadiliano na kufikia makubaliano, Serikali hizo zinatarajiwa kuchukua hatua za kurasimisha makubaliano hayo, ikiwemo kusaini mkataba wa ushirikiano wa maendeleo.
Alisema mazungumzo hayo yanatarajiwa kuendelezwa mwezi Novemba mwaka 2026, hatua ambayo inalenga kuhakikisha vipaumbele vilivyokubaliwa vinaendelea kufanyiwa kazi hadi kufikia makubaliano ya utekelezaji.
Tanzania yaweka Dira 2050 mbele
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, alisema Tanzania iko tayari kuimarisha na kuhuisha ushirikiano wake wa muda mrefu na Ujerumani ili kuendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Alisema Dira hiyo inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati cha juu, mseto, himilivu na jumuishi, huku ikihakikisha wananchi wanapata maisha bora na ustawi wa hali ya juu.
“Tanzania imejiwekea lengo la kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 na kuongeza pato la Taifa kwa mtu mmoja hadi takribani dola 7,000, kutoka uchumi wa sasa unaokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 90,” alisema Dkt. Kida.
Alisema Tanzania pia inalenga kupunguza kwa kiasi kikubwa umaskini, kuondokana na umaskini uliokithiri na kukabiliana na umaskini wa chakula, sambamba na kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa uendelevu na mazingira yanalindwa.
Dkt. Kida alisema ushirikiano na Ujerumani unaweza kuwa sehemu muhimu ya kufanikisha malengo hayo kupitia uwekezaji, uendelezaji wa sekta za uzalishaji, uimarishaji wa huduma za jamii na matumizi bora ya rasilimali.
Ujerumani yasisitiza uwekezaji na sekta binafsi
Naye Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati katika Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani, Joachim Schmitt, alisema Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku ikilenga kujenga ushirikiano wa kimkakati unaoendana na vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania.
Schmitt alisema mkakati mpya wa ushirikiano utaelekezwa katika maeneo yenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kupunguza umaskini pamoja na ukosefu wa usawa.
Alisisitiza pia umuhimu wa kulinda utawala wa sheria, nafasi ya asasi za kiraia, amani na usalama katika kuhakikisha mazingira ya maendeleo yanakuwa endelevu.
Kwa mujibu wa Schmitt, Ujerumani inalenga kuona ushirikiano huo ukijikita zaidi katika miradi mikubwa na yenye mwelekeo wa kimkakati, badala ya kutegemea miradi midogo isiyounganishwa katika mpango mpana wa maendeleo.
Aidha, alisema Ujerumani imeweka msisitizo maalumu katika ushirikiano wa kiuchumi, maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji, ikiwemo kuongeza ushiriki wa kampuni za Ujerumani na Tanzania katika miradi yenye tija kwa uchumi na wananchi.
Wawakilishi wa pande zote washiriki
Mkutano huo umewakutanisha wawakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka wizara na taasisi mbalimbali, wakiwemo Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa upande wa Ujerumani, ujumbe huo umehusisha Serikali ya Shirikisho la Ujerumani pamoja na taasisi zake za ushirikiano wa maendeleo, zikiwemo KfW na GIZ.
Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuweka msingi wa awamu mpya ya ushirikiano wa Tanzania na Ujerumani, kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania na kuongeza fursa za uwekezaji, ajira na ukuaji wa uchumi wenye manufaa kwa wananchi.




No comments:
Post a Comment