Breaking News

Aug 9, 2026

SERIKALI YAWEKA MKAKATI WA FEDHA, MIUNDOMBINU KUCHOCHEA UCHUMI NYANDA ZA JUU KUSINI

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb)

 SERIKALI YAWEKA MKAKATI WA FEDHA, MIUNDOMBINU KUCHOCHEA UCHUMI NYANDA ZA JUU KUSINI

Na Mwandishi wetu

SERIKALI imeweka mkakati wa kuhakikisha upatikanaji wa fedha za miradi ya miundombinu unakuwa wa uhakika, hatua inayolenga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya barabara na miundombinu mingine muhimu kwa ajili ya kuchochea shughuli za uzalishaji na ukuaji wa uchumi nchini.

Mkakati huo unalenga zaidi kuimarisha miundombinu katika maeneo ya uzalishaji, hususan Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ambayo ni miongoni mwa maeneo muhimu kwa uzalishaji wa chai na mazao mbalimbali ya kilimo.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), aliyasema hayo alipofika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati wa kuhitimisha sherehe za Maadhimisho ya Nane-Nane yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo zinapatikana kwa wakati ili kuondoa changamoto ya kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi, hasa ya barabara na miundombinu mingine inayochochea shughuli za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kwa muda mrefu utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo ulikuwa ukikabiliwa na changamoto ya ucheleweshaji wa fedha, hali iliyosababisha miradi kadhaa kusuasua.

Hata hivyo, alisema Serikali imefanya mageuzi ya kimfumo kwa kuweka utaratibu wa kuhakikisha asilimia 70 ya mapato yanayokusanywa kupitia mifuko maalum yanaelekezwa moja kwa moja kwenye mifuko hiyo badala ya kupitia Hazina.

“Katika mwezi wa Julai pekee, jumla ya shilingi bilioni 324 zilitolewa kwa mifuko mbalimbali ya maendeleo, ambapo shilingi bilioni 76 zilipelekwa moja kwa moja kwenye Mfuko wa Barabara. Utaratibu huu utaendelea kwa mwaka mzima wa fedha ili kuhakikisha miradi ya miundombinu haikwamishwi na uhaba wa fedha,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Balozi Omar alisema Serikali pia inaendelea kushirikiana na sekta ya fedha kutafuta njia mbadala za kupata fedha nyingi kwa wakati kwa ajili ya kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu.

Alisema miongoni mwa njia zinazotazamwa ni matumizi ya hati fungani za miundombinu (infrastructure bonds), ambazo zinaweza kusaidia kupata fedha za miradi mikubwa mapema badala ya kusubiri mapato ya ndani kukusanywa hatua kwa hatua.

Kwa mujibu wake, hatua hiyo itasaidia Serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi yenye umuhimu mkubwa kwa uchumi na wananchi.

Akizungumzia umuhimu wa miundombinu, Balozi Omar alisema barabara ni kiungo muhimu kati ya maeneo ya uzalishaji, masoko na viwanda, hivyo uwekezaji katika sekta hiyo una nafasi kubwa katika kuongeza tija na kipato cha wananchi.

Alisema hali hiyo ni muhimu zaidi katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ambako kilimo cha chai na mazao mengine kinafanyika kwa kiwango kikubwa.

“Maeneo haya ya Nyanda za Juu Kusini, ambako zao la chai na mazao mengine ya kilimo huzalishwa kwa wingi, miundombinu bora ya barabara itasaidia kuongeza tija kwa wakulima na kuchochea ukuaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao hayo,” alisema.

Aliongeza kuwa miundombinu bora itarahisisha usafirishaji wa mazao, kupunguza gharama za usafirishaji na upotevu wa bidhaa, pamoja na kufungua fursa za masoko mapya kwa wakulima na wazalishaji.

“Hii ndiyo njia ya kuongeza kipato cha wakulima na kukuza uchumi wa nchi,” alisema.

Balozi Omar pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa miradi ya miundombinu ili kuhakikisha wakandarasi wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mikataba waliyoingia na Serikali.

Alisema wakandarasi watakaobainika kuchelewesha utekelezaji wa miradi bila sababu za msingi watachukuliwa hatua kali, ikiwemo kuwekwa kwenye orodha ya kutopatiwa zabuni nyingine za Serikali.

Alisisitiza kuwa suala la miundombinu si ajenda ya kisiasa pekee, bali ni sehemu ya kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi katika maisha na shughuli zao za kiuchumi.

Alisema hali mbaya ya barabara katika baadhi ya maeneo imekuwa kikwazo kwa shughuli za uzalishaji, usafirishaji wa bidhaa na upatikanaji wa masoko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, alisema Mkoa huo unatambua na kuthamini jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu, hususan barabara.

Alisema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 9 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya njia nne inayounganisha Igawa–Uyole–Songwe–Tunduma, akieleza kuwa mradi huo ni hatua muhimu katika kuboresha usafiri na usafirishaji katika Mkoa wa Mbeya.

Kwa mujibu wa Mhe. Malisa, ujenzi huo utasaidia kupunguza msongamano wa magari, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji.

“Mradi huu utarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, kupunguza msongamano wa magari na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi na wawekezaji,” alisema.

Malisa alisema pamoja na maboresho ya barabara, Serikali inaendelea kuwekeza katika huduma nyingine muhimu, ikiwemo umeme na maji, ili kuweka mazingira bora kwa shughuli za uzalishaji na uwekezaji.

Alisema TANESCO tayari imetoa ratiba ya kupeleka umeme katika maeneo yaliyokuwa na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo.

Alibainisha kuwa upatikanaji wa umeme katika maeneo ya uzalishaji, ikiwemo migodi inayozalisha hadi kilo 400 za dhahabu kwa mwezi, utasaidia kuongeza tija na thamani ya uzalishaji.

Alisema maboresho ya huduma za maji, umeme na miundombinu mingine yataendelea kuwa msingi muhimu wa kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Mbeya.

Kwa ujumla, Serikali imeeleza kuwa uwekezaji katika miundombinu utaendelea kupewa kipaumbele kama nyenzo muhimu ya kuunganisha wazalishaji na masoko, kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji, kuongeza thamani ya mazao na hatimaye kuongeza kipato cha wananchi pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

 

No comments:

Post a Comment