Breaking News

Nov 28, 2020

SERIKALI YATAMBUA MCHANGO WASAIDIZI WA KISHERIA-RAS MOROGORO

Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emanuel Kalobelo,akisisitiza jambo wakati akifungua Kongamano la Wasaidizi wa Kisheria Mkoa wa Morogoro,kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi wa MPLC,Henry Mgingi.Kulia kwake ni Mkurugenzi wa MPLC,Flora Masoi.
Na Thadei Hafigwa

HALMASHAURI za Wilaya Mkoa wa Morogoro zimetakiwa kushirikiana na vituo vya wasaidizi wa kisheria katika maeneo yao ikiwa ni mkakati wa kupunguza changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi katika ngazi cha chini katika masuala ya kisheria.

Wito huo umetolewa na Katibu tawala Mkoa wa Morogoro,Mhandisi Emanuel Kalobelo wakati akifungua kongamano la wasaidizi wa kisheria mkoa wa Morogoro lililoandaliwa na Kituo cha Msaada wa sheria Morogoro (Morogoro Paralegal centre) Novemba 28,mwaka huu.

Mhandisi Kalobelo alisema kuwa serikali mkoa wa Morogoro inatambua mchango wa wasaidizi wa serikali kwa kuwa wanasaidia wananchi katika ngazi za chini katika ngazi ya vijiji,kata hadi wilaya ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakihitaji msaada wa kisheria na kulazimika wakikimbilia ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupata ufumbuzi na  msaada wa kukabiliana  na changamoto zinazowakabili.

“Mimi na Mkuu wa Mkoa toka tulipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kuongoza Mkoa wa Morogoro tulipoanza kazi tu tulikuta foleni kubwa ya wananchi wakihitaji msaada wa kisheria ikiwemo masuala ya ndoa lakini pamoja na mambo mengine watu wa msaada wa sheria wanasaidia sana.”Alisema Mhandisi Kalobelo.

Aidha,Mhandisi Kalobelo ameshauri uongozi wa Morogoro Paralegal kuandaa taarifa ya mafanikio na mahitaji walio nayo na kuwawasilisha katika vikao vya ushauri wa Mkoa(RCC) na ngazi ya Wilaya (DCC) ili kuangalia namna ya kuweza kusaidia.

Hata hivyo,Mhandisi Kalobelo amewasa wasaidizi wa kisheria kutotumia nafasi ya uwelewa wao katika masuala mbalimbali ya kisheria kwa kufanya matukio yenye viashiria vya udanganyifu kwa wananchi kwa masilahi binafsi,hali hiyo iwapo ikisitokeza kamwe ofisi yake haitawafumbia macho watu wa aina hiyo.

Awali,Mkurugenzi wa Morogoro Paralegal Centre(MPCL),Frola Masoi,alielezea malengo ya Kongamano hilo ni kubadilishana uzoefu kwa wadau wa kisheria,kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi wa miaka minne katika msaada wa kisheria,mafanikio changamoto na uendelevu wa utoaji wa huduma za msaada za kisheria katika harakati za kupinga ukatili wa jinsia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya MPLC,Henry Kigingi alishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuonesha utayari wake katika kushirikiana na Watu wasaidizi wa kisheria na kufanikiwa kutatua changamoto za migogoro ya ardhi,ndoa na Mirathi pamoja na ukatili wa jinsia.

Kigingi alisema katika utekelezaji wa majukumu yao wamebaini ya kuwa kuna baadhi ya watendaji wa serikali katika ngazi ya vijiji wamekuwa hawana uelewa wa kutosha katika utendaji wao wa kazi,hivyo ameshauri serikali ya mkoa kuwajengea uwezo wa mara kwa mara juu ya masuala ya uongozi ili kuondoa urasimu usiyo wa lazima katika kuwahudumia wananchi.

Risala ya wana kongamano kwa mgeni rasmi iliyosomwa na Germana Peter kutoka Kituo cha msaada wa sheria Morogoro vijijini wamebainisha ya kuwa katika kipindi cha miaka nne wameweka kushughulikiwa kesi 19,396 na kuwafikiwa watu 285,000 kwa kuwapa semina,kongamano,mafunzo na elimu kwa njia ya redio.

1 comment: