Breaking News

Nov 26, 2020

MBUNGE TALETALE KUCHIMBA VISIMA 14 KWA WANANCHI WAKE

Mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Teletale
 Na Severin Blasio, Morogoro

OFISI ya mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kwa kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu, wanatarajia kuchimba visima vya maji 14 katika kata tatu za Ngerengere, Mkulazi na Gwata Halmashauri ya wilaya ya Morogoro.


Visima hivyo vikikamilika vitawasaidia wananachi hususani wanawake wa Kata hizo kumaliza changamoto ya kutembea umbali mrefu kusaka maji.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maeneo yatakayochimbwa visima hivyo, mbunge wa jimbo hilo, Hamis Teletale alisema kuwa Kata hizo kwa muda mrefu zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya maji, ambapo wananchi wanatumia muda  mwingi wa uzalishaji mali kutafuta maji.

Alisema hatua hiyo ni kumuunga mkono dhamira ya rais Dkt John Magufuli ya kutaka kuwatua ndoo wakina mama ambao wanatumia muda mwingi kutafuta maji safi hali inayowapelekea baadhi yao kuingia katika migogoro kwenye ndoa zao.

“Dhamira kubwa ni kuwaondolea kero ya maji wananchi hasa huku pembezoni mwa mkoa ambako wanapata maji kwa shida na hata wanayoyapata ni maji chumvi, kwahiyo utumuwaleta hawa wataalam ili watupe ushauri wa maeneo sahihi ya kuchimba visima” Alisema Taletale

Alifafanua kuwa Kata ya Ngerengere watapata visima 8, Mkulazi 2 na Kata ya Gwata visima 5, ambapo katika muda mfupi visima hivyo vitachimbwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Mtaalam wa maji chini ya ardhi, bonde la Wami Ruvu, Abdusalum Nana alisema ofisi ya bonde imejiandaa kuchimba visima virefu vitakavyowezesha kutoa maji baridi.

Nana alisema wanatambua changamoto hiyo ya maji imekuwa ni kero ya muda mrefu katika kata hizo na kuwatoa hofu wananchi kuwa mara baada ya kubainisha maeneo ya kuchimba visima zoezi hulo linatekwenda haraka ili huduma iweze kupatikana.

Naye, Diwani wa Kata ya Ngerengere, Kibena Kingu alisema kuwa ujio wa wataalamu hao pamoja na mbunge umeleta faraja kwa wananchi kwamba kero hiyo itakuwa historia kwao kwa kuwatua wanawake ndoo.

 

No comments:

Post a Comment