MKUU WA MKOA WA PWANI,MHANDISI EVARISTI NDIKILO AKITOA MSISITIZO WA UWAJIBIKAJI KWA WALIMU WA SEKONDARI MKOA WA PWANI
RC PWANI ACHUKIZWA NA WALIMU WA SEKONDARI WASIOWAJIBIKA
NA VICTOR MASANGU, PWANI
MKUU wa
Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amewaagiza wakuu wote wa shule za
sekondari kubadilika na kuhakikisha wanaweka mipango madhubuti ambayo
itaweza kuongeza kasi ya ufundishaji ili kuboresha sekta ya elimu
na kusaidia kasi ya kiwango cha ufaulu iweze kuongezeka hasa katika
shule za serikali
Pia, Mkuu huyo wa Mkoa ameonesha kuchukizwa na tabia ya baadhi
ya walimu kutotekeleza majukumu yao ya kazi hali ambayo ina viashiria vya
uzembe na kushusha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Ndikilo ametoa kauli hiyo wakati wa kufungua kikao kazi ambacho
kimewakutanisha wakuu wa shule za sekondari za serikali wapatao 85 kutoka Wilaya
zote za Mkoa wa Pwani kwa lengo la kujadili mikakati madhubuti ambayo
itasaidia kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi na kuwataka
wakuu wote wa shule kulivalia njuga suala hilo na kuwachukulia hatua kali
walimu ambao ni wazembe.
Aliongeza kwamba lengo la serikali ya Mkoa wa Pwani ni
kuhakikisha kwamba inaweka mipango madhubuti kwa ajili ya kuongeza kasi zaidi
kwa wanafunzi wanaosoma katika shule mbalimbali za serikali hivyo walimu wote
wanapaswa kuongeza juhudi zaidi katika kutilia mkazo suala zima la kuwafundisha
wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
“Mimi kama Mkuu wa Mkoa wa Pwani huwa nashangaa sana kuona
katika shule zingine zinafanya vizuri na zingine zinafanya vibaya kwa hivyo rai
yangu na maagizo kwa wakuu wote wa shule za sekondari ambazo ni za serikali
lazima sasa mhakikishe mnawafuatilia kwa ukaribu walimu wote ambao ni wazembe
katika ufundishaji maana haiwezekani mwalimu anapokea mshahara lakini katika
kuwafundisha wanafunzi hafanyi hivyo hii sio sahihi hata kidogo,”alisema
Ndikilo.
Aidha, Ndaikilo aliongeza kuwa ili wanafunzi wa shule za
serikali waweze kufanya vizuri katika mitihani yao mbalimbali ya Taifa
inatakiwa kuwe na ushirikiano wa karibu baina na walimu wakuu pamoja na
walimu wa kawaida katika suala zima la kuweza kuwaandaa mapema wanafunzi ili
wanapoingia katika mitihani yao wanakuwa wameshajiweka katika maandalizi
mazuri.
Katika hatua nyingine Ndikilo aliwapongeza walimu wakuu hao wa
shule za sekondari za serikali kwa kuweza kujitahidi kwa hali na mali kuongeza
kiwango cha ufaulu mwaka hadi mwaka na kuwataka waendelee na moyo wa kuongeza juhudi na maarifa ili Mkoa wa
Pwani uweze kuingia katika tano bora katika ngazi ya Taifa.
Kwa upande wale Afisa elimu wa Mkoa wa Pwani, Khadija Mcheka amesema kwamba licha ya kiwango cha elimu ya sekondari kuongezeka kwa asilimia 85.8 ukiringanisha na miaka iliyopita lakini bado kuna changamoto katika sekta hiyo ikiwemo ya miundombinu ya majengo ya madarasa, pamoja na uhaba wa vitendea kazi ambavyo vinahitajika ili kuboresha sekta ya elimu.
KATIBU TAWALA MKOA WA PWANI DKT.DELPHINE MAGERE AKITOA UFAFANUZI UMUHIMU WA KIKAO KAZI ALICHOKIITISHA NA KUHUDHURIWA NA WALIMU WAKUU 85 WA SHULE ZA SEKONDARINaye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Dk. Delphine Magere ambaye
ndiye aliyeitisha kikao kazi hicho alibainisha kwamba dhumuni kubwa ni
kuwakutanisha wakuu wote wa shule hizo za sekondari za serikali ni kujadili changamoto zilizopo katika sekta ya
elimu ili kuzitafutia ufumbuzi na kuweka mbinu zitakazosaidia kuongeza
kiwango cha elimu.
Dk. Magere aliongeza kuwa
ana imani kikao kazi hicho kati ya walimu wakuu kitaweza kuleta chachu zaidi ya
kukuza kasi ya maendeleo katika sekta ya elimu na kwamba katika siku zijazo
wanatarajia wanafunzi wanaosoma katika shule mbalimbali za serikali wataweza
kufanya vizuri zaidi tofauti na miaka iliyopita.
“Hiki kikao nimekiandaa kwa lengo la kukutana na walimu wakuu wa
shule mbalimbali za serikjali na hapa wamekuja walimu wapatao 85 kwa hivyo ni
imani yangu tutaweza kufikia malengo ambayo tumejiwekea ya Mkoa wetu wa Pwani
kuingia katika nafasi ya tano bora kitaifa na hili sisi tunaliweza endapo
tukishikamana kwa sasa utaona ufaulu wetu kwa shule za sekondari umeongezea
hadi kufikia asilimia 85 na tutaendelea na kasi hii.”alisema Dk. Magere.
No comments:
Post a Comment