Thadei Hafigwa
WATANZANIA wametakiwa
kuacha vitendo vya ukatili wa kijinsia,ulawiti,ubakaji dhidi ya mtoto wa kike
kwani ni chukizo kwa Mungu hasa katika kipindi cha kusherekea sikukuu ya Krismas.
Msimamizi wa kitume Jimbo Katoliki la Morogoro,Padre
Lazarus Masimbe alitoa rai hiyo wakati akitoa salamu za sikukuu ya Krismas kwa
mwaka 2020 katika misa takatifu iliyofanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu
Patrick,ibada iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare.
Padre Msimbe alisema kuwa vitendo vya kikatili na
vya kinyama vilianza kushamiri katika vita ya kwanza na pili duniani ambapo
katika kipindi hicho watu wamekuwa wakifanya matukio ya kikatili na kumchukiza
Mwenyezi Mungu.
“Kitendo cha kuwafanyia ukatili watoto,utoaji wa
mimba ni chukizo kwa Mungu ni sawa na dhambi ya uaji,hivyo jamii tunapaswa
kubadilika kifikra ili kuzaliwa na Kristu Yesu upya” Aliasa.
Aidha,aliwataka kila mtanzania kwa nafasi yake
kuwalinda watoto kwa kile alichokieleza kwamba matukio ya ukatili wa jinsia
dhidi ya watoto unafanywa na ndugu wa karibu na wanafamilia.
Alisema kuwa sherehe ya Krismas haitakuwa na maana
yoyote iwapo vitendo vya kikatili kwa watoto vikiwa vinaendelea kushamiri
katika jamii za watanzania pia alishukuru viongozi wa serikali kwa jitihada
mbalimbali wanazozifanya dhidi ya matukio ya aina hiyo.
Hivi Karibuni, Papa Francisko, alimteua Padre Lazarus
Msimbe, kutoka Shirika la Kimisionari la Mungu Mwokozi (Salvatorian), Kuwa
Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Morogoro.

No comments:
Post a Comment