TAKUKURU YAZUIA UPOTEVU WA FEDHA ZA UMMA, YAIBUA MAPUNGUFU KWENYE MRADI WA VYOO SHULE YA SEKONDARI KISAKI
Na Thadei Hafigwa
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imefanikiwa kubaini na kusaidia kurekebisha mapungufu ya kiufundi katika mradi wa ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Kisaki, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, hatua inayolenga kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na miradi inatekelezwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha (Value for Money).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Casius Kiaro, alisema mradi huo unaotekelezwa kwa mfumo wa Force Account ulipokea kiasi cha shilingi milioni 25 kutoka Serikali Kuu katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya ujenzi wa matundu hayo ya vyoo.
Kiaro alisema katika ufuatiliaji uliofanywa na TAKUKURU katika eneo la mradi, taasisi hiyo ilibaini kutokuzingatiwa kwa vipimo vya upana wa vyumba vya vyoo vilivyoanza kujengwa, ambapo kwa mujibu wa michoro ya mradi vilipaswa kuwa na upana wa milimita 2,275, lakini ujenzi ulikuwa umeanza kwa upana wa milimita 2,050.
Alisema baada ya kubaini kasoro hiyo, TAKUKURU ilitoa ushauri kwa wasimamizi wa mradi kuhakikisha marekebisho yanafanyika kwa kuzingatia michoro na viwango vilivyokubalika.
Alifafanua kuwa ushauri huo ulizingatiwa na marekebisho yalifanyika, hali iliyowezesha ujenzi kuendelea kwa kufuata vipimo vilivyoainishwa katika michoro ya mradi.
Kwa mujibu wa Kiaro, hatua hiyo imechangia kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma, huku ikihakikisha mradi unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na thamani halisi ya fedha zilizotengwa.
Aidha, alisema katika kipindi cha miezi sita, TAKUKURU Mkoa wa Morogoro ilifanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo na kusaidia kuhakikisha miradi mitano yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.099, ambayo ilikuwa na mapungufu katika utekelezaji wake, inatekelezwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha zilizotolewa.
Alisema TAKUKURU ilitoa ushauri kwa wasimamizi wa miradi hiyo kutokana na mapungufu yaliyobainika, na ushauri huo ulizingatiwa, hali iliyowezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha zilizotengwa.
Vilevile, Kiaro alisema taasisi hiyo ilifuatilia matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 17.2 yaliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 29 ya maendeleo katika sekta mbalimbali, zikiwemo elimu, maji, afya, kilimo, usafirishaji, miundombinu na biashara.
Alisema kwa ujumla, ufuatiliaji huo umechangia kuimarisha usimamizi na matumizi sahihi ya fedha za umma, kuongeza uwajibikaji kwa wasimamizi wa miradi na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa, viwango vya ubora na thamani halisi ya fedha zilizotengwa.

No comments:
Post a Comment