Na Mwandishi Wetu, Miono
SHULE ya Msingi Msufini, iliyopo katika Kijiji cha Miono, Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, imepokea msaada wa mashine ya kudurufu (photocopy) na mashine ya kuchapisha nyaraka (printer) vyenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 2.6 kutoka kwa Amara Executive Lodge.
Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kurudisha hisani kwa jamii na kuchangia katika kuboresha huduma za kijamii, hususan sekta ya elimu.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Amara Executive Lodge, Karim Rutwengwe, amesema uamuzi wa kutoa msaada huo umetokana na changamoto zilizobainishwa na uongozi wa shule wakati wa mahafali ya wanafunzi wa darasa la saba yaliyofanyika Oktoba 9 mwaka huu.
Amesema miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa wakati huo ni ukosefu wa mashine za kudurufu na kuchapisha nyaraka, hali iliyokuwa ikiathiri baadhi ya shughuli za kitaaluma shuleni hapo.
"Leo tumekabidhi mashine mbili, moja ya kudurufu makaratasi na nyingine ya kuchapisha, ambazo kwa pamoja zina thamani ya shilingi milioni 2.6. Msaada huu ni sehemu ya kurudisha hisani kwa jamii katika nyanja mbalimbali za afya, elimu na maendeleo ya jamii, kwa sababu tunaamini ni jukumu letu kushiriki katika kuleta maendeleo," amesema Rutwengwe.
Ameeleza kuwa Amara Executive Lodge ina mkakati wa kuendelea kushirikiana na wananchi wa Chalinze katika kutambua na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii.
Amesisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kutoa misaada ya kijamii inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha wanafunzi wanapata mahitaji muhimu yatakayowawezesha kusoma katika mazingira bora.
"Ni mkakati wetu kuhakikisha watoto wanaosoma katika Halmashauri ya Chalinze wanapata mahitaji muhimu yanayowawezesha kujifunza vizuri. Tutaendelea kushirikiana na jamii na kutoa misaada mbalimbali ya kiutu na kijamii kwa lengo la kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu," ameongeza.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msufini, Bless Kanuti, ameishukuru Amara Executive Lodge kwa msaada huo, akieleza kuwa vifaa hivyo vitapunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili walimu wakati wa kuandaa na kuchapisha mitihani pamoja na nyaraka nyingine za shule.
Amesema awali shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na ugumu wa kudurufu na kuchapisha mitihani, hali iliyowalazimu kutafuta huduma hizo nje ya shule.
"Awali tulikuwa tunapata changamoto ya kuchapisha na kudurufu mitihani, lakini msaada huu ni mkubwa kwetu kwa sababu sasa tumepata vitendea kazi muhimu vitakavyotuwezesha kufanya shughuli hizo ndani ya shule," amesema Kanuti.
Aidha, ameeleza kuwa uongozi wa shule utaendelea kuweka mikakati ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na kufanya vizuri katika mitihani yao.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa vifaa hivyo ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na kurahisisha maandalizi ya nyaraka mbalimbali za kitaaluma.
No comments:
Post a Comment