TAKUKURU MOROGORO YAOKOA MIRADI 5 YENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 1.099
Na Thadei Hafigwa
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imesaidia kuboresha utekelezaji wa miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.099, baada ya kubaini mapungufu yaliyokuwa yakisababisha miradi hiyo kutotekelezwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha zilizotengwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha miezi sita, Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Casius Kiaro, alisema taasisi hiyo ilitoa ushauri kwa wahusika wa miradi hiyo baada ya kubaini kasoro mbalimbali kupitia ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma.
Alisema ushauri uliotolewa ulizingatiwa na kusababisha miradi hiyo kukamilika kwa kuzingatia thamani ya fedha zilizotengwa pamoja na muda uliopangwa wa utekelezaji.
Kiaro alisema katika kipindi hicho, TAKUKURU pia ilifuatilia matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 17.2 yaliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 29 ya maendeleo katika sekta za elimu, maji, afya, kilimo, usafirishaji, miundombinu na biashara.
Alibainisha kuwa kwa ujumla, ufuatiliaji huo umechangia kuimarisha usimamizi na matumizi sahihi ya fedha za umma, kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha zilizotengwa na malengo yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Kiaro alisema kupitia Programu ya TAKUKURU Rafiki, taasisi hiyo imefanikiwa kufikia kata 52 na kubaini kero 467 za wananchi, ambapo asilimia 77.3 zimekwisha kutatuliwa, huku asilimia 22.7 zikiendelea kushughulikiwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Kuhusu utoaji wa elimu kwa umma, alisema TAKUKURU imeendelea kuimarisha ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwafikia makundi mbalimbali, yakiwemo watumishi wa umma, wadau wa sekta binafsi, vijana na wazee.
Alisema juhudi hizo zinalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya rushwa, kukuza uwajibikaji na kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kupambana na vitendo vya rushwa.
Alitaja njia zilizotumika kutoa elimu hiyo kuwa ni kuendesha semina 198, mikutano ya hadhara 41, kuimarisha klabu zilizopo na kuanzisha klabu 225, kutoa taarifa nne kupitia vyombo vya habari pamoja na kuendesha vipindi nane vya redio.
Katika eneo la uchunguzi wa malalamiko na mashauri ya rushwa, Kiaro alisema TAKUKURU Mkoa wa Morogoro ilipokea jumla ya malalamiko 201 katika kipindi hicho, ambapo 158 yalihusu tuhuma za vitendo vya rushwa na yanaendelea kufanyiwa uchunguzi katika hatua mbalimbali.
Alisema malalamiko mengine 43 hayakuhusu masuala ya rushwa, hivyo baadhi ya walalamikaji walipatiwa ushauri, huku mengine yakipelekwa katika idara na taasisi husika kwa ajili ya kushughulikiwa.
Kuhusu mwenendo wa mashauri mahakamani, Kiaro alisema katika kipindi hicho kulikuwa na mashauri mapya 11, mashauri 10 yalitolewa uamuzi na hakuna shauri lililoondolewa mahakamani, huku shauri moja likiwa bado linaendelea kusikilizwa.

No comments:
Post a Comment