TAKUKURU MOROGORO KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA, YAWATAKA WANANCHI KUTOA TAARIFA KUPITIA 113
Na Thadei Hafigwa
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro imeweka mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa katika kipindi cha miezi mitatu, kuanzia Oktoba hadi Desemba 2026, kwa kuendeleza ushirikiano na wananchi pamoja na wadau mbalimbali katika kubaini na kuziba mianya ya rushwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Casius Kiaro, alisema moja ya vipaumbele vya taasisi hiyo katika kipindi hicho ni kuimarisha ushiriki wa jamii katika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na viashiria vyake ili viweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.
Alisema TAKUKURU itaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vipindi vya redio na televisheni, semina pamoja na mikutano ya hadhara kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya rushwa, haki na wajibu wao, sambamba na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Kiaro alitaja mkakati mwingine kuwa ni kuendeleza utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU Rafiki kwa kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali, ili kubaini na kuondoa mianya ya rushwa katika mifumo ya utoaji huduma kwa umma.
Aidha, alisema taasisi hiyo itaendelea kufanya uchambuzi wa mifumo ya utoaji huduma za umma kwa lengo la kubaini mianya inayoweza kuchochea vitendo vya rushwa na kutoa ushauri kuhusu hatua stahiki za kuzuia na kudhibiti vitendo hivyo.
Aliongeza kuwa TAKUKURU itaendelea kuhamasisha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia njia rasmi zilizowekwa, ili kuwezesha malalamiko na taarifa hizo kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, Kiaro amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kulinda maadili na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa, akisisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kutoa taarifa mapema anapobaini au kupata taarifa za viashiria vya rushwa.
Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutoa taarifa hizo kwa siri na haraka kupitia namba 113, ambayo ni ya bure na haina malipo.
Alisema hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuzingatia kaulimbiu isemayo: “KUZUIA RUSHWA NI JUKUMU LAKO NA LANGU, TUTIMIZE WAJIBU WETU.”

No comments:
Post a Comment