Na Andrew Chimesela – Morogoro
Imeelezwa kuwa sekta ya Ustawi wa Jamii hapa nchini inayotekelezwa na Maafisa wa Ustawi wa Jamii chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto ni nyezo muhimu na chimbuko la kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa juu.
Hayo yamelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi
Emmanuel Kalobelo Agosti 27 mwaka huu wakati akifungua kikao cha wadau wanaotoa
huduma za Ukimwi na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Mkoani
Morogoro.
Katika kikao hicho kilichofanyika Ukumbi wa mikutano wa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na kujumuisha Maafisa wa Ustawi wa Jamii,
Mhandisi kalobelo amesema Tanzania inapojipanga kuelekea uchumi wa juu umuhimu
wa Maafisa hao unazidi kutambulika na kwamba maafisa hao hawawezi kujiondoa
kama sehemu ya kuipeleka nchi katika ustawi wa juu zaidi.
Amesema kwa sababu hiyo Maafisa Ustawi wa Jamii wajiamini na
kwamba hata hatua ya Tanzania ilipofikia sasa kwa sehemu kubwa wao wamechangia
kwa kuziwezesha familia na jamii kwa jumla kuishi kwa Amani na utulivu.
“na huenda hata tulipofikia katika uchumi wa kati pia nyie
mmekuwa wadau muhimu katika kutufikisha hapo” amesema Mhandisi Kalobelo.
Amesema sehemu yoyote yenye migogoro haiwezi kuwa na
maendeleo ya haraka, hivyo amewataka maafisa Ustwai wa Jamii kufanya kazi kwa
bidii katika kuleta utulivu ndani ya nchi ili jamii ipate fursa ya kufanya kazi
ya kujiletea maendeleo yao.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwashukuru wahisani wanaosaidia
masuala ya huduma za Ustawi wa Jamii hususan eneo la kuhudumia watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi.
Pamoja na kuwashukuru wahisani hao ambao wamewezesha
kutekelezwa kwa afua mbalimbali kwenye eneo la watoto katika ngazi ya jamii,
amewataka wahisani hao kufanya kazi zao kwa uaminifu ili kile kinachoombwa kwa
ajili ya kuwasaidia watoto kiwafikie ili watoto hao nao wafaidi rasilimali za
nchi yao.
Mwisho, amewataka wale wote wenye vituo vinavyojihusisha na
utoaji wa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, kusajili vituo
vyao ili pamoja na nia yao njema ya kusaidia watoto hao vituo hivyo vifuate
taratibu za nchi na kutambulika kisheria.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro Bi. Jesca
Kagunila alitaja lengo kuu la kikao hicho kuwa pamoja na kufahamiana mashirika
yote yanayojihusisha na kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi, kikao hicho kililenga kuboresha utendaji kazi na namna ya kutatua
changamoto za Matukio ya Ukatili kwa watoto ndani ya Mkoa wa Morogoro.
Aidha, Bi kagunila amesema kuanzia mwezi Januari hadi Juni
mwaka huu jumla ya matukio 2848 ya ukatili yariripotiwa, kati yake matukio 1561
walifanyiwa watu wazima na matukio ya ukatili 1287 walifanyiwa watoto.
Katika matukio yote hayo ukatili wa kihisia umeonekana
kuongoza kwa kuripotiwa matukio 1287 na kufuatiwa na ukatili wa kimwili matukio
699, ukatili wa kiuchumi matukio 551 na ukatili wa kingono matukio 111 huku
Halmashauri ya Mji wa Ifakara ikiongoza kwa kuripoti matukio ya ukatili 1873.
Akifunga kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa,
ambaye baada ya kufungua alipata dharura, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt.
Urio Kusirye ametaka kuimarisha ushirikiano kwa wadau wanaofanya kazi za
kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuagiza ngazi za
Wilaya nao kuitisha vikao kama hivyo.
Wadau mbalimbali akiwemo Christina Wirner wa kutoka kituo
cha Agape Chidren’s cha Kihonda Mkoani humo ameiomba Serikali kuendelea
kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaojihusisha na ukatili kwa
watoto hasa katika eneo la Ubakaji na kulawiti ili jamii igope kufanya matendo
kama hayo.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto – Polisi Mkoa wa Morogoro
Sophia Ngosso amesema changamoto kubwa wanayoipata jeshi la polisi katika suala
la ukatili kwa watoto ni jamii kutokuwa tayari kutoa ushahidi pindi wahusika
wanapohitajika.
Kwa sababu hiyo watuhumiwa huachiwa na ndipo dhana
iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa polisi inawaachia watuhumiwa huanzia. Kwa
sababu hiyo Sophia ameiomba Jamii pamoja na kuripoti matukio hayo jamii iwe
tayari kutoa ushirikiano katika kutoa ushahidi ili kuwatia hatiani watuhumiwa
na kukomesha matendo ya ukatili kwa watoto.
Wadau wa kikao hicho akiwemo Bi Ruth Mnale kutoka kituo cha
Day Care Centre amewatuhumu baadhi ya wazazi kutetea ukatili wa kingono
wanaofanyia watoto wao ambapo hudai kuwa watoto hao nao wanahitaji starehe kama
watu wazima.
Naye Peter Kimath kutoka kituo cha kutoa msaada wa kisheria
ameishukuru Serikali kwa kutoa ushirikiano kwao mara wanapokuwa wanahitaji
hususan jeshi la polisi.
No comments:
Post a Comment