Breaking News

Sep 27, 2020

WAKAZI WA PWANI WAPEWA RAI KUTUNZA MAZINGIRA

 

               Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Mhandisi Evarist Ndikilo 

“Kitu kikubwa ninachowaomba ni lazima tuhakikishe tunabadilika kwa kuweka misingi mizuri kuanzia ngazi za chini katika suala zima la utunzani wa mazingira na kuachana kabisa na vitendo vya ukataji wa miti ovyo pamoja na uchimbaji wa michanga hii ni hatari sana kwa hivyo mimi kama kiongozi wenu nina wasihi kuachana na hali hii na badala yake pandeni miti kwa wingi.”Mhandisi Evarist Ndikilo Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Mhandisi Evarist Ndikilo mkuu wa Mkoa wa Pwani amekemea vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyofanywa na baadhi ya wananchi kwa kukata miti hali inayopelekea uoto wa asili kutoweka na kusababisha baadhi ya maeneo kuwa majangwa.

Maadhimisho ya wiki ya matembezi ya Amani kwa ajili ya Juma la mazingira kidunia katika ngazi ya mkoa wa Pwani kwa mwaka 2020 yamefanyika katika shule ya St, John Bosco iliyopo Wilayani Kibaha ikiwa na kauli mbinu isemayo “Jubilee ya Dunia yenye mwenendo mpya na tumaini  jipya”.

Mhandisi Ndikilo, pia amekemea shughuli za kibinadamu za  uchimbaji holela wa michanga  pamoja na uvuvi haramu, Wakati wa kuadhimisha siku ya wiki ya matembezi ya amani yalioratibiwa na Kanisa Katoliki Parokia ya Tumbi  kwa ajili ya juma la mazingira kidunia ambayo  yamefanyika katika eneo la shule ya msingi ya St. John Bosco iliyopo Wilayani Kibaha na kuudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na viongozi wa dini.

Aidha, Ndikilo amesema kuwa uhifadhi wa mazingira ni suala la mtambuka hivyo ni muhimu kwa uhai wa viumbe pamoja na maendeleo ya uchumi wa nchi, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anawajibuka katika utunzaji wa mazingira.

“Kitu kikubwa ninachowaomba ni lazima tuhakikishe tunabadilika kwa kuweka misingi mizuri kuanzia ngazi za chini katika suala zima la utunzani wa mazingira na kuachana kabisa na vitendo vya ukataji wa miti ovyo pamoja na uchimbaji wa michanga hii ni hatari sana kwa hivyo mimi kama kiongozi wenu nina wasihi kuachana na hali hii na badala yake pandeni miti kwa wingi,”alisema Ndikilo.

Pia Ndikilo ametoa wito kwa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza mazingira kwa kuhakikisha kunakuwepo na mipango madhubuti kwa ajili ya kudhibiti vitendo vya uchomaji wa mkaa pamoja na uchimbaji holela wa mchanga ambao unaleta madhara makubwa katika kuharibu mazingira kutokana na wakati mwingine kuendesha shughuli mbali mbali za kibinadamu.

Katika hatua nyingine Ndikilo alielezea madhara ambayo yanatajwa na wataalamu wa mazingira ni pamoja na kupungua kwa maji safi, kuongezeka kwa magonjwa ya wanyama pamoja na mimea sanjari na kutoweka kwa baadhi ya wanyama na mimea mbalimbali.

Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Tumbi iliyopo Wilayani Kibaha, Padri  Beno Kikudo amesema  kwamba wameamua kufanya maadhimisho hayo kwa kushirikiana na watoto wa shule ya St, John Bosco kwa lengo la kuwaelimisha juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira pamoja na kufanya  uzinduzi rasmi  wa klabu ya wanafunzi kwa ajili ya upandaji  wa miti  na kuitunzana kuilinda.

Kadhalika,  Padri Kikudo, amesema kwamba zoezi ambalo wamelifanya kwa ajili ya maadhimisho hayo litaweza kuleta mabadiliko makubwa katika suala zima la utunzaji wa mazingira na kwamba miti mbali mbali ambayo wameipanda wataitunza kwa lengo la kuweza kuboresha zaidi mazingira.

“Kikubwa kila mmoja wetu anao wajibu wa kutunza mazingira, ninawaomba wanafunzi ambao leo hii tumeweza kufanya uzinduzi kwa klabu maalumu ambayo itakuwa inasimamia masuala ya mazingira kuhakikisha kwamba wanailinda na kuitunza miti yote na kwamba kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake ili kusiwe na uharibufu wowote”Alisema Padri Kikudo.

No comments:

Post a Comment