Breaking News

Sep 23, 2020

MWANAMKE NI CHACHU YA MAENDELEO-SPIKA MSTAAFU WA TANZANIA

                                                 

Spika Mstaatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Anna Makinda

Na Mwandishi wetu

MWANAMKE hapa nchini  ana nafasi  kubwa ya  kuleta mabadiliko katika ngazi ya jamii kwa kujiamini na kuwa na moyo wa uthubutu katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, kwa hali hiyo wanawake wana mchango wa kusukuma maendeleo ya taifa.

Spika mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Anna Makinga amebainisha  hayo septemba 23,mwaka huu,2020 wakati akifungua mkutano wa baraza kuu la Jumuiya Vijana Wanawake  wa Kikristo(YWCA) mjini Morogoro.

Spika huyo mstaafu Anna,ambaye kwa sasa ni Mlezi wa Jumuiya ya Vijana Wanawake ya Kikristo,YWCA-Tanzania amesema kuwa Jumuiya hiyo ni ya kiulimwengu lakini kwa hapa nchini kinahitaji mabadiliko ya kimfumo ili kuendane na wakati kwa kuzitafutia ufumbuzi changamoto za wanawake zinazowakabili.

YWCA  ilianzishwa  kwa mara ya kwanza nchini Uingereza mnamo 1855, wakati vikundi viwili vilikutana kusaidia wanawake,kikundi kimoja kiliunda Umoja wa Maombi kuombea wanawake, na jingine lilianzisha nyumba za Kikristo kwa wasichana. Vikundi hivyo viwili viliungana mnamo 1877 na kuchukua jina la Jumuiya ya Vijana  Wanawake ya Kikristo.

Ametoa wito kwa viongozi wa Jumuiya hiyo kujitathmini na kuangalia changamoto zinazowakabili wanawake katika ngazi ya familia,kwenye uongozi na mahala pa kazi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Alitaja moja ya changamoto zinazowakabili wanawake ni magonjwa yasio ambukiza ikiwemo shinikizo la damu,saratani hali hiyo inaweza kukabiliwa kwa kubadili mfumo wa maisha katika ngazi ya familia.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk.Grace Soko alisema jumuiya hiyo inashughulikia kutatua changamoto zinazoikabili ni pamoja na mimba za utotoni na unyanyasaji wa kijinsia pamoja na kuwaunganisha vikundi wanawake(Vicoba) kwa kuwapa elimu ya ujasiliamali katika mikoa ya Arusha,Dar es Salaam na Shinyanga

Kwa upande wake,rais wa Jumuiya hiyo, Lois Mligula amesema YWCA licha ya uwepo wake lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya kutofikia maeneo mengi ya mjini na vijijini,hivyo katika mkakati waliokuwa nao ni kuhakikisha wanayafikia maeneo yote yakiwemo makundi ya walemavu na watu wanaishi katika mazingira magumu.

 

No comments:

Post a Comment