DC Same atafuta ‘Muarobaini’ Wanafunzi waliokwama kuripoti shuleni
Na Lilian Lucas.
MKUU wa Wilaya ya Same
mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameagiza wakuu wa shule kuwasilisha mara moja
majina ya wanafunzi ambao bado hawajaripoti shule kwa ajili ya taratibu
nyingine za kisheria.
Mkuu wa Wilaya Kasilda, alibainisha
hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa
kwenye vikao na walimu wakati wa ziara yake kufuatilia mwenendo wa kuripoti
kwenye shule walizopangiwa wanafunzi wa kidato cha kwanza wilayani humo.
“Kwenye hili la wanafunzi
ambao bado hawajaripoti, wakuu wa shule hakikisheni mnanipatia majina ya
wanafunzi wote tuanze ufuatiliaji lazima tujue walipo,”.alisema Kasilda.
“Binafsi sitaki kabisa kuona tukitajwa vibaya
kwenye Elimu, Same inachukua asilimia 40 ya eneo lote la mkoa wa Kilmanjaro kwa
ukubwa huo huo lazima tufanye pia makubwa kwenye elimu wakati nahangaika
kutafutia suluhu changamoto mlizonazo walimu pia mtimize wajibu wenu”.alisema Kasilda.
Minja Elias ni Mkuu wa
Shule ya Sekondari Kwakoko alibainisha mbele ya Mkuu wa wilaya kuwa asilimia
kubwa ya wazazi na walezi ni kama wamewatekeleza watoto wao kwani hakuna
ufuatiliaji.
“Unakuta mtoto haonekani
shule karibia wiki nzima, sisi tunachokifanya siku akija tunamwambia amlete
mzazi mzazi haonekani, ukimdadisi sana ndio unakugundua anaishi na Bibi ambae
ni mzee sana hata kutembea hawezi , na wazazi wake wanaishi maeneo mengine muda
mwingi mtoto anakua ndie mtafutaji”.alisema Minja Elius Mkuu wa shule ya
Sekondari Kwakoko.
Akiongea kwa niaba ya Walimu
wenzake Minja alisema pamoja na kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi kidato cha
kwanza wamekwisha ripoti baadhi yao ambao bado hawajulikani walipo ni wale
ambao wamekosa ushiriki wa moja kwa moja wa wazazi kwakua huishi na walezi hasa
Bibi zao ambao wenyewe pia hawajiwezi.
Kwa mujibu wa taarifa ya elimu
katika halmashauri ya Wilaya ya Same imebainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya
wanafunzi wa kidato cha kwanza wamekwisha ripoti shuleni,kwamba mpango wa sasa walionao ni kufuatilia wanafunzi
ambao bado hawajaonekana ingawa taarifa za awali zinaonesha wengi wao
wamehamishiwa shule nyingine.
Hata hivyo, imebainika kuwa baadhi ya wanafunzi hasa wa shule za Sekondari wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wanalazimika kutumia muda mwingi kwenye shughuli za utafutaji kwa kuelemewa na majukumu ya kutunza familia (Walezi wao) miongoni mwa sababu zinazochangia kudhorota kwa elimu kwakua hakuna ufuatiliaji wa karibu wa wazazi.
No comments:
Post a Comment