Na Catherine Sungura,Morogoro
MAKATIBU wa
afya nchini wametakiwa kusimamia nyenzo na rasilimali za kuendeshea huduma za
afya zilizopo kwenye maeneo yao ya
kazi kama ilivyo kwenye majukumu yao
kwani wao ni kioo na alama ya uendeshaji wa taasisi.
Hayo yamesemwa leo na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy
Gwajima wakati wa kufungua mkutano wa mwaka wa Chama Cha Makatibu wa Afya Tanzania (AHSATA) unaofanyika
mkoani Morogoro.
Dkt. Gwajima amesema
Makatibu wa afya lazima waelewe vizuri majukumu yao ili kuweza kusimamia na kuendesha taasisi zao
vizuri na hatimaye kupata mafanikio kwani
wao ndio watendaji wakuu katika kusimamia mifumo ya afya .
“Tunataka mifumo imara ya
afya na kuthamini jinsi Serikali ilivyowekeza kwenye mifumo hii ya afya"
alisisitiza Dkt. Gwajima.
“Hata hivyo aliwataka
makatibu hao kwenda kuisimamia kauli mbiu yao ya mwaka huu ambayo inasema,
"Uimarishaji wa mifumo ya afya ni nguzo muhimu katika usimamizi wa
rasilimali za sekta ya afya nchini” kuwa kutokana na kauli mbiu hiyo wanapaswa
kuwajibika na kujiongezea thamani ya kazi zao wao wenyewe na kuweza
kusimamia maslahi ya watumishi walio
chini yao.
Aidha, Dkt. Gwajima amesema
anatambua kada hiyo ndio pekee haina kurugenzi wizarani, hivyo kuagiza hilo
lifanyiwe kazi ya uchambuzi kuona kuna kipingamizi gani kinachozuia hilo iwapo
ni jambo lenye tija?
‘’Lazima tubadilike na
tuondoe dhana ya uongozi kwenye afya lazima mtu
awe kada ya utabibu 'Medical Doctor andaeni kongamano litakalojadili
hili,kwani mimi nilipokuwa DMO hata RMO
nilifanikiwa kwa kusaidiwa na kada zingine,hivyo Muuguzi au taaluma
nyingine ya afya anaweza kuongoza
taasisi ya afya maana huo ni uongozi na siyo kazi ya taaluma maalumu’.
Aliongeza kuwa taasisi
itakua na mafanikio endapo katibu wa afya atakua imara na taasisi haitofanikiwa
endapo katibu wa afya atakua legelege hivyo lazima kada hiyo isimamie majukumu
na kujiamini ili kuweza kuzifanya taasisi kuwa imara.
Pia Dkt. Gwajima amewataka
Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwapatia fursa na uhuru wenye kuzingatia
sheria makatibu wa afya ili kuweza kutekeleza majukumu yao.
Upande wa nidhamu, Waziri huyo aliwataka wanaporudi kwenye vituo vyao wakasimamie nidhamu kwani haitapendeza kuona taasisi wanazozisimamia zinafeli wakati wao ni watendaji wakuu ndani ya sekta ya afya.
Suala la Dawa na kadi za kliniki, Waziri huyo amesema anaona bado Kuna makosa yanaendelea kutokea licha ya kutoa tamko kwa baadhi ya vituo vya afya kuacha kuuza kadi hizo hivyo amewataka wasimamie hilo.
Awali akimkaribisha Waziri wa afya, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mh. Albinus Mugonya amewataka makatibu hao kuzingatia miongozo iliyopo katika utoaji wa huduma za afya zinazostahili na kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na ubunifu hivyo kutoa huduma bila upendeleo na kuwajibika kwa umma na kwa kuzingatia miiko na maadili ya taalumma zao.
Naye, Rais wa AHSATA Daniel Muhochi amesema katika mkutano huo watajadili na kubadilishana uzoefu na changamoto wanazokabiliana nazo na kutoka na njia ni namna gani wanaweza kuzitatua.
Muhochi aliomba ridhaa kwa
wizara ili kada hiyo kuwa na baraza la taaluma litakalokuwa linashughulikia
maadili kuweza kuboresha huduma za afya
sehemu zao za kazi.
No comments:
Post a Comment