WAZIRI KALEMANI: WATANZANIA WANAJINYANYAPAA KUINGIZA UMEME MAJUMBANI
Lilian Lucas, Morogoro
WAZIRI wa
Nishati Dk Medard Kalemani amesema watanzania wengi wamekuwa wakijinyanyapaa
wenyewe katika suala zima la kuingiza umeme kwenye nyumba zao.
Waziri Dk kalemani alisema
hayo jana wakati wa Uzinduzi wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya tatu Mzunguko
wa Pili kimkoa uliofanyika kitongoji cha Muheza Ititu wilayani Gairo.
Alisema kwa sasa Serikali
inamtaka kila mtanzania mwenye nyumba popote alipo atumie umeme, na kwamba
imeendelea kuhamasisha kuingiza umeme majumbani bila kujali aina ya nyumba.
“Gharama za kuingiza umeme
kwa wananchi kwa sasa imepunguzwa kwenye maeneo yote ni sh 27,000 sasa
unashindwaje kuingiza umeme, umeme sasa ni lazima kwa kila mtanzania na si
jambo la hiari,”alisema waziri Dk Kalemani.
Aidha waziri huyo alisema
Serikali haitaacha eneo hata moja
kufikisha umeme kwani kazi ya umeme ni kuongeza thamani ya mazao na
kwenye Kilimo umeme una kazi kubwa ikiwemo usindikaji wa mazao hivyo viwanda vinatakiwa kuanzishwa
kwa wingi.
Waziri Dk Kalemani
aliwataka wananchi hususani vijana kuchangamkia fursa ya uwepo wa umeme kwenye
maeneo yao kwa kuanzisha biashara na kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao.
Akizungumza na wananchi wa
kitongoji cha Muheza Ititu kijiji cha Kisitwi kata ya Rubeho wilayani Gairo
alisema mpaka kufikia Desemba Mwaka 2022 Tanzania itaandika historia kwa vijiji
vyote kupata umeme na kuungana na mataifa mengine.
“Mpaka sasa vijiji 10,312
vina umeme na vilivyobaki ni 1,956 ambavyo vitapelekewa katika awamu hii
mzzunguko wa pili, kwa Morogoro vijiji vyenye umeme ni 440 kati ya
673,”alisema.
Alisema kwa kutambua
umuhimu wa Umeme Serikali imetenga takribani sh 66.8 bilioni kwa mkoa wa
Morogoro ili kuhakikisha vijiji 233 vilivyosalia vinapatiwa umeme.
Mmbunge wa Jimbo la Gairo
Ahmed Shabiby alisema pamoja na Waziri huyo kufika katika wilaya hiyo zaidi ya
mara saba, alimuomba Waziri Dk Kalemani kuleta Gari la meneja wa shirika la
Umeme (TANESCO) wilaya ya Gairo ili
aweze kutembelea maeneo korofi ambayo yamekuwa kufikika kwa taabu.
Aidha Shabiby alimuomba
waziri huyo kuvifikia vijiji kwenye halmashauri nyingine ambazo vijiji vyao
havijafikiwa ili mkoa wote wa Morogoro uweze kuwa na umeme na kuweza kuzalisha
kwa wingi mazao mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro
Martine Shigela alisema kukosekana kwa umeme kunachangia uzalishaji wa mazao
kuwa mdogo, hivyo upatikanaji wa umeme kutaongeza uanzishwaji wa viwanda kwenye
wilaya.
Shigela aliwataka wataalamu
kwenye halmashauri za wilaya kutenga muda wa kuwatembelea wananachi pindi umeme
unapopelkwa kwenye maeneo ya wananchi kwani kuwepo kwa umeme kunaleta tija.
No comments:
Post a Comment