VICTOR MASANGU, GOBA
BAADHI ya
shule za awali na msingi zilizopo katika Manispaa ya Ubungo jijini Dar es
Salaam zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu chakavu ya
madarasa, upungufu wa madawati,pamoja na matundu ya vyoo hivyo kupelekea
wanafunzi kusoma katika mazingira ambayo sio rafiki na wengine kukaa chini
kutokana na mlundikano.
Katika kuliona hilo, uongozi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Organization for Community Development (OCODE) limeamua kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kuamua kutoa msaada wa madawati, meza pamoja na kuwajengea darasa moja la elimu ya awali katika shule ya msingi goba ili kuondokana na usumbufu wanaoupata wanafunzi hao.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi madawati na darasa hilo,
Mwakilishi kutoka Shirika la Ocode, Digna Mushi ambaye alimwakilisha mkurugenzi
mtendaji, alibainisha kwamba, kwa sasa wanatekeleza mradi katika shule za
msingi nne zilizopo katika manispaa ya Ubungo na kwamba lengo kubwa ni
kuwasaidia wanafunzi waweze kupata elimu ambayo ni jumuishi.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo George Maiga aliyeshika mkasi akikata utepe rasmi kuashiria uzinduzi rasmi wa daraja jipya la wanafunzi wa awali katika shule ya msingi Goba Jijini Dar es Salaam
“Leo tupo hapa kama shirika la Ocode na mimi nipo kwa niaba ya
Mkurugenzi mtendaji,tunatekeleza mradi huu kwa shule mbalimbali na leo
tunakabidhi darasa moja ambalo limeshakamilika”
Aidha,Alisema kuwa darasa hilo, limejengwa maalumu kwa ajili ya
wanafunzi wa awali katika shule ya msingi goba na kutoa madawati,pamoja na meza
za walimu katika kuhakikisha kwamba tunaboresha sekta ya elimu katika shule za
awali na msingi.
Kaimu huyo Mkurugenzi, alibainisha kuwa shirika lake wameshatoa
misaada mbalimbali katika shule za msingi ikiwemo kuwasaidia katika ujenzi wa
miundombinu ya madarasa pamoja na kuwapatia madawati, pamoja na meza kwa ajili
ya walimu ili kuweza kufikia malengo ambayo wamejiwekea ya kuwasaidia
watoto wa rika mbalimbali ikiwemo walemavu.
Kadhalika, alifafanua kwamba katika utafiti ambao tayari
wameshaufanya katika baadhi ya shule zilizopo katika manispaa ya ubungo
wameweza kubaini kuwepo kwa watoto 62 ambao wana mahitaji maalumu na kwamba
tayari baadhi yao wameshapatiwa msaada katika awamu ya kwanza na wengine
wataendelea kupatiwa sapoti kulingana na mahitaji yao husika ikiwemo kuwapatia
vifaa maalumu.
“katika shule hii ya msingi Goba sisi kama shirika tulibaini
kuwepo kwa changamoto mbali mbali hivyo kwa kuanzia tumeona tutoa mchango wetu
kwa kuwajengea darasa moja watoto awali, madawati, viti, pamoja na meza bila
kusahau vifaa mbali mbali amabvyo vitatumika kwa ajili ya kuwafundishia
wanafunzi waweze kuelewa vizuri pindi wanapokuwa darasani,”alisisitiza.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Goba ,Ambrose Mwakimbwala
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Goba Ambrose
Mwakimwala ametoa pongezi zake za dhati kwa shirika la Ocode kwa msaada huo wa
kuwajengea darasa na kuwapatia madawati ambayo yatakuwa ni mkombozi mkubwa
zaidi katika kuwasaidia wanafunzi kuondokana na changamoto ya kukaa chini na
wengine kusoma wakiwa katika hali ya mlundikano.
“Kwa kweli nipende kutoa shukrani zangu mimi kama mwalimu Mkuu
kwa shirika hili la Ocode kwa kutupatia msaada huu ambao utaweza kuleta matokeo
chanya kwa wanafunzi wetu ambao hapo aawali walikuwa wanakabiliwa na changamoto
katika suala zima la kukaa chini hivyo nina imani kwa kuanzia hatua hii itaweza
kuwafanya wasome katika mazingira ambayo ni rafiki.
Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo,
George Maiga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alibainisha
kwamba shirika la Ocode limeweza kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kwa hali
na mali kuboresha sekta ya elimu hivyo watakuwa tayari kushirikiana bega kwa
bega katika kuzitatua changamoto za wanafunzi zinazowakabili hasa katika
miundombinu ya madarasa.
Nao, baadhi ya wazazi na walezi ambao walifika katika hafla hiyo
ya makabidhiano walisema kwamba wana imani kubwa na shirika hilo la Ocode kwa
kuweza kuwawezesha vifaa mbali mbali vya kuwafundishia watoto wao na kwamba
kutaweza kupunguza kwa kiasi Fulani changamoto ya kusoma wakiwa katika hali ya
mlundikano madarasani.
Wadau mbali mbali wa maendeleo katika sekta ya elimu pamoja na viongozi wa serikali wakiwa wanasalimiana na kujadiliana mambo ya elimu jumuishi katika hafla hiyo ya makabidhiano ya darasa moja ambalo limejengwa kwa ufadhili wa shirika la Ocode.
Shirika lisilokuwa la kiserikali la Ocode limekuwa likiendesha miradi
yake mbali mbali katika Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es Salaa ikiwemo mkradi
ya elimu ambayo imeweza kuzigusa shule nne zilizopo katika kata mbali mbali
lengo ikiwa ni kutoa elimu jumuishi ikiwa sambamba na kuwajengea madarasa,
pamoja na kuwapatia madawati, viti na meza ili kuboresha sekta ya elimu.
No comments:
Post a Comment