Breaking News

Dec 13, 2020

NIC YATOA MIL.23 KUWAFIDIA WAKULIMA WALIOATHIRIWA NA MAJANGA YA KILIMO


                   Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,Gerald Kusaya
Na Thadei Hafigwa 

SHUGHULI za kilimo hapa nchini zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo milipuko ya magonjwa ya mimea na visumbufu,ukungu ,mafuriko na ukame.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,Gerald Kusaya alibainisha hayo mjini Morogoro katika halfa ya malipo ya fidia kwa wakulima 32 kupitia shirika la bima la taifa(NIC) na kuongeza kuwa changamoto hizo zimekuwa zikiathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kilimo na kusababisha wakulima kupata hasara.

Kusaya alisema kuwa katika kipindi cha msimu uliopita wakulima 32 kutoka maeneo mbalimbali nchini walikatia bima shughuli zao za kilimo kupitia NIC lakini mashamba yao yaliathiriwa na majanga mbalimbali.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,Gerald Kusaya katikati akiwa katika picha ya pamoja na  Baadhi ya wakulima  waliosimama safu ya nyuma katika fhafla fupi ya  malipo ya fidia kwa wakulima waliopata hasara katika shughuli za kilimo baada ya kukatia bima ya kilimo.

“ninatoa wito kwa wakulima wote hapa nchini kukata bima ya mazao ili iwakinge na kuwapa uhakika na usalama wa shughuli za kilimo,tembeleeni ofisi za shirika la Bima la Taifa(NIC) zilizopo mikoa yote nchini kupata huduma ya bima ya kilimo”Alisema Katibu Mkuu.

Awali,Katibu Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC),Dk.Elirehema Doriye akitoa taarifa ya mfumo wa bima ya Kilimo kwamba,shirika la bima linauzoefu katika endeshaji shughuli za bima kwa wananchi toka ilipoasisiwa  miaka 52 iliyopita.

Baadhi ya wakulima walioshiriki katika hafla fupi ya malipo ya fidia ya hasara zilizotokana na shughuli zao za kilimo katika msimu uliopita.

Dk.Doriye alisema kuwa Bima ya kilimo imewanufaisha wakulima 562 kote nchini kati ya hao wakulima 32 waliopata hasara kutokana na shughuli zao za kilimo lakini kwa kuwa walijiunga na bima ya kilimo watapatiwa fidia kiasi cha shilingi milioni ishirini na tatu(23).

Jumla ya wakulima watano kutoka Wilaya ya Mvomero wakipokea malipo ya fidia kwa niaba ya wanzao,Mmoja wa wakulima walionufaika na mfumo huo, Kassim Said kutoka kijiji cha Mvomero,Wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro alitoa shukrani kwa wizara ya Kilimo,Shirika la bima la taifa(NIC) kwa kuanzisha bima ya kilimo ambayo inawafanya wakulima kuendesha shughuli zao wakiwa na uhakika wa usalama wa afya zao na kilimo ikiwa ndio chanzo kikuu cha mapato yake.


Katibu mkuu wa wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya ( kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi ya Sh milioni 23 mkulima wa wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Dorica Mlacha ( kulia mwenye ushungi) kwa niaba ya wenzake  31 kutoka wilaya tofauti hapa nchini ambao walikata bima ya shughuli zao za kilimo kupitia Shirika la Bima ya Taifa (NIC) ikiwa ni  kuwafidia harasa ya mazao yao  kutokana na majanga mbalimbali waliokumbana nayo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 na ( wapili kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dk Elirehema Doriye.

Hivi karibuni serikali ilitoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa ya bima ya kilimo ya mazao,hali hiyo imelezwa kuwawezesha wakulima wengi kutumia huduma ya bima ya mazao.

No comments:

Post a Comment