Breaking News

Feb 9, 2021

MWENYEKITI 'MSTAAFU' MKULANGA AKUTWA NA HATIA KUPOKEA RUSHWA

 

SEHEMU YA JENGO LA MAHAKAMA YA WILAYA YA MKURANGA,MKOA WA PWANI

MWENYEKITI 'MSTAAFU' MKURANGA AKUTWA NA HATIA KUPOKEA RUSHWA

NA MWANDISHI WETU, MKURANGA

ALIYEKUWA Mwenyekiti katika kipindi kilichopita wa halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Juma Abeid amehukumuwa kwenda Jela kwa makosa ya kupokea rushwa kinyume na sheria na taratibu za nchi.

Kwa mujibu wa taarifa, imetolewa na Taasisi  ya  Kuzuia na Kupambana na Rushwa Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani,  imeeleza kuwa  mnamo mwezi Novemba mwaka  2019 ilifungua mashitaka ya kuomba na kupokea rushwa dhidi ya mshitakiwa Juma Abeid, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mkuranga  kabla ya  kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa Viongozi wa mwaka 2020.

 Kesi hiyo  ambayo iliendeshwa  katika mahakama ya hakimu mkazi  Wilaya ya Mkuranga,  mkoa wa Pwani, mbele ya hakimu mkazi  Erieth Mwailolo .

Awali  ilidaiwa  kwamba Mshitakiwa alitenda kosa la kupokea hongo ili kumsaidia mwananchi (jina limehifadhiwa) ambaye alikuwa anahitaji uhamisho wa mke wake anayefanya kazi ya Ualimu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara kwenda Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Pia, ilidaiwa  mshitakiwa aliomba na kupokea  kiasi cha Shilingi Laki mbili na elfu ishirini (Sh. 220,000/=)  ili kuwezesha  kufanyika kwa  uhamisho huo kwenda Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga ambayo yeye alikuwa anaiongoza kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo. Kitendo hiki ni kosa chini ya kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11 ya Mwaka 2007.

Hukumu ya kesi hiyo, ilisomwa na hakimu mkazi Mheshimiwa Erieth Mwailolo mnamo tarehe 08 Februari, 2021 ambapo Mwenyekiti huyo wa Zamani Juma Abeid alihukumiwa kwenda jela miaka minne (4) au kulipa faini ya Shilingi laki saba (Sh.700,000/=) kwa kila kosa.

 Mshitakiwa alikubali kulipa faini ya  shilingi Milioni Moja na laki Nne (Sh. 1,400,000/=) na kuachiwa huru.

Awali, Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU, Naftal Mnzava alimwomba mheshimiwa hakimu kutoa adhabu kali dhidi ya mshitakiwa ili iwe fundisho kwa viongozi wengine wanaojihusisha na rushwa.

Wakati huo huo,mnamo tarehe 08 Februari, 2021, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Pwani ilimfikisha mahakamani,Gidman Bishinwa Athanas, mtumishi wa Mamlaka ya Maji safi na Maji taka (DAWASA), Mkoa wa Pwani kwa makosa ya kuomba na kupokea Rushwa kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na:11 ya mwaka 2007.

Mtuhumiwa huyo aliomba rushwa ya Shilingi laki mbili na elfu hamsini (Sh. 250,000/=) kutoka kwa mwananchi mkazi wa Kibaha (jina limehifadhiwa) ili mshitakiwa asiingize deni la matumizi ya maji analodaiwa kiasi cha Shilingi laki tano (Sh. 500,000/=) kwenye mfumo wa malipo ya maji wa DAWASA.

Hata hivyo, baada ya kusomewa mashitaka mtuhumiwa huyo alikiri kutenda kosa mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama ya wilaya Kibaha Mhe. KIBONA na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini kiasi cha Shilingi laki tano (Sh. 500,000/=) ambapo mtuhumiwa alilipa faini na kuachiwa huru.

Aidha,Mkuu  wa Takukuru, Mkoa wa Pwani, Suzana Raymond  amewaasa watumishi wa mkoa huo,  wenye dhamana ya kutoa huduma kwa jamii kuzingatia misingi ya uadilifu katika utendaji wao wa kazi,  kwani vitendo vya Rushwa katika kazi vinasababisha huduma kutolewa chini ya viwango na kwa upendeleo kinyume na malengo ya serikali.

No comments:

Post a Comment