DAS BAGAMOYO AHIMIZA WADAU ‘KU-SAPOTI’
BAGA FRIENDS
NA MWANDISHI WETU, BAGAMOYO
KATIKA
kuunga juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kukuza sekta ya michezo, hususan
mchezo wa soka, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni amewaomba
wadau mbalimbali wa michezo kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuisaidia kwa
hali na mali timu ya soka ya ‘Baga friends’ ambayo ndio mabingwa wa ligi
ya soka daraja la tatu ngazi ya Mkoa wa Pwani ili ifanye vizuri katika hatua ya
ligi ya mabingwa wa Mkoa ngazi ya Taifa.
Mgeni ametoa rai hiyo, wakati alipotembelewa na baadhi ya
viongozi wa Chama cha soka Wilaya ya Bagamoyo (BFA), Ofisini kwake pamoja na
kamati ya utendaji ya timu hiyo ya ‘Baga friends’ kwa ajili ya kuweza kuweka
mikakati ambayo itawesa kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri katika hatua
nyimgine inayofuata ya ngazi ya Taifa.
“Lengo la kukutana na viongozi hawa wa mpira wa miguu ambao
wamekuja ofisini kwangu wakiongozwa na Mwenyekiti wa BFA tuweze kujadili
na kuweka misingi imara ambayo itawasaidia wachezaji wetu ambao wamepigana kufa
na kupona katika kipindi chote na kufanikiwa kuwa mabingwa wa ligi daraja la
tatu ngani ya Mkoa wa Pwani kwa hivyo tunapaswa kuwapa sapoti ya ina yake”.Alisema
Katibu Tawala huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa wa baraza la
michezo Wilaya Bagamoyo, alifafanua kuwa timu hiyo kwa sasa ipo katika
maandalizi ya kujianda na ligi ya mabingwa ngazi ya Taifa, hivyo serikali
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo inabidi tunaweka mipango
madhubuti ya kuhakikisha kwamba tunaweza kufika mbali zaidi na kupanda daraja
la pili na hatimaye katika siku zijazo tuweze kushiriki katika ligi kuu ya
Tanzania bara.
“Hii timu imeweza kuutwaa ubingwa wa ligi daraja la tatu ngazi
ya Mkoa wa Pwani kwa hivyo kwa sasa inawakilisha Mkoa wa Pwani kwa ujumala japo
inatokea Wilaya ya Bagamoyo, kitu kikubwa ninachowaomba wadau wote kwa pamoja
tuungane na kutoa michango yetu ya fedha ambazo zitaweza kutumika katika
mahitaji mbali mbali ya chakula kwa wachezaji pamoja na mambo mengine ya msingi
kama mipira na jezi hivyo ninawaomba sana na nia yetu tushiriki ligi kuu ya
Tanzania bara katika siku ya baadae,”alifafanua mgeni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha soka Wilaya ya Bagamoyo
(BFA), Olnjilie Maliwa, alisema kwamba lengo kubwa na kwenda kumtembelea
katibu Tawala wa Wilaya hiyo juu ya timu yao ya soka ya baga friends ambayo
imefanikiwa kuutwaa ubingwa wa ligi daraja la tatu, katika ngazi ya Mkoa wa
Pwani ili kuweza mikakati ambayo itasaidia kuweza kufika mbali zaidi katika
hatua nyingine.
“Mimi kama Katibu wa BFA tumeweza kuongozana na uongozi wa
kamati ya utendaji ya mabingwa wetu wa soka katika ligi daraja la tatu ambao ni
timu ya ‘Baga friends’ tukae kwa pamoja ili tuombe kituo ambacho kitatumika kwa
ajili ya michuano ya Taifa na lengo letu ni kuhakikisha timu hii inaweza
kufanya vizuri na kufika hatua ya ligi daraja la pili katika msimu
unaokuja”alisema Mwenyekiti huyo.
Aidha, Katika hatua nyingine alimpongeza kwa dhati Katibu Tawala
wa wilaya ya Bagamoyo, kwa kuwa bega kwa bega katika kipindi chote cha michuano
iliyopita hadi wameweza kufanikiwa kuibuka na ubingwa katika ligi hiyo daraja
la tatu ngazi ya Mkoa wa Pwani na kuwaomba wadau wengine wa soka katika maeneo
mbali mbali kujitokeza kwa wingi ili kuipa sapoti ya kutosha timu yao ambayo
ndio pekee inawakilisha Mkoa wa Pwani.
No comments:
Post a Comment