Mtafiti wa Magonjwa na Visumbufu vya zao la Korosho Dk Wilson Nene,kutoka TARI Naliendele,kulia akiwafundisha wakulima wa korosho kutoka wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma (kushoto) jinsi ya kubaini na kudhibiti magonjwa yanayoshambulia zao hilo,(PICHA NA ASHTON BALAIGWA,DODOMA)
Na
Ashton Balaigwa,Dodoma
TANZANIA
imeanza kujipanga kwa ajili ya kuliteka soko la Afrika la korosho kutokana na
kuzalishaji korosho bora kuliko nchi nyingi za Afrika na Duniani.
Hatua hiyo inatokana na Tanzania kuwa ndio nchi
iliyozifundisha kilimo cha korosho nchi za Afrika ikiwemo za Ivory Coast
na Naigeria, ambazo kwa sasa zinafanya vizuri na zinaongoza kwa kuzalisha
zao hilo Afrika.
Kutokana na hali hiyo sasa Tanzania imeanza mkakati wa kuanza
kuongeza uzalishaji wa zao hilo hapa nchini kwa kuwafundisha wakulima wa zao la
korosho katika mikoa 17 hapa nchini ili kuliteka soko la hilo kutokana na
kuzalisha korosho bora kuliko nchi hizo.
Mtafiti kutoka Taasisi
ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI), Kituo cha Naliendele kitengo cha Agronomia
ya Korosho, Kasiga Ngiha, aliyasema kwenye mafunzo ya wakulima wa korosho
kutoka Halmashauri za Kongwa na Mpwampwa mkoani Dodoma.
Alisema takwimu ambazo
zimepatikana kutoka mtandao wa Kilimo forum.com zinaonyesha kuwa Tanzania nchi
ya nne kwa nchi Afrika kwa kuzalisha korosho ikitanguliwa na Nigeria
inayoongoza kwa kuzalisha tani za ujazo laki tisa kwa mwaka ikifuatiwa na Ivory
Coast inayozalisha tani za ujazo laki sita.
Alisema nchi ya Tatu kwa
kuzalisha Korosho barani Afrika ni Guinea Bissau inayozalisha tani za ujazo
laki nne kwa mwaka ambapo Tanzania inazalisha tani za ujazo laki tatu kwa
mwaka.
“Tunajisikia vibaya
kuzifundisha nchi hizi kilimo cha korosho kisha wanakwenda kulima na kuzalisha
kwa wingi kuliko sisi, ndio maana sasa tumeamua kusambaza elimu kwa wakulima
wetu ili na sisi tuongeze uzalishaji,” alisema Kasiga.
Akitoa elimu ya kilimo bora cha korosho kwa wakulima wa wilaya
hizo ,Mtafiti wa Magonjwa na Visumbufu vya zao la Korosho Dk Wilson
Nene,alisema sababua inayopelekea kuwepo kwa uzalishaji mdogo wa zao hilo hapa
nchini ni pamoja na wakulima wamekuwa wakitumia mbegu za kienyeji.
Alisema tayari TARI Naliendele wameanza kuwafundisha
wakulima kutumia mbegu bora za kisasa aina 54 zinazozalishwa na
TARI Naliendele zenye uwezo wa kuzalisha mti mmoja zaidi ya kilo 20 tofauti na
mbegu za kienyeji zinazotoa kilo 11 .
Alisema pamoja na hayo wameshawafundisha njia za
kudhibiti magonjwa na visumbufu vya korosho kwa kutumia njia kuu tatu ikiwemo
njia ya asili ikiwemo kufanya usafi katika shamba,kupanda kwa
nafasi na kupunguzia matawi yasiyo faa ili kusaaidia kutengeneza njia
rafiki ya vimelea vingi vinavyoleta athari za magonjwa.
Naye Mratibu wa zao la korosho kutoka TARI Naliendele Dk
Geradina Mzena,alisema sasa wamekuja na mikakati mipya ya kutekeleza agizo la
Serikali la kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 315,000 na kufikia tani
milioni moja kwa kuwapa wakulima mbinu za kisasa za kilimo hicho pamoja na
kutumia mbegu bora za kisasa katika mikoa 17 hapa nchini.
No comments:
Post a Comment